Monday, February 5, 2007

Mungu ataihukumu dhuluma hii




MWENYEZI MUNGU ATAIHUKUMU DHULUMA HII ILIYOTENDEKA

Na William Shao

WASOMAJI wengi wa gazeti hili wameuliza maswali mengi wakitaka majibu. Miongoni mwa maswali mengi ni kutaka kujua hatima ya Kassim Hanga katika uchambuzi wa historia ninaoufanya.

Nawashukuru wote walionipigia simu na kunitumia ujumbe kuhusu mada hizi. Lakini napenda kuwaambia kuwa ni vigumu—na pengine haiwezekani—kupata majibu ya maswali yote wanayouliza wasomaji.

Tunao wanahistoria wengi makini wanaoweza kueleza mambo haya kinaganaga kuliko tunavyofanya katika makala za magazetini, lakini ama hawajapata jukwaa au hawako tayari kufanya hivyo.

Namuunga mkono Issa bin Nasser kwa aliyosema katika kitabu chake, ‘Zanzibar: Kinyang’anyiro na Utumwa’. Aliandika: “Mwenyezi Mungu ndiye mjuaji wa yote.” Sentensi inayotangulia maneno hayo, ambayo ndiyo imenikopesha maneno ya kichwa cha habari ya mada hii, inatia uchungu hata zaidi inaposomeka hivi: “…Mwenyezi Mungu mwenyewe anaelewa namna ya kuihukumu dhuluma hii iliyotendeka…”

Naiandika mada hii kwa ufupi sana kutokana na ufinyu wa nafasi. Kassim Hanga alikuwa rafiki mkubwa wa kisiasa wa Oscar Kambona. Kama Kambona alivyopoteza nyadhifa zake katika siasa, ndivyo Hanga naye alipoteza nyadhifa zake katika Serikali ya Muungano wakati yalipofanyika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.

Hanga hakujua mambo mengi kuhusu Tanzania kama Kambona alivyojua. Baada ya kwenda Guinea, Hanga alihakikishiwa na Rais wa nchi hiyo, Ahmed Sekou Toure, na Nyerere wa Tanzania, kwamba angekuwa huru na salama akirejea nchini. Hanga alirejeshwa Tanzania kutoka Guinea.

Hanga hakuuona uhuru alioahidiwa na, badala yake, Desemba 1967 alikamatwa kwa tuhuma za uhaini. Alipohoji sababu ya kukamatwa alijibiwa kuwa alikula njama za kuwarubuni maofisa wa jeshi ili aweze kuiangusha serikali ya Sheikh Abeid Karume.

Katika mahojiano aliyoruhusiwa kufanyiwa akiwa rumande, kwa mujibu wa jarida Africa Confidential, Hanga alikana kuhusika kwa vyovyote katika kula njama na maofisa wa jeshi na akasisitiza kwamba siku zote jitihada zake zilikuwa ni katika kutaka kuwapatanisha Kambona na Nyerere.

Mapema mwaka 1969, Kassim Hanga aliachiwa huru kutoka rumande. Badala ya kurejea Zanzibar, aliondoka na kwenda kuishi katika mojawapo ya nyumba zilizomilikiwa na Kambona mjini Dar es Salaam ambayo ilikuwa bado kutaifishwa.

Lakini matatizo yake na serikali za Tanganyika na Zanzibar hayakuwa yamemalizika. Kuna Watanzania ambao hawakuridhishwa na hali ya kisiasa nchini. Miongoni mwa mengi waliyohoji ni suala la Kassim Hanga na ‘udikteta wa Zanzibar’ wakidai kuwa Karume hakutaka uchaguzi kufanyika Zanzibar.

Baada ya kupinga sana sera za serikali, Oktoba 1968, wabunge kadhaa walitimuliwa Bungeni na baadhi ya watu wengine wakakamatwa na kutiwa kizuizini. Hawa walikuwa ni pamoja na Eli Anangisye, Joseph Kasella-Bantu, Christopher Kassanga Tumbo, Ndugu Choga, Ndugu Bakampenja na Ndugu Kaneno.

Taarifa za watu kutiwa kizuizini zilipochapishwa katika gazeti Daily Nation (Okt. 2, 1968) la Kenya, serikali ya Tanzania iliamuru kukamatwa kwa mwandishi wa Kitanzania aliyevujisha habari hizo, Melek Mzirai Kangero.

Baadaye ikajulikana kuwa Hanga na Othman Sharif walikamatwa mjini Dar es Salaam kutokana na shinikizo la Karume aliyewataka watu hao kwa gharama zozote—hata kama ni kwa kuuvunja Muungano.

Othman Sharif, msomi kutoka Chuo cha Makerere, alikuwa mmoja wa waasisi wa Afro-Shirazi na kiongozi wa chama Bungeni wakati Karume akishikilia Urais wa chama.

Mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kudhani kuwa Othman alikuwa na tamaa ya mamlaka ya kisiasa na uwezekano wake wa kula njama za kuiangusha serikali yake, akisaidiwa na Nyerere, Karume alimwondosha Othman Unguja na kufanywa kuwa Balozi.

Kwanza alikuwa Balozi wa Tanzania mjini London, Uigereza, kisha akapelekwa Washington, Marekani. Wakati mmoja, inadaiwa, Othman Sharif aliporudi Zanzibar kwa matembezi aliponyoka kuingia katika kucha za Abeid Karume.

Karume alianza kumwandama kama simba anavyoandama windo lake. Kuona hivyo, Nyerere aliingilia kati mara hiyo hiyo akidai kwamba Othman Sharif alikuwa Balozi wa Muungano wa Tanzania, na si Balozi wa Zanzibar.

Karume alipotambua kuwa hakuwa na mamlaka kisheria ya kumdhibiti Othman, alibadili mbinu ya kumtafuta. Nyerere alipogundua hilo alijaribu kufanya kila mbinu aliyoweza ili Othman asirudi Zanzibar.

Baada ya kupoteza wadhifa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mwalimu Nyerere alimpatia Othman kazi nyingine kwa kumteua kuwa afisa uganga wa mifugo mkoani Iringa.

Lakini hiyo haikumzuia Karume kumwandama hadi mkoani Iringa na, kwa mujibu wa kitabu ‘Conflict and Harmony in Zanzibar’, Karume aliwashawishi Wazanzibari watatu waliokuwa marafiki wa karibu sana wa Othman ili wamsaliti.

Watu hao walikubali. Wakafikishwa mbele ya Baraza la Mapinduzi, wakatoa ushahidi kwa kiapo na kudai kwamba ni kweli Othman Sharif alikula njama za kutaka kuiangusha serikali ya Karume. Watu hao walipelekwa kwa Nyerere na kurudia madai hayo hayo.

Wakati Nyerere anaelekea kuuamini huo ‘mchezo wa kuigiza’, tayari uhusiano kati yake na Karume ulianza kuingiwa na dosari nyingine. Muungano wa Tanganyika-Zanzibar ulikuwa majaribuni.

Hatimaye Nyerere akasema watu hao watapokea “hukumu ya haki” Zanzibar. Gazeti Ulimwengu (Nov. 19, 1967) katika tahariri yake liliandika kuwa lazima hukumu ya haki itolewe. Kisha likaonyesha kupinga suala la watu kuwekwa kizuizini.

Kama matokeo, mhariri wa gazeti hilo, Otini Kambona, alikamatwa. Hata ndugu yake Otini, aliyeitwa Mathias, naye alikamatwa kwa sababu nyingine tofauti kwa madai ya kushiriki katika njama za kuiangusha Serikali.

Kikundi cha viongozi kutoka mkoani Iringa, ambako Sheikh Sharrif alikuwa akifanya kazi, walimsihi sana Nyerere asiruhusu watu hao wapelekwe Zanzibar kwani walijua hatima yao.

Jawabu la Nyerere lilikuwa hivi: “…Hili si jambo la ubishi kwa sababu halina uzito wa kubishaniwa. Lakini kama kutakuwa salama, ni vizuri tukajua watu hawa watakuwa salama kiasi gani.” Lakini historia ni shahidi. Hakukuwa na usalama wa kiasi chochote. Wanadamu hawa walinyang’anywa haki yao ya kuishi.

Baada ya kuona kuwa mambo yameshindikana, na kwa kuwa Muungano wa Tanzania ndilo lililokuwa suala kuu katika akili yake, Mwalimu ‘alibwaga manyanga’. Septemba 1969 Nyerere akajikuta akiwapa idhini maofisa wake kuwatoa Kassim Hanga na Othman Sharif wakabidhiwe SMZ kama Abeid Karume alivyotaka.

Walipelekwa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Dar es Salaam (DIA), wakipewa maneno ya kuwafariji, na kisha wakasafirishwa kwenda Zanzibar. Hiyo ikawa ndiyo safari yao ya mwisho—angalau safari ya mwisho kutoka Dar es Salaam—tena, inadaiwa, wakiwa na wamefungwa pingu.
Huko ndiko walikokutana na mauti yao, pengine kwa kupigwa risasi—ingawa taarifa nyingine zilisema kuwa waliuawa kwa kuzamishwa katika maji. Lakini, kinasema kitabu ‘Conflict and Harmony in Zanzibar’, hata wale waliomsaliti Othman Sharif nao waliuawa mmoja baada ya mwingine. Machapisho mengine ya kihistoria yanaunga mkono madai hayo.

Katika hotuba aliyoitoa Oktoba 1969, ukiwa ni mwezi mmoja baada ya kufanyika kwa mauaji hayo, Abeid Karume alitangaza kuwa watu wanne waliokuwa wakila njama za kuiangusha serikali yake “…wameuawa kwa kupigwa risasi.” Hili alilikiri mwenyewe.

Vyanzo kadhaa vinasema kuwa Kassim Hanga, na aliyekuwa Waziri wa Elimu na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Sheikh Othman Sharrif, waliuawa Zanzibar na utawala wa Karume.

Hata hivyo mauaji hayo hayakuwa mwisho wa mambo. Inaelekea kuanzia hapo, au kabla ya hapo, kulijengeka utamaduni wa kuwakamata watu, kuwaweka kizuizini na hatimaye wengine kuuawa.

Zaidi ya watu kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka, kulikuwa na madai ya kuweko kwa zile kambi za mateso. Kwa mfano katika miaka ya 1960 na mwanzoni mwa 1970, inasemwa, Zanzibar kulikuwa na ile kambi iliyoitwa ‘Kwa Bamkwe’ au ‘Kwa Mandera’.

Mkoani Mwanza kaskazini mwa Tanzania kulikuwa na (kambi ya) Kigoto. Hiyo ni moja ya kambi zilizokuwa mbaya. Baada ya kuwakamata watu kwa tuhuma za uchawi mwaka 1977 katika maeneo ya Mwanza na Shinyanga, ikijumlishwa na matendo waliyofanyiwa watu hao, ilitosha kumfanya Alhaj Ali Hassan Mwinyi kujiuzulu ‘kwa kuwajibika’.

Ingawa wengi walitarajia kuwa kuwajibika huko kungekuwa ndio mwisho wa Mwinyi katika siasa, Nyerere ‘alimpigia debe’ kuwa Rais wa Zanzibar (Jan. 30, 1984—Okt. 24, 1985) na hatimaye Rais wa Tanzania (Nov. 5, 1985—Nov. 23, 1995) kwa kura za NDIYO.

Kwa mujibu wa kitabu ‘Zanzibar: Kinyang’anyiro na Utumwa’, mwanasiasa aliyekuwa Unguja wakati mambo yote hayo yakitokea, Issa bin Nasser Al-Ismaily, anaandika kuwa mwaka 1970 Wazanzibari tisa “walitiwa nguvuni na Serikali ya ASP kwa kisingizio cha kutaka kuipindua serikali hiyo.”

Wazanzibari hao ni Salim Ahmed Busaidi, Abdallah Suleiman Riyami, Othman Soud, Aziz Bualy, Hemed Said, Muhammed Juma, Muhammed Hamza, Musa Ali na Said Hamoud.

Bila ya kufikishwa mahakamani, Karume aliwahukumu kutupwa gerezani na kupewa kazi ya kuchunga ng’ombe katika uwanda wa “Hanyagwa-Mchana”. Baada ya kifo cha Karume Aprili 1972, “wananchi hao waliuawa wakati wa utawala wa mrithi wa Karume, Aboud Jumbe.”

Kitabu hicho kinaomboleza hivi: “…Mwenyezi Mungu mwenyewe anaelewa namna ya kuihukumu dhuluma hii iliyotendeka…; kwani Mwenyezi Mungu ndiye mjuaji wa yote.” Ni kweli kwamba “Mwenyezi Mungu ndiye mjuaji wa yote” kwa sababu hakuna mwanadamu atakayejua yote yaliyotendeka, hasa yale ambayo hayatajulikana kamwe.

********************************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754 989 837. E-mail: shao2020@yahoo.co.uk., Blog: willyshao.blogspot.com.
********************************************************

1 comment:

Tim Hunt said...

Can you confirm that Otini Kambona is also know as Mathias Kambona?

Is Mathias nickname or given name?