Monday, February 5, 2007

Penye ukweli, uongo hujitenga



PENYE UKWELI, UONGO HUJITENGA



Na William Shao



“Nawaandikia makala hii wale wanaoheshimu Maandiko Matakatifu ya Biblia.” Ndivyo alivyoanza kuandika msomaji aitwate Innocent R. Mutahyabarwa katika gazeti la RAI (Novemba 23-29, uk. 20).



Nimependa changamoto yake, lakini hakukumbuka kuwa tafsiri anazotumia kimsingi zinamtatiza yeye mwenyewe na kutatiza wengine. Kuna mambo mengi ambayo ama anaficha kwa makusudi au hayajui kwa ‘maasumu’ kama jina lake linavyofasiriwa kwa Kiswahili.



Kwa kuwa kujibu yote aliyoandika katika makala hiyo ni sawa na kuandika kitabu kizima, kupoteza wakati na kujaza nafasi gazetini, nitataja machache sana kwa uchache sana, kisha wasomaji wa RAI ninaoamini wamefunguka bongo zao wataamua kama majibu hayo ni halali au la.



Ingawa Innocent hakukosea katika kila sentensi, amekosea katika kila aya aliyoandika. Kwanza hakuna kitu duniani kinachoitwa ‘Maandiko Matakatifu ya Biblia’. Biblia yenyewe ndiyo inayoitwa Maandiko Matakatifu.



Hilo ni kosa lililoonekana katika sentensi yake ya kwanza katika aya ya kwanza ya makala yake. Labda alitaka kusema Biblia Takatifu, ambayo hutafsiriwa kama Maandiko Matakatifu.



Biblia yenyewe, hasa Union Version na King James Version, inajitafsiri hivi: hii ni “Maandiko Matakatifu ya Mungu yaitwayo Biblia, yaani Agani Jipya na Agano la Kale.” Kutamka “Maandiko Matakatifu ya Biblia” ni sawa na kusema “Biblia ya Biblia, au Maandiko Matakatifu ya Maandiko Matakatifu”.



Kitabu kinachofuatwa na Wakritso ni Maandiko Matakatifu ‘yaitwayo’ Biblia na wala si Maandiko Matakatifu ‘ya’ Biblia. Innocent amekosea katika sentensi ya kwanza ya makala yake kama alivyokosea karibu kila sentensi ya katika kila aya.



Innocent aliandika kuwa “Biblia huweza kunukuliwa na yeyote, hata shetani.” Kwa hili nakubaliana naye, kwamba hata shetani anaweza kuinukuu Biblia, ili mradi hakuniita shetani. Lakini amesema “Mwandishi Shao anaichukulia juu juu Biblia.”



Katika aya nyingine aliandika, “Kuna vitabu vingine ambavyo wamejiandikia wapotoshaji wa Ukristo anavyotaka mwandishi (Shao) tuvisome. Vitabu hivyo siyo vitabu vya historia halisi ya Kanisa Katoliki.”



Alitaka kumaanisha nini? Kwamba ni vitabu vya historia ya Kanisa Katoliki ni kwa vile tu siyo vitabu “halisi”? Ni kweli kwamba vitabu nilivyonukuu katika kitabu changu, MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA, siyo vitabu ‘halisi’ vya historia ya Kanisa Katoliki.



Innocent anataka kuwaambia wasomaji wake kuwa kitabu kikishakuwa cha historia ya Kanisa Katoliki ni kitakatifu na kwamba hakipotoshi, hakiwezi kukosewa na mwandishi wake na ni kitakatifu—au pengine ni zaidi ya wanadamu?



Hata hivyo, ukweli ni kwamba Biblia siyo kitabu cha historia ya Kanisa Katoliki—iwe ni historia halisi au isiyo halisi. Hakuna mahali popote katika Biblia palipo na neno ‘Katoliki’ au ‘Ukatoliki’. Hicho ni kitabu kinachotumiwa na Wakatoliki, lakini si cha Kikatoliki. Ni kitabu cha Kikristo.



Kuna Biblia za Kikatoliki, ambazo zimetafsiriwa na Wakatoliki kutoka katika Biblia halisi. Mojawapo ni Biblia ya Douay, au Douay-Rheims, ambayo tafsiri yake ilikamilika kati ya mwaka 1582 na 1609.



Ingawa kuna hoja nyingi za kumjibu, nianzie pale ninapoichukulia Biblia kijuu juu na yeye anapoichukulia kwa uzito. Tuache kutumia nukuu yoyote katika kitabu chochote kisichohusiana na “historia halisi ya Kanisa Katoliki”. Tuchukulie kwamba Biblia inahusiana na Kanisa Katoliki, madhali wanaikubali.



Innocent alisahau kwamba katika sentensi ya mwisho ya aya ya sita ya makala yake hiyo alidai hivi: “Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja.” Hapo alitamka ukweli usioweza kupingwa.



Ni kweli Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja. Je, makasisi wa Kikatoliki siyo Wakristo? Kama Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, mbona mapadri, ambao ni Wakristo, hawafungi ndoa? Au angalau ndoa ya mke mmoja?



Haya ni maswali yanayotokana na hoja ya Innocent. Pengine alijisahau tena alipoandika: “Kama mnavyoelewa Wakatoliki wote ni mapadri.” Nani anayeelewa? Ni rahisi kumwelewa? Tazama sentensi zake: “Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, … Wakatoliki wote ni mapadri.”



Ukizitumbukiza sentensi hizo katika mantiki zitakataa. Kama Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, na kama Wakatoliki wote ni mapadri, kwanini mapadri hawafungi ndoa? Kama mapadri hawafungi ndoa kamwe, na kama Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, ni rahisi kuhitimisha kimantiki kuwa mapadri siyo Wakristo(?)



Innocent anaonyesha kudai kwamba Biblia inaunga mkono makasisi kutooa. Sikuona mahali popote katika Biblia panaposema hivyo. Yeye anasema: “Na hata tukimsoma 1 Wakorintho 7:7…,” kana kwamba mstari huo unaunga mkono padri kutooa.



Tuanzie hapa. Ni kweli kwamba Biblia inasema: “...Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendeje Bwana; bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.” (1Wakorintho 7:32,33).



Sentensi hiyo ndiyo inayotumika kama kigezo? Kama hivyo ndivyo, hiyo haijaelezwa kuwa ni lazima, bali ni hiari tu.



Kwa kuonyesha tu kwamba hilo ni pendekezo, Biblia inasema hivi: “Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia ... Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi, ... Lakini mtu awaye yote akiona ya kuwa hamtendei mwanamwali wake vipendezavyo, na ikiwa huyo amepita uzuri wa ujana wake, na ikiwapo haja, basi, afanye apendavyo, hatendi dhambi; na awaruhusu waoane.” (1 Wakorintho 7:28, 35, 36). Huko ni kusoma Biblia kijuu juu?



Yesu mwenyewe, wakati akijibu maswali ya Mafarisayo, alisema: “…Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si mwili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” Mathayo 19:4-6.



Lakini katika Biblia, ndoa huchukuliwa na kuheshimiwa kama zawadi safi na takatifu kutoka kwa Mungu. Na Mungu huzibariki ndoa kuwa ni kitu chema, kama ilivyoelezwa hapo juu kutoka katika kitabu cha Mithali 18:22, kwamba: “Apataye Mke apata kitu chema; naye ajipatia kibali kwa Bwana.” Kwa kutumia mantiki hii, mapadri hawana kitu chema, wala kibali kutoka kwa Bwana?



Zaidi ya hilo, inaelezwa kuwa ni “afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwezake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kimwinua” (Mhubiri 4:9, 10) Ndiyo maana kuna mapadri wengi huanguka katika zinaa na wala hawana wa kuwainua wala wa kuwazuia wasiangukie tena huko.



Mungu alipomuumba mwanadamu wa kwanza ambaye alikuwa mwanaume, hakukusudia aendelee kuishi peke yake. Ingawa alikuwa akimtafutia mwenza wake, hakumletea mwanaume mwenzake, bali alimtengenezea mwanamke----mke wake.



Baada ya kumuumba mwanadamu katika Bustani ya Edeni, “Bwana Mungu akasema, Si vyema mtu huyo awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye … na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.



“Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu ... kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” (Mwanzo 2:18, 22-24).



Mtume Petro na baadhi ya watumishi wengine wa Mungu waliokubaliwa na waliokuwa na nyadhifa na mamlaka katika kazi za Kikristo siku za mwanzo za Ukristo walikuwa ni wanaume waliofunga ndoa.



Walikuwa na wake na familia zao. Hawa walikuwa ni Wakristo halisi kuliko Wakristo wengine, au wote, wa siku hizi. Mungu aliwakataa watu hao kwa sababu ya kuoa kwao?



Biblia inasema: “Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.” (Mathayo 8:14) Haiwezekani Petro akawa na mkwe na wakati huo huo asiwe ameoa mke. Hata mitume nao walikuwa wameoa. Hawakulazimishwa kuwa waseja ili waweze kushiriki katika kazi zao za utume.


Kitabu cha Matendo 21:8-9 kinasimulia hivi: “Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake. Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.” Je, mtumishi huyo alikuwa na mabinti aliowapata kutoka wapi kama hakuwa na mke aliyemzalia watoto hao kupitia njia ya ngono?


Ingawa Kanisa Katoliki ndilo linalosisitiza makasisi wake wasioe, ukweli wa kihistoria ni kwamba kuna mapapa waliokuwa wameoa—nasema mapapa, si makasisi wa kawaida au viongozi wa kanisa Katoliki wa vyeo vya chini. Na hawa walikubaliwa na kanisa.


Hata wale ambao hawajaoa wana mahawara, vimada na watoto waliozaa kwa siri. (tazama kitabu changu, MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA). Kitabu hicho kinawataja mapapa waliooa, idadi ya watoto waliozaa na hata watoto wa mapapa ambao nao walitawazwa kuwa mapapa kama baba zao.


Innocent, unaweza kusema ni kwanini kuna papa waliokuwa wameoa? Kwanini hatimaye wakaamua mapadri wasioe tena baada ya karne nyingi baada ya Kristo? Mapapa hawa hawakulijua neno la Mungu?


Mwaka 1967, Papa Paul VI (1897-1978)—au kama ndugu na rafiki zake wa eneo la Concesio, Italia walivyomjua, Giovanni Battista Montini, kwa mujibu wa jarida la Kikatoliki, ‘Priestly Celibacy’ (la Ijumaa ya Juni 23, 1967), alikiri hivi:


“Agano Jipya ambalo ndilo hutoa mafundisho ya Kristo na Mitume wake …halidai useja wa kushurutishwa kwa wahudumu wa kanisa …Yesu mwenyewe hakuweka jambo hilo kama sharti la kuwachagua Mitume wake Kumi na Wawili, wala Mitume walioongoza Ukristo katika zile siku za mwanzo hawakuwalazimisha watu wasioe ili wawe watumishi …Agano Jipya …halilazimishi useja kwa wahudumu wa makanisa.”


Hata hivyo, maelekezo ya mtume Paulo kwa Timotheo juu ya kuwekwa rasmi kuwa waangalizi wa Wakristo, au mapadri, au maaskofu, hudhihirisha jambo hili: “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha ... mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu ... Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.” (1 Timotheo 3:2, 4, 11).


Hayo ni masharti yaliyotajwa na Mtume Paulo, lakini katika masharti hayo yote yaliyotolewa katika kitabu cha Timotheo, ingawa hakuna hata moja linalomlazimisha askofu kuoa, hakuna hata moja linalomkataza asioe kwa ajili ya utumishi wake akiwa katika cheo cho chote cha utumishi wa kanisa katika Ukristo.


Mtume Paulo alionyesha tu kwamba ‘askofu’ hapaswi kuoa wake wengi, lakini haikudokezwa popote katika Biblia kwamba hapaswi kuoa kamwe.


Anawajibika awe mume wa mke mmoja, na wake zao wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. Ikiwa amefunga ndoa, anapaswa kuwa na mke mmoja tu----wala si kutooa kamwe.


Sehemu ya Waraka wa Kwanza wa Paulo Mtume kwa Wakorintho unasomeka hivi: “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karamu yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane. Ni heri wakae kama mimi nilivyo.” (1 Wakorintho 7:7, 8).


Je, hilo ndilo neno linalochukuliwa kama chanzo cha useja katika nyadhifa za Kanisa? Huenda. Lakini Kanisa halijaitamka waziwazi. Na kama linachukuliwa hivyo, ni kwanini jambo la kutooa linasisitiziwa makasisi peke yao lakini lisisisitizwe kwa “wale wasiooa bado, na wajane” kama Biblia inavyosema?


Apendalo Mtume Paulo halijaelekezwa kwa makasisi, bali ni kwa wasiooa bado na wajane. “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.” (1 Wakorintho 7:8). Walioambiwa wakae kama Mtume Paulo alivyo ni wale wasiooa bado, na wajane, lakini si makasisi.


Hata kama walioambiwa maneno hayo ni makasisi, pale mwanzoni mtume Paulo aliwaambia Wakorintho hivi: “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. (1Wakorintho 7:1-2).


Mstari wa tisa anasema, “Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” Ni kweli kwamba mapadri hawagusi wanawake? Hawawaki tamaa? Hawazini? Vyovyote iwavyo, hata kama hawawaki tamaa au hawazini, katika Maandiko Matakatifu haijasemwa kwamba hiyo ilikuwa amri. Ni pendekezo tu.


“Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.” (1 Wakorintho 7:6). Hakuna amri iliyotolewa. Ilikuwa ni idhini tu—au pendekezo tu. Ikiwa Biblia inatoa idhini tu, “...si kwa amri.” Hiari hiyo haikutolewa kwa makasisi, bali ni wale wasiooa bado na wajane.


Kwanini leo Makanisa yanatoa amri, si kwa idhini? Kwanini yanatoa amri ambayo Biblia haijatoa? Wao walizipata wapi amri hizo? Amri zenyewe zinatimiza kusudi gani? Je, wao ni matowashi?


Biblia imezungumzia hali hiyo. Inasema kuwa wanaume na wanawake fulani huchagua useja kwa hiari zao wenyewe, na ingefaa useja uchaguliwe kwa “idhini..., si kwa amri.” (1Wakorintho 7:6).


“Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; (kama ilivyoelezwa hapo juu kuhusu nchi ya India) tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” (Mathayo 19:12).


Labda Innocent atuambie kuwa mapadri ni matowashi kwa maana ya neno ‘towashi’. Hata hivyo, katika Biblia, neno ‘towashi’ halijapewa uzito wa upadri. Neno hilo, ambalo kwa Kiingereza ni ‘eunuch’, limeonekana mara 19 tu katika Biblia.


Limeonekana mara kadhaa katika vitabu kadhaa vya Biblia. Katika kitabu cha Esta (5), Isaya (2), Daniel (1), Mathayo (5), Yeremia (1) na Matendo (5). Kufikia hapo nafunga mjadala. Kwa wasomaji wa RAI, ambao ni wasomaji makini, wachambue hoja hizo waamue kama ni halali au si halali.


William Shao ni mwandishi wa kitabu kiitwacho MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA na mwandishi wa habari wa HABARI CORPORATION LTD. Anapatikana kupitia 0754-989837, shao2020@yahoo.co.uk.

Rudi Nyuma

No comments: