Monday, February 5, 2007

Maasi kijeshi 1964



MAASI YA KIJESHI 1964: MHUSIKA MKUU ALIKUWA NANI?

Na William Shao

“NIA yake (Nyerere) iliyojaa busara ya kuendelea kulijenga taifa inaonekana inaanza kueleweka kwa watu wake (Watanganyika), hususan katika kauli mbiu yake, “Uhuru ni Kazi”. Lakini ghafla jambo fulani lisilotarajiwa linatokea katikati ya nia yake.

“Jeshi lake linaasi; ghasia zinazuka katika mitaa ya Dar es Salaam. Watu wanauawa. Mali zinaporwa. Alinusurika tu kwa kuita majeshi ya Uingereza. Wakati moto ulipotulia, swali la kutisha likakosa jawabu: ‘Ikiwa Nyerere anaweza kutikiswa hata kufikishwa kwenye ukingo wa kuangamia, ni nani aliye salama katika Bara la Afrika?’”

Hayo yaliandikwa na jarida TIME la Marekani (Machi 13, 1964), ikiwa ni siku 53 tu tangu kulipotokea maasi ya kijeshi katika Tanganyika. Je, jarida hilo liliona kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa salama kuliko kiongozi mwingine yeyote katika Afrika kiasi cha kuuliza swali hilo “la kutisha”?

Kuna siku ambazo historia rasmi ya Tanzania haipendi kuzikumbuka, lakini haitaweza kuzisahau. Januari 19, 1964, siku kulipotokea maasi ya kijeshi katika Tanganyika, ni miongoni mwa siku hizo. Hiyo ilikuwa ni wiki moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12.

Hata Mwalimu Nyerere alijua kuwa ni vigumu kusahau, ingawa inawezekana kwa kuificha historia. Kwa huzuni Nyerere alikaririwa na jarida TIME (Jan. 31, 1964), chini ya makala yake, The Rise of the Rifles, akisema: “Itachukua miezi, na hata miaka, kufuta katika bongo za walimwengu kile walichosikia kuhusu matukio ya juma hili.” Hata hivyo imeshaanza kufutika katika bongo za walimwengu.

Kwa maneno mengine tunaweza kusema haya yalikuwa ni Mapinduzi ya Tanganyika. Tofauti kati ya Mapinduzi ya Zanzibar yale ya Tanganyika ni kwamba: Mapinduzi ya Zanzibar yaliruhusiwa yafaulu, lakini Mapinduzi ya Tanganyika hayakuruhusiwa kufaulu.

Usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 18—19, 1964 kulitokea zahama mjini Dar es Salaam katika Kambi ya jeshi ya Colito (sasa inajulikana kama Lugalo), ambalo lilisambaa hadi kambi nyingine nchini.

Baada ya tukio hilo, maswali mengi yaliulizwa. Ingawa tayari mengi yamejibiwa, majibu hayo ni ya ‘kuzunguka mbuyu’. Je, yalikuwa ni mapinduzi ya serikali (kama yale ya Zanzibar)? Yalikuwa ni maasi tu ya kijeshi? Ulikuwa ni mgomo tu wa wanajeshi waliotaka kuongezwa mishahara?

Majibu yaliyotolewa na wale walioitwa—au waliojiita—wanasayansi wa siasa yalijaribu kupunguza uzito wa maasi hayo kutoka katika mapinduzi ya serikali na kuyafanya yaonekana kana kwamba yalikuwa ni mgomo tu wa kutaka kuongezwa mishahara na vyeo.

Tafsiri zao zilikuwa hivi: kama ingekuwa ni mapinduzi, ilikuwa ni lazima kwanza wanajeshi walioasi wangeteka maeneo yote muhimu ya kama Bunge na Ikulu. Ilikuwa ni lazima wawakamate mawaziri, jambo ambalo hawakufanya. Hawakuwa wamemtangaza kiongozi wa nchi.

Huenda haikuwa mapinduzi ya serikali, lakini kwa namna fulani ilikuwa ni mapinduzi ya aina yake. Tangu wakati huo mfumo mzima wa Jeshi la Tanzania ulibadilika moja kwa moja. Hata bei ya baadhi ya bidhaa—kama vinywaji—zinazopatikana kwa raia siyo bei ile ile ya bidhaa zile zile zinazouzwa katika makambi ya jeshi.

Isitoshe, tangu wakati huo, Tanzania imekuwa ya kijeshi zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake. Ilifika wakati ambao ili kuwa msomi wa nchi hii ilikuwa lazima kwanza uwe na mafunzo ya kijeshi (JKT). Hata viongozi wengi wa nchi wanatamkwa kwa vyeo vya kijesho.

Ilidaiwa kuwa aliyekuwa afaidike na maasi hayo ni Waziri wa zamani wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Tanganyika, Oscar Kambona ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Kaasim Hanga wa Zanzibar.

Hata wakati Mapinduzi ya Zanzibar yanafanyika, Hanga aliondoka haraka kwenda Dar es Salaam kuzungumza na Kambona kuhusu matukio ya Zanzibar. Hadi leo mazungumzo hayo yamekuwa siri.

Baada ya Mapinduzi Hanga alikataa kutoa sababu zozote za yeye kwenda kuonana na Kambona na hakutaka kuzungumzia jambo walilojadiliana. Alichosema, alipohojiwa na mwandishi wa Kiingereza, Keith Kyle, kwa mujibu wa gazeti The Spectator, Februari 14, 1964, “...Nilikuwa kazini.”

Kambona walikutana tena na Kassim Hanga siku moja kabla ya maasi ya kijeshi yaliyotokea mjini Dar es Salaam usiku wa Januari 18-19, 1964 ambayo yalitokea juma moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Inawezekana Mwalimu Julius Nyerere alijua jambo fulani kuhusu mapendekezo ya Kambona kumsaidia Kassim Hanga, lakini hakujua jambo lolote kuhusu maasi ya kijeshi yaliyotokea Dar es Salaam na kumfanya yeye akimbilie mafichoni Kigamboni.

Kambona alijua kuhusu mpango wa maasi ya kijeshi na, kwa mujibu wa Anthony Clayton katika kitabu chake, The Zanzibar Revolution, “...Kambona alitazamia kufaidika kisiasa kutokana na machafuko ambayo yangetokea.”

Haikuelezwa ni namna gani angefaidika. Lakini wasiwasi wa baadhi tu ya watu waliofuatilia mambo hayo wanadai kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa yamepangwa kufanyika wakati mmoja na Maasi ya Dar es Salaam yaliyoanzia katika Kambi ya Colito (Lugalo).

Kwa maana nyingine kuna watu waliokuwa wamepanga kufanya mapinduzi huko Zanzibar usiku wa Januari 18, siku ambayo kulitokea machafuko katika mji wa Dar es Salaam, lakini John Okello akawazidi ‘kete’.

Kwamba Mapinduzi ya Zanzibar yalipangwa kufanywa na Kassim Hanga na watu wake huko Zanzibar usiku wa Jumamosi ya Januari 18 kuamkia Jumapili ya Januari 19 na usiku huo huo Kambona, au watu waliohusiana naye, wangefanya Mapinduzi ya Dar es Salaam ni jambo lililozua gumzo wakati huo.

Kama yote hayo ni ya kweli, Mapinduzi ya Unguja na yale ya Dar es Salaam yalipangwa kufanywa siku moja—usiku wa Januari 18—19, 1964. Mipango hiyo ilikuwa imeandaliwa kwa muda mrefu.

Hata mijadala fulani fulani, kama ile ya kuwajadili Wacuba walioonekana Dar es Salaam na Unguja katika kipindi hicho—ilifanyika Bagamoyo na maeneo mengine ambayo hayakujulikana haraka.

Kwa kawaida Kambona alijua au alikuwa amearifiwa mapema kuhusu maasi ya Dar es Salaam katika vitengo vya usalama vya Tanganyika na maofisa wa Kiingereza ambao bado walikuwa wakiitumikia Serikali ya Tanganyika, lakini hakuchukua hatua yoyote kuikabili hali hiyo hadi pale ilipotokea. Mmoja wa maofisa hao ni Luteni Kanali Rowland Mans.

Ilidaiwa kuwa mara kwa mara, Kambona, akiwa Waziri wa Ulinzi, alikuwa akiwatembelea maofisa wa ngazi za chini katika kambi ya Colito, na mara nyingine bila kuonana na viongozi wakubwa wa kambi hiyo.

Pia, kwa sababu zisizojulikana dhahiri lakini ambazo inawezekana ni njia ya kumsaidia Kassim Hanga, Kambona alitenga silaha na zana nyingine za vita zilizotoka Algeria na kuwasili Dar es Salaam Jumatano ya Januari 3, 1964 na kupakuliwa chini ya ulinzi maalum. Silaha hizo ziliwasili siku tisa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar na wiki mbili kabla ya maasi ya Dar es Salaam.

Silaha hizi, baada ya maasi yaliyotokea Dar es Salaam, inadaiwa—na hii inadaiwa tu—zilichukuliwa na kutoswa baharini na Jeshi la Maji la Uingereza lililoombwa na Serikali ya Tanganyika Jumamosi ya Januari 25, 1964, kukomesha maasi ya jeshi Dar es Salaam.

Hata hivyo nyingi za silaha hizo zilitumiwa wakati wa Vita Kuu II Kaskazini mwa Afrika. Zilitumiwa na Waingereza, Wajerumani, na Waitalino na zingekuwa vigumu kutumiwa katika miaka ya 1960 kwa kuwa hazikuwa na vipuri.

Inasemekana kwamba silaha hizo ziliagizwa na Serikali ya Tanganyika kwa ajili ya chama cha Frelimo cha Msumbiji. Zilipowasili Dar es Salaam, pamoja na kwamba maofisa wakubwa wa Jeshi la Tanganyika walikuwa ni Waingereza, silaha hizo zilipakuliwa na wanajeshi Waafrika tu.

Inasemwa pia kwamba silaha hizo hazikuhifadhiwa kama ilivyopaswa, kwa hiyo zikawafanya Waingereza washtuke. Walipozichunguza sana wakagundua kuwa zana nyingine zilitiwa alama ya msalaba mweusi, wakachukulia kwamba hizo zilizotiwa alama zilikusudiwa kupelekwa Zanzibar kumsaidia Kassim Hanga kulingana na tetesi walizokuwa wamezipata hapo awali. Lakini silaha hizo hazikuwahi kufika Zanzibar. Je, zilikusudiwa kutumika wakati wa maasi yaliyotokea Dar es Salaam?

Kwa mujibu wa utafiti wa Ndugu Nestor Luanda katika kitabu Tanganyika Mutiny, Kambona alianza kufika mara kwa mara katika Makao Makuu ya Jeshi mwishoni mwa 1963 na aliwaambia maofisa wa kijeshi wa Kiingereza kwamba alitaka wawe wameondoka nchini ifikapo mwishoni mwa 1964.

Kambona alitaka maofisa wengi wa Kitanganyika wapewe vyeo haraka, jambo ambalo Waingereza walidai haliwezi kutendeka kwa ghafla kama alivyotaka. Kuanzia hapo maofisa hao wakaanza kuwa na wasiwasi kuwa chochote kinaweza kutokea.

Ingawa uhusiano wa maofisa wa kijeshi wa Uingereza na Waziri Kambona ulianza kupungua, huo si ushahidi wa kutosha kueleza kuwa Kambona alihusika kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

Hata hivyo, usiku ule wa maasi maofisa wengi wa Kiingereza walikamatwa na ‘kutiwa ndani’ katika Kambi ya Colito’ ambako kwa wakati huo umeme tayari ulikuwa umekatwa.

Kikosi cha kiasi cha wanajeshi 25 waliondoka kambini hapo kwenda Ikulu kumfuata Rais Julius Nyerere kikiongozwa na mwanajeshi machachari, Sajenti Francis Hingo Ilogi, mzaliwa wa Bukene, Tabora.

Wakati huo huo, Mkuu wa Tawi Maalum, Emilio Mzena, baada ya kuambiwa yaliyotokea na kwamba wanajeshi walio na silaha wameelekea Ikulu, aliwaarifu watu wake waliokuwa Ikulu na kuwaambia wamtoroshe Rais.

Mzena aliambiwa kuhusu maasi hayo majira ya saa 8:00. Nusu saa baadaye, saa 8:30, baada ya kuamshwa na walinzi wao, Rais Nyerere, akiongozana na Makamu wake, Rashidi Kawawa, waliondoka Ikulu kupitia mlango wa nyuma. Walipishana na wanajeshi hao kwa sekunde chache tu.

Baadaye wanajeshi hao walipelekwa kwa Oscar Kambona, wakamchukua kwenda naye kambini kwao, Colito. Wakati huo ghasia na uporaji wa mali za raia tayari ulikuwa umetanda katika mitaa ya mji wa Dar es Salaam.

Wakati hayo yakitokea, tayari walikuwa wameanza kupeana vyeo huko huko kambini. Wengine walipokea vyeo hivyo lakini wengine hawakuharakisha kupokea. Kwa mfano, Ilogi ambaye alikuwa na cheo cha Sajini alijikuta katika cheo cha Luteni Kanali na wengine walimtaka mtu kama Kapteni Alex Nyirenda kuwa Brigedia.

Maasi hayo yalisababisha ghasia nyingi mitaani, hususan Mtaa wa Msimbazi maeneo ya Kariakoo. Maeneo mengi ya katikati ya mji risasi zilirindima. Mwarabu mmoja eneo la Magomeni, kwa kuona duka lake linavamiwa, alimpiga risasi mwanajeshi mmoja aliyejulikana kwa jina la Kassim.

Koplo Nashon Mwita, ambaye alishuhudia mauaji hayo, alirudi kambini kujizatiti. Akiongozana na askari mwingine, Luteni Mwakipesile, pamoja na wanajeshi wengine, walifika Magomeni na kummiminia risasi Mwarabu huyo.

Kana kwamba haikutosha, waliiteketeza nyumba yake kwa moto. Katika nyumba hiyo, inasemekana, Mwarabu huyo aliteketea na familia yake ya watu 15.

Maasi hayo yalianza kusambaa haraka. Siku moja baadaye, Jumatatu ya Januari 20, yalifika hadi kambi ya jeshi ya Tabora ambako wanajeshi wengi, kama Mrisho Kapteni Sarakikya, Luteni David Msuguri na Luteni Abdallah Twalipo walikuwa wamepandishwa vyeo.

Jumanne ya Januari 21, maasi hayo yakafika Nachingwea—kambi ambayo ndiyo kwanza tu ilikuwa imeanzishwa, ikiongozwa na Meja Temple Morris.

Jumamosi ya Januari 25, 1964, baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mwalimu Nyerere aliomba msaada kutoka Serikali ya Uingereza kunyamazisha maasi ya kijeshi yaliyokuwa yanazidi kusambaa katika Tanganyika. Hatimaye makomandoo wa Uingereza waliwasili kwa helikopta na kuwanyang’anya silaha waasi. Jioni ya siku hiyo hiyo maasi ya Tabora nayo yakazimwa.

Maasi hayo, hasa katika kambi ya Colito, yalizimwa baada ya makomandoo hao wa Uingereza kutua na kuanza kulipua lango la mbele la kambi hiyo. Mara moja askari walioasi walijisalimisha.

Kikosi cha Uingereza kiliongozwa na Brigedia Patrick Sholto Douglas. Waasi watatu waliuawa katika operesheni hiyo. 20 walijeruhiwa na wengine 400 walikamatwa, kwa mujibu wa ‘TIME’ (Jan. 31, 1964). Wengine walitoroka.

Kwa njia hiyo Rais Nyerere alirejea madarakani, lakini historia ya Tanganyika ikabadilika moja kwa moja.

Jioni ya Januari 25, baada ya kutembelea mitaa ya Dar es Salaam kujionea uharibufu uliofanywa na wanajeshi walioasi, Mwalimu alisikika moja kwa moja Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC) akisema:

“Jana nililazimika kuomba msaada wa Mwingereza. Kwa bahati akakubali. Asubuhi hii kikosi cha kwanza kikawasili …yote sasa ni shwari. Nasikia maneno ya wajinga kwamba eti Waingereza wamerudi Tanganyika.”

Zaidi ya hilo aliwachekesha waliokuwa wakimsikiliza. Alisema: “…Askari wametuvua nguo. Tuko uchi. Jamaa wanasema tuazime nguo, nasema nguo ya kuazima bwana! …Unaweza kwenda kuazima ukapata baibui.”

Wiki tatu baada ya maasi (Feb. 16, 1964), aliitisha mkutano wa hadhara Viwanja vya Jangwani na kuwaambia Watanganyika hivi: “…(Wanajeshi walioasi) Walidanganywa. Wendawazimu walikuwa wawili, watatu. Wale wengine waliswagwa tu. Wakivutishwa bangi, wakaja mjini kutenda maovu. Tukaenda kwa Mwingereza. Bwana Mwingereza tusaidie utuondolee balaa hili.”

Baada ya maasi hayo, Mwalimu Nyerere alianza kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa hakuna kosa linalorudiwa. Hatua ya kwanza, kwa mujibu wa jarida TIME (Feb. 07, 1964) alianza kukamata wote waliohusika, kisha akapiga marufuku gazeti Nation la Kenya linalomilikiwa na Aga Khan kutouzwa katika Tanganyika.

Kwanini marufuku hayo? TIME linasema hivi: “Gazeti hilo (Nation) lilitoa taarifa sahihi lakini yenye raghba kuhusu kuangushwa kwa serikali yake. Kupunguza uwezekano wa mfarakano wa mawazo, amewabadilisha makamanda wa Kiingereza akaweka wa Kiafrika. Wakati huo huo, ameteua kamati ya kutafakari mabadiliko ya kikatiba ambayo yataifanya Tanganyika kuwa nchi ya kidemokrasia ya ‘chama kimoja kisheria na kiuhakika.”

“…Uso wake ulikuwa na simanzi. Hakuna hata Mtanganyika mmoja aliyeuawa kwa miaka yote 17 ya kupigania Uhuru wa Tanganyika. Lakini sasa baada ya uhuru Watangayika wameuawa,” likasema TIME (Jan. 31, 1964)

Jumanne ya Aprili 21, Mwalimu Nyerere alimwapisha Sir Ralph Wildham ndani ya Ikulu ya Dar es Salaam kuwa Jaji Mkuu wa Tanganyika, na kumwambia awashughulikie kikamilifu wanajeshi waliofanya jaribio la kuipindua serikali yake hapo Januari 19, 1964. Ndipo Sir Wildham akatangaza rasmi kuwa wanajeshi wa Kambi ya Colito waliotaka kuiangusha serikali watafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu, Aprili 27, 1964.

Wakati huo huo Rais alimteua Kapteni Abdallah Twalipo (35) na Kapteni Lukias Shaftaeli (39), wote wakiwa ni wanajeshi wa jeshi la Wananchi, kuwa wajumbe wa mahakama ya kijeshi. Sir Wildham akawa Rais wa mahakama hiyo. Baada ya uteuzi huo, Mkurugenzi wa Mashitaka, Herbert Wiltshire Chitepo, alisema angewaita mashahidi 25.

Kesi hiyo iliendeshwa kwa siku chache na hatimaye hukumu ikatolewa. Ijumaa ya Mei 15, 1964, siku 19 baada ya kufanyika kwa Muungano wa Tanzania, wanajeshi walioasi katika Kambi ya Colito walihukumiwa, lakini adhabu zao zilikuwa tofauti.

Sajini Francis Hingo Ilogi alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, Koplo Aliche miaka kumi, Koplo Baltazar miaka kumi, Private Jonas Chacha miaka kumi, Private Pius Francis miaka kumi.

Wengine ni Private Patric Said John aliyehukumiwa miaka kumi, Sajini Lucas miaka kumi, Kapteni Kamaka Mashiambi miaka kumi, Kapteni Benito Manlenga miaka kumi, Private Dominicus Said miaka kumi, Kapteni Andrea Dickson miaka mitano, Private Hamidus miaka mitano na Roger Mwanaloya miaka mitano.

Wanajeshi walioshitakiwa lakini hawakupatikana na hatia na hivyo kuachiwa huru ni Koplo Peter Mbasha, Private Ernao Msafiri, Private Gerado Raphael, Kapteni Mahara Magom na Kapteni Moses Kawanga.

Kwamba Oscar Kambona alihusika katika maasi hayo ni jambo lisilothibitishwa. Kambona aliwahi kuhusishwa katika matukio mengi ya uhaini. Alihusishwa katika uhaini wa 1970 ambao inadaiwa alikula njama za kuiangusha serikali ya Mwalimu Nyerere.

Kama Tanzania ilikuwa tulivu tangu ilipopata uhuru wake, basi utulivu huo hauna tafsiri ile ile ambayo Watanzania wengi wanaifikiria. Ule muongo wa kwanza tangu uhuru kulijitokeza mambo mengi, na mengine hayakujulikana sana, na huenda hayatajulikana kamwe. Tukio muhimu zaidi lililotokea katika kipindi cha mwisho cha miaka ya 1960 ni kuvurugwa kwa mpango wa kuiangusha Serikali ya Julius Nyerere.

Pamoja na Kambona, ambaye alikuwa uhamishoni Uingereza, walihusishwa watu wengine waliodaiwa kuiangusha serikali ya Mwalimu Nyerere wakiongozwa na Kambona. Kesi yao ilianza Jumatatu ya Juni 8, 1970 katika Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Mkuu, P. T. Georges.

Bila kutambua kilichokuwa kinatokea, watu saba: Gray Likungu Mattaka, John Dunstan Lifa Chipaka, Bibi Titi Mohamed, Michael Marshall Mowbray Kamaliza, Eliyah Dunstan Lifa Chipaka, William Makori Chacha na Alfred Philip Milinga, walijikuta wakifikishwa mahakamani kwa kosa la uhaini wakituhumiwa kula njama za kuiangusha Serikali ya Tanzania na kumuua Rais wake, Mwalimu Julius Nyerere.

Gray Likungu Mattaka (34) zamani alikuwa Mhariri wa Habari wa katika gazeti la chama cha TANU, The Nationalist na Uhuru. Mattaka alijulikana pia kwa majina mengine ambayo ni Chaima, Kavuma, Mikaya au Edward Kavuma.

John Dunstun Lifa Chipaka (38) alikuwa katibu wa zamani wa chama cha Congress. John Chipaka, kwa mujibu wa hati za mashitaka, alikuwa na majina mengine ya bandia kama M. M. Chimwala, Chimwala Ching’wechene, Chimwala au Padre John Chimwala.

Bibi Titi Mohamed (45) ni Rais wa zamani wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT). Inasemekana kuwa naye alikuwa na majina mengine aliyojiita au kuitwa. Hayo ni pamoja na Mama Mkuu, Mwamba au Anti.

Michael Marshall Mowbray Kamaliza (40) alikuwa Katibu Mkuu wa zamani wa NUTA (Chama cha Wafanyakazi Nchini) na kadhalika Waziri wa zamani wa Kazi na alikuwa na majina mengine ya bandia kama Palijekantu, Bwana Miguu, Wamaliza au Hakuna Kitu.

Eliya Dunstun Chipaka (32) ni ndugu yake John Chipaka. Eliya Chipaka alikuwa afisa wa zamani katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania. William Makori Chacha (46) alikuwa Kanali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na majina mengine ya bandia aliyotumia ni pamoja na Ben Tasu au Kitumbo.

Kisha kuna Alfred Philip Milinga (27) aliyekuwa afisa wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Oscar Selathie Kambona, alitoroka Tanzania na kwenda kuishi nchini Uingereza.

Kisha utekaji wa ndege ukatokea Mwanza saa 11 jioni ya Ijumaa, Februari 26, 1982 uliofanywa na wale waliojiita “Vijana wa Harakati za Mapinduzi Tanzania”. Ndege hiyo ilipofika Uingereza baada ya kupita nchi kadhaa, ikadaiwa kuwa Kambona, wakati huo akiwa mafichoni Uingereza, alihusika.

Habari zilizochapishwa na gazeti The New Statesman zilisema kuwa Kambona alikuwa hospitali moja ya London inayojulikana kama Surrey karibu na wakati ambao tukio hilo lilitokea.

Alipohojiwa baadaye, Kambona mwenyewe aliliambia gazeti Africa Now (Aprili 1982) hivi: “…Naumia sana moyoni ninapohusishwa na watu hawa (wateka nyara)…” Alisema kama ambavyo hakuwahi kuwajua, hakujua hata kilichokuwa kimetokea na kwamba alipata habari za kutekwa kwa ndege ya Tanzania sawasawa na namna mtu mwingine yeyote alivyozipata.

Lakini, alisema, “kwa kuyatafakari yote, hili linaonekana kuwa ni matendo ya mwanadamu na kudra za Mwenyezi Mungu ambaye mimi kwake nasali sana …Hakuna damu itakayomwagika…” Hakufafanua kauli hiyo, na wala hakuna aliyejaribu kuitolea ufafanuzi.

Pengine alijua kitu ambacho wengine hawakukijua na hakutaka wakijue. Kwake yeye, matukio hayo ni “matendo ya mwanadamu na kudra za Mwenyezi Mungu ambaye mimi kwake nasali sana.”

Ingawa uhaini mwingi uliwahi kutendeka tangu Januari 1964, tangu baada ya maasi ya Dar es Salaam, uhusiano wa Kambona na Nyerere ulianza kuzorota hadi lilipokuja Azimio la Arusha lililomwondosha kabisa katika ardhi ya Tanzania.

Hata hivyo, hadi sasa maasi ya kijeshi ya mwaka 1964 yamebaki kama fumbo lisilo na mfumbuaji. Yalikuwa ni mapinduzi ya kijeshi? Ulikuwa ni mgomo wa wafanyakazi? Mhusika mkuu alikuwa nani? Nani aliyeendesha nchi katika kipindi cha wiki ile iliyokuwa ngumu zaidi katika historia ya Tanganyika/Tanzania?

Rais alikuwa wapi kwa kipindi chote cha karibu juma nzima? Nani hasa aliyeita Waingereza—au labda kumshauri Rais Nyerere kuita wanajeshi wa kigeni—kuja kuzima maasi? Je, wanajeshi hao walikuwa wakiasi dhidi ya maofisa wa kijeshi wa Uingereza tu? Pengine maswali haya na mengine mengi yanahitaji majibu ili kuitazama upya historia ya Tanganyika/Tanzania.

********************************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754 989 837. E-mail: shao2020@yahoo.co.uk., Blog: willyshao.blogspot.com.
********************************************************

No comments: