Monday, February 5, 2007

Vita fupi zaidi



VITA FUPI ZAIDI YA MAPINDUZI DUNIANI, JANUARU 12, 1964

Na William Shao


KISICHOJULIKANA sana katika historia hadi karne ya 20 ni kwamba vita vifupi zaidi vya mapinduzi ni vile vya Zanzibar vilivyodumu kwa saa chache tu na hatimaye kufanikisha lengo lake. Hayo yalitokea usiku wa kuamkia Januari 12 1964.

Hali ya kisiasa Zanzibar ilikuwa ikizorota tangu kifo cha Sultani Khalifa kilichotokea Oktoba 9, 1960. Khalifa alikuwa ameitawala Zanzibar kama Sultan tangu Desemba 9, 1911.

Chaguzi za mseto zilipofanyika mwaka 1961, vyama vikuu vya Zanzibar, kila kimoja, vilishindwa kujipatia wingi wa kura. Hatimaye, mwaka 1963, Waingereza waliondoa majeshi yao. Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar Desemba 10, 1963, aliashiria kuondoka kwa Gavana wa mwisho wa Kiingereza huko Zanzibar, na huo ukawa mwisho wa ukoloni wa Uingereza.

Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa 1963 ulikipa ushindi finyu muungano wa vyama viwili ZNP na ZPPP. Lakini taifa hilo lililokuwa mwanchana kamili wa Jumuia ya madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.

Mashambulizi ya kuipindua Serikali ya Sultan yalianza Januari 11 kuamkia Januari 12, 1964. Yalianza Jengo la polisi la Ziwani kwa ukataji wa nyaya za seng’enge. Ingawa baadhi yao waasi walianza kuogopa walipoanza kukata nyaya hizo, walipeana moyo kwamba ikiwa hili lingeshindwa, wangekamatwa na kuuawa.

Ilikuwa ni bora zaidi kwao kufa katika mapambano kuliko kushindwa kisha wakauawa na serikali. Kwa hiyo, walielezana kuwa ni afadhali kuhakikisha kuwa hili linafanikwa ama kwa kufa au kwa kupona kuliko kuacha lishindwe halafu tuuawe.

Askari wa zamu waliokuwa wakilinda kituo hicho walishtuka. Wakaanza kujibu mashambulizi mazito yaliyoelekezwa kwao. Mlango wa mbele ulifunguliwa, lakini wakati huo askari wa serikali ambao walikuwa wamelala ghorofani katika jengo hilo waliamka ghafla na kuteremka haraka haraka.

Kiasi cha askari 40 wa serikali walishambuliana na askari wa wanamapinduzi, ambao wengi wao walikuwa wakitumia pinde na mishale pamoja na mawe ili kuwazuia polisi hao wasiteremke kutoka ghorofani wakati wengine wakivunja ghala la silaha.

Bunduki aliyoichukua kiongozi wa mapinduzi hayo, John Okello, kutoka kwa askari mmoja aliyekuwa zamu kituoni hapo ilikuwa imebakiwa na risasi tatu tu, na hiyo ndiyo iliyokuwa silaha ya kwanza ya kisasa waliyokuwa nayo katika Mapinduzi yao, na ilikuwa muhimu mno kwa sababu iliwapa faida katika zile dakika chache za kwanza.

Katika hali ya kuchanganyikiwa, polisi walianza kubonyeza ving’ora na kupiga tarumbeta na kuwarushia waasi mabomu ya kutoa machozi. Lakini kwa kuwa kundi la Okello lilikuwa na askari ambao waliwahi kufanya kazi katika baadhi ya vituo hivyo, waliweza kukata nyaya za ving’ora hivyo na kuvinyamazisha. Waliweza pia kukabiliana na mabomu ya machozi kwa kuyasokotea katika mashati yao na kuwarushia polisi hao.

Kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo, Okello aliipiga risasi tarumbeta iliyokuwa ikipulizwa na mmoja wa polisi hao, ikaanguka sakafuni. Wakitumia mashoka, nyundo, mapanga na vifaa vingine vya kuvunjia nyumba, hatimaye askari wa Okello walifanikiwa kuvunja ghala la silaha.

Mpaka walipovunja ghala hilo, nusu ya wale polisi 40 walikuwa ama wameuawa au wamejeruhiwa na waliobakia walilazimika kujisalimisha hata kabla silaha na zana nyingine za kivita hazijaanza kugawanywa askari wa Okello kutoka ghalani.

Kikosi cha wapiganaji 200 cha serikali kiliwasili katika eneo hilo saa 10:30 usiku, lakini baada ya mapigano ya saa nzima hakikufua dafu. Ilipofika saa 11:30 asubuhi wengi wa wapiganaji wa serikali walikuwa tayari wameuawa, wangine wakiwa wamejeruhiwa na wengi walikimbia.

Okello alidai kuwa Ziwani lilikuwa ni eneo la kwanza kutekwa, lakini kuna waandishi walioandika kuwa Mtoni ndilo eneo la kwanza kutekwa. Baada ya kituo cha Polisi cha Mtoni kutekwa, ambacho hakikuwa na ulinzi mkali kama kile cha Ziwani, askari wa Okello walikamata bunduki 200 za kawaida, Sub Machine-Gun 20, mabomu ya kutupwa kwa mkono pamoja na mabomu ya kutoa machozi.

Ingawa Haji alijeruhiwa wakati wa utekaji wa kituo hicho, alituma ujumbe wa mafanikio na hongera kwa Okello ambaye alitembelea kituo hicho cha polisi kabla hajaenda katika kituo cha redio ambako alimkuta fundi mitambo wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akijiandaa kutoa matangazo yake na kumlazimisha kwa mtutu wa bunduki kutangaza aliyotaka yeye (Okello) yatangazwe.

Kukamatwa kwa kituo cha redio kulikofanywa Mzee Mohamed na kundi lake la askari 100 waliounda kundi la pili, ‘2nd Battalion’, kulikuwa ni kwa mafanikio makubwa. Wanamapinduzi sasa wangeweza kutangaza mapinduzi yao. Sasa wangeweza kuiambia dunia kuwa wamekwishateka nchi. Njia pekee ya matangazo ambayo serikali ilikuwa imebakiwa nayo ni simu.

Katika kituo cha Polisi cha Ziwani ndipo palikuwa na ghala za silaha za polisi. Kwa mujibu wa kitabu Conflict and Harmony in Zanzibar, polisi wa zamu walikuwa na bunduki na kila moja ilikuwa na risasi tano.

Wakati fulani usiku wa manane Mrakibu wa Polisi, Durham, ambaye alikuwa Mwingereza, aliwapitia walinzi hao, akachukua risasi za walinzi hao na kuziweka kwenye kikapu alichoondoka nacho.

Ali Muhsin, katika kitabu hicho, anadai kuwa muda mfupi baadaye kituo cha Polisi Ziwani kilianza kushambuliwa kwa mishale na bunduki, na ghala lake la silaha likavunjwa.

Baadhi ya askari waliokuwa na bunduki, lakini hawakuwa na risasi, waliuawa, na wengine wakakimbilia vichakani. Muhsin anadai kwamba mmoja wa askari hao, ambaye alikuwa akifanya kazi ya kumpelekea habari, walitiwa pamoja kizuizini huko Dodoma.

Anadai kwamba hata polisi wengine waliokuwa kituo cha Ziwani walimwambia habari hizo hizo na kwamba maofisa wote wa polisi wa Kiingereza waliondoka na familia zao kutoka katika kituo cha Ziwani bila kuguswa, wakati polisi wa Unguja wakichinjwa.

“Kweli kweli katika muda wote wa ‘mapinduzi’ ambao maelfu ya watu weusi na watu wa rangi ya kahawia wakiuawa, kulemazwa na kubakwa, watu wa rangi nyeupe hawakuguswa,” alidai Muhsin.

Majira ya saa moja asubuhi ya Jumapili, Januari 12, Okello alianza kutoa moja ya matangazo yake. Aliwatisha Waarabu. Alisema: “Amkeni ninyi mnaojiita wafalme, hakuna tena serikali ya kifalme katika kisiwa hiki. Sasa hii ni serikali ya wapigania uhuru. Amkeni nyie watu weusi, na kila mmoja wenu abebe bunduki na zana za vita na kuanza kupigana.”

Baada ya kutangaza hivyo John Okello aliondoka katika studio za redio kisha akaenda katika gereza la Mazizini akiwa na kundi lenye silaha walizokamata kutoka katika maghala ya polisi na kuamuru mashambulizi yafanyike majira ya saa nne asubuhi.

Matokeo ya mashambulizi hayo ni kwamba katika muda usiozidi dakika 30 wapiganaji wa Okello waliyakamata majengo yote ya gereza hilo, baadhi ya majengo mengine yalichomwa moto.

Hakukuwa na upinzani mkubwa. Walinzi wa gereza hilo walikuwa na silaha lakini hazikuwasaidia sana. Wakati hili likitokea Mazizini, Okello alipata habari kwamba Waarabu wa Kimanga wameanza kuwaua Waafrika katika maeneo ya vijijini, kwa hiyo aliwagawanya wapiganaji wake kwenda kuwashambulia Wamanga hao na wengine wote waliobakia katika kituo cha polisi cha Malindi.

Baadhi ya wafuasi wa Okello walianza kuteka nyara maduka ya Wahindi na Waarabu katika eneo la Darajani na kwingineko. Katika maeneo kadhaa watu walikuwa wakiuawa ovyo. Waingereza hawakuwa wakiuawa kama Waarabu, lakini walikuwa wakipigwa kwa mawe.

Saa moja asubuhi Sultan alipanga safari ya haraka ya kuondoka Zanzibar. Alitumia meli ya serikali iliyojulikana kwa jina la Salama iliyokuwa imetia nanga bandarini. Muda mfupi baadaye aliwasili bandarini tayari kuondoka, huku akiwa chini ya ulinzi mkali ukiwa katika msafara wa magari matatu.

Maofisa wa Uingereza waliwashauri mawaziri wa serikali ya Zanzibar pia waondoke Unguja kwa kutumia meli hiyo kwa usalama wa maisha yao na kwamba wangeweza kurejea Unguja wakitokea Pemba ambako wangeweza kupokelewa vizuri na kupanga mikakati kamambe ya kurejea madarakani.

Mawaziri hao walikataa, na ilionekana kana kwamba mawaziri wengine walitaka kujaribu kufanya mashauriano na mapatano na waasi walioiangusha serikali yao kutoka walikokuwa. Wengine hawakutaka kuondoka kwa sababu waliogopa kuondoka katika maeneo walimokuwa wamejificha.

Baadhi waliomba hifadhi katika Ubalozi wa Uingereza; wengine, kama Ali Muhsin (Waziri wa Mambo ya Nje) na Juma Aley (Waziri wa Maendeleo ya Fedha) walijaribu kwenda katika vituo vya polisi ambavyo vilikuwa havijatekwa bado, lakini wasiwasi uliwafanya washindwe kutekeleza uamuzi huo.

Wakati hali ya kisiasa Unguja imechafuka, mapema asubuhi Sheikh Abeid Amani Karume aliamshwa nyumbani kwake Miembelado na kundi la askari wa Okello. Alileta ubishi kidogo, lakini alizidiwa nguvu na shuruti ya askari hao.

Walimtaka aondoke Unguja haraka iwezekanavyo. Kisha wakampakia katika jahazi lililompeleka Dar es Salaam. Sababu za kuondolewa kwa Karume Unguja kwa lazima na kutakiwa kwenda Dar es Salaam zilielezwa na wafuasi wa Okello kuwa “...ni usalama wake ikiwa mapinduzi yangeshindwa” au ikiwa Waarabu wangewazidi maarifa.

Karume alijikuta amefikishwa Dar es Salaam huku akiwa amechanganyikiwa kutokana na hali iliyotokea Zanzibar. Mwingine aliyekuwa amechanganyikiwa sawasawa na Karume ni Kassim Hanga na Abdulrahman Babu ambao tayari walikuwa wamewasili Dar es Salaam.

Othman Sharif naye alifanyiwa kama Karume alivyofanywa—kuamshwa mapema asubuhi. Aliamshwa asubuhi na wanaume wawili, mmoja akiwa na bunduki na mwingine akiwa na mishale na upinde.

Lakini, tofauti na Karume, badala ya kusafirishwa kwenda nje ya Unguja, aliambiwa asiongee lolote kwa muda wa saa kadhaa, lakini aliamriwa kuwaonesha wanaume hao mahali wanapoishi mafundi mitambo wa redio. Viongozi wengine wa ASP walifichwa mahali ambako walilindwa na wanamapinduzi mpaka mwisho wa maasi.

Wakati huo huo, aliposikia milio ya kwanza ya bunduki, Smithyan, Katibu wa Kudumu Katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alijaribu kutambua ni kitu gani kilichokuwa kikitokea.

Alijaribu kumweka katika hali ya tahadhari ofisa wa Kiingereza katika serikali ya Zanzibar, H. Hawker, ambaye naye alimtahadharisha Balozi wa Uingereza aliyekuwa Unguja, Tim Crosthwait.

Ingawa kituo cha redio kilikuwa tayari kimetekwa, mawasiliano ya simu yalikuwa bado yanafanya kazi muda wote wakati mapinduzi yakifanyika. Mpaka jioni ya siku hiyo, Januari 12, mfumo wa mawasiliano usiotumia waya wa uwanja wa ndege ulikuwa ukifanya kazi pia.

Kwa kupitia uwanja wa ndege, nchi za nje zilikuwa zikijulishwa mambo yaliyokuwa yakitendeka Zanzibar kwa wakati huo, na misaada kadhaa iliombwa kukabiliana na waasi. Meli moja ya jeshi la maji iliyojulikana The Owen, ilitumwa kutoka Uingereza kwenda Zanzibar kufanya kazi ya uokozi, lakini ilikuja kuwaokoa raia wa Uingereza na wala si kukabiliana na waasi.

Baada ya kuona hakuna msaada wa ziada unaokuja, Smithyan aliona kuwa makao yake hayakaliki, hivyo saa mbili asubuhi aliondoka katika himaya yake. Baada ya kukabidhi madaraka kwa Hawker ambaye alikuwa akiwasiliana na mawaziri wa Sultan, Smithyan, kwa usalama wake aliogelea baharini kutoka ufukweni hadi alipofanikiwa kuingia katika meli iliyoitwa Salama.

Hawker alifanya mpango wa kurejeshwa kwa meli kubwa ya serikali iliyoitwa ‘Seyyid Khalifa’ ambayo kwa wakati huo ilikuwa Tanga. Lakini meli hiyo iliwasili Zanzibar jioni ya Januari 12.

Wakati Shamte Hamadi, Juma Aley na Muhsin wakiwa katika Kituo cha Polisi cha Malindi kabla hakujapambazuka, kwa kushauriwa na Kamishna wa Polisi, J. M. Sullivan, walijaribu kuomba msaada kutoka kwa jeshi la Uingereza lililokuwa Kenya. Lakini ombi lao halikufanikiwa.

Ilipofika jioni, huku hali ikiwa ya kutatanisha, Waarabu wa Kimanga walikuwa wakitafuta hifadhi katika vituo vya polisi ambavyo vilikuwa havijatekwa bado. Wanamapinduzi walimtumia ujumbe ofisa mmoja wa Kitengo Maalum cha Polisi aliyekuwa akishirikiana nao amshawishi Sullivan aondoke ili waweze kuteka maeneo yote ya Ziwani.

Mashambulizi katika kituo cha Polisi cha Malindi yalifanywa mchana wa kati ya saa saba na saa nane huku yakishuhudiwa na makundi makubwa ya watu. Baada ya matukio mengi ya kisiasa na kijeshi, na baada ya kujaribu kufa na kupona kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na wanaharakati ambao sasa walikuwa wameweka kituo chao eneo la Raha Leo, Sullivan aliwakusanya watu wake waliomtii—weupe kwa weusi—katika kundi moja na kuwapeleka bandarini.

Kutoka hapo walivushwa kwenye maji hadi ilipokuwa meli ya Salama na wengine, baadaye, wakapakiwa katika meli ya Seyyid Khalifa na kisha wakapelekwa Dar es Salaam. Baadhi ya hawa walirejea Zanzibar baadaye, ambapo wengine walikamatwa na kutiwa ndani.

Huku mfumo wa serikali ya Zanzibar ukiporomoka zaidi, na taarifa kuhusu waliouawa na majeruhi zikitolewa, na kutokuwa na idadi isiyoaminika ya askari, Sullivan alikuwa katika hali ngumu ya kuamua mambo.

Kisio la polisi waliouawa au kujeruhiwa katika mashambulizi siku hiyo walidaiwa kufikia 300, lakini inawezekana idadi ilikuwa ndogo zaidi ya hiyo kutokana na polisi wengine kukimbia wakati mashambulizi yalipokuwa makali na hivyo kuhesabiwa kama ama walijeruhiwa au kuuawa.

Upinzani ulikuwa mkubwa zaidi katika eneo la kituo cha polisi cha Mjini kilichokuwa chini ya ofisa wa Kiarabu aliyejulikana sana kwa jina moja la Sketi, ambaye mapema alikuwa ameteuliwa na Shamte kuwa Msaidizi wa Kamishna wa Polisi. Sketi aliuawa kwa kukatakatwa kwa mapanga na mashoka na kundi lililounga mkono wanaharakati wa mapinduzi.

Ilipofika jioni ya Januari 12, 1964 hakukuwa na upinzani wowote dhidi ya wanamapinduzi mjini Unguja, ingawa kulikuwa na milio ya risasi na mauaji kadhaa yaliyoripotiwa kuendelea kufanyika katika maeneo ya vijijini kwa muda fulani hadi jua lilipozama, hususan maeneo ya Bumbwini kaskazini ambako Waarabu waliokuwa na silaha waliendelea kuwafyatulia watu risasi kwa saa kadhaa. Vikundi vingine vya Waarabu viliendelea kupigana katika maeneo ya Nungwe na Bububu hadi waliposhindwa na wanaharakati na kuuawa kwa kuchinjwa mithili ya wanyama machinjoni.

Huo ukawa mwisho wa Serikali ya Sultan iliyodumu Zanzibar kwa zaidi ya karne moja. Sultan wa kwanza wa Zanzibar alikuwa Majid bin Said (1856–1870). Kisha wengine waliofuata ni pamoja na Barghash bin Said (1870–1888), Khalifah bin Said (1888–1890), Ali bin Said (1890–1893), Hamad bin Thuwaini (1893–1896), Khalid bin Barghash (1896).

Wengine ni Hamud bin Muhammed (1896–1902), Ali bin Hamud (1902–1911), (alijiuzulu), Khalifa bin Harub (1911–1960), Abdullah bin Khalifa (1960–1963) na hatimaye akaja Jamshid bin Abdullah (1963–1964) ambaye alipinduliwa Januari 12, 1964.


No comments: