Monday, February 5, 2007
Kilichomtokea Kambona Tanzania
KILICHOMTOKEA KAMBONA BAADA YA MAASI YA TANGANYIKA
Na William Shao
KATIKA toleo lililopita nilijaribu kuonyesha madai na ushahidi wa mazingira unaoonyesha kuwa usiku wa Januari 18-19, 1964, Oscar Kambona, au watu wake, walikuwa wafanye mapinduzi ya Tanganyika na Kassim Hanga, usiku huo huo, angefanya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kilichovuruga mambo ni kwamba John Okello aliwahi kufanya mapinduzi ya Zanzibar juma moja kabla na hivyo mipango mingi iliyokuwa imeandaliwa ikaharibika.
Wasomaji wengi walinipigia simu kutaka kujua yaliyowafika Kambona na Hanga baada ya matukio hayo muhimu ya kihistoria. Ukweli ni kwamba ni vigumu kwa mambo yote kujulikana. Lakini yale yaliyoonekana na kuandikwa yanaweza kusemwa.
Ingawa nilitaka kuleta mada nyingine, nitajaribu kueleza kwa ufupi machache sana yaliyo katika historia. Lakini, kama kisemavyo kitabu kiitwacho Zanzibar: Kinyang’anyiro na Utumwa cha Issa bin Nasser Al-Ismaily, “Mwenyezi Mungu ndiye mjuaji wa yote”, hakuna mwanadamu atakayejua yote yaliyotendeka.
Uhusiano kati ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyezaliwa Alhamisi ya Aprili 13, 1922 huko Musoma (alifariki 1999) na Oscar Salathiel Kambona aliyezaliwa Jumamosi ya Agosti 13, 1928 huko Songea (alifariki 1997) ulianza kuzorota mara baada ya Muungano wa Tanganyika-Zanzibar na wala si wakati ule ule wa ‘Mapinduzi ya Tanganyika’ (Maasi).
Katika kipindi cha mwaka 1964—66, urafiki kati ya Oscar Kambona na Kassim Hanga uliongezeka zaidi kuliko ulivyokuwa awali, pengine hali hiyo ilitokana na matatizo ya Kassim Hanga, na kwa ajili hiyo Hanga alijikuta amenasa katikati ya ugomvi—au mgogoro wa uongozi—uliokuwepo kati ya Nyerere na Kambona. (Rejea RAI No. 693).
Ugomvi huo uliongezeka na kuzaa uhasama, na uhasama huo ukabadilika kutoka katika hali yake mbaya na kuwa katika hali mbaya zaidi.
Uhasama huo ulizidi zaidi ilipojulikana kwa Nyerere kwamba Kambona alikuwa na mawasiliano na Wakomunisti wa Ulaya na kwamba maoni yake kuhusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) yalitofautiana kabisa na yake (Nyerere).
Isitoshe, fununu alizopewa Nyerere kwamba Kambona alihusika kwa kiasi fulani katika kupanga mapinduzi ya Tanganyika zilifanya uhusiano huo kuharibika zaidi.
Hata hivyo, katika zile siku za kwanza, muda mfupi tu kabla ya Muungano kufanyika, Nyerere alikuwa anamwonea Kambona huruma wakati Kambona alipomlalamikia bosi wake kuwa alikuwa hajisikii vizuri kiafya.
Mwalimu Nyerere alimfanyia Kambona mpango wa kwenda nchini Netherlands kwa matibabu, na gharama zote zililipwa na Serikali ya Tanganyika. Lakini sasa wakiwa wametumbukia katika mgogoro wa wao kwa wao, Nyerere akagundua kuwa kutawala watu hakuhitaji huruma.
Kuanzia wakati huo aliendelea kuamini kwamba kushughulika na watu hakuhitaji sana mtu kuwa upole.
Ingawa alikuwa akiishikilia imani hiyo kimya kimya, ilipofika Jumatatu, Agosti 16, 1993, alitamka imani hiyo waziwazi alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam. Alisema: “Mambo ya nchi hayapendi upole sana. Siku nyingine lazima uwe rough.”
Mwaka 1966 Mwalimu Nyerere alihisi kwamba katika serikali yake kulikuwa na kile alichodai kuwa ni “utovu wa nidhamu.” Hilo lilitosha kumfanya Kambona—Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje—apoteze nyadhifa zake katika serikali ya Nyerere.
Ilionekana kwamba dawa ya Kambona ilikuwa inapikwa jikoni kwa Nyerere, na mpishi alikuwa Nyerere mwenyewe. Dawa hiyo iliyoitwa Azimio la Arusha iliyoanza kupikwa katikati ya 1966 ingetumika kama silaha ya kupunguza nguvu za wale wanasiasa waliokuwa na uwezo kipesa.
Mmoja wa wanasiasa hao ni Oscar Kambona. Baada ya dawa hiyo kupikwa na kuiva, mali za watu binafsi, zikiwemo zile za Kambona mwenyewe, zilianza kutaifishwa na kufanywa ‘mali ya umma kwa manufaa ya umma’. Kambona alipoteza mali nyingi alizokuwa amejilimbikizia.
Jambo baya zaidi kwa Kambona lilikuwa ni madai dhidi yake kuhusiana na pesa alizotumia lakini mahesabu yake yakawa hayalingani na matumizi. Alitakiwa kuzitolea maelezo. Na alijua alipaswa kufanya hivyo.
Lakini aliikimbia nchi kabla hajaambiwa afanye hivyo. Jumanne ya Januari 23, 1968, tarehe ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya ufunguzi wa kikao cha Bunge la Muungano kwa mwaka huo, Bunge lilitajiwa mali za Oscar Kambona.
Kikao hicho kilielezwa kuwa “Kambona ameikimbia nchi mwishoni mwa mwaka jana (1967)” na kwamba kabla hajaondoka, Tshs. 500,000/- ziliingizwa kwenye akaunti yake mjini Dar es Salaam kutoka benki moja ya Uingereza ambayo haikujulikana ni benki gani. (‘Hansard’—kumbukumbu rasmi za mijadala ya bunge, hazielezi hiyo ilikuwa ni benki gani).
Pesa hizo, kwa mujibu wa ‘Hansard’, ziliingizwa katika akaunti hiyo Jumanne ya Desemba 6, 1966. hiyo ilikuwa ni miezi miwili kabla ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Hayo yalisemwa na Makamu wa Pili wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa, alipokuwa akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Rombo, Bw. Maskini.
Miezi mitano baada ya Azimio la Arusha—Julai 1967—ilielezwa kuwa kiasi kikubwa cha pesa kilikuwa kikiingia katika akaunti ya Kambona ambaye pia alidaiwa kumiliki majumba katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Songea ambazo kwa pamoja zilikuwa na thamani ya Tsh. 485,612/-
Rashidi Kawawa alisema kulingana na uchunguzi uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya Kambona kuikimbia nchi, uligundua kwamba kati ya mwezi Juni 1965 na Desemba 1966, Kambona aliingiza katika akaunti yake mjini Dar es Salaam kiasi cha Shs. 896,800/-. Pia haikuelelezwa akaunti hiyo ni ya benki gani.
Matokeo ya uchunguzi wa BoT yalionesha yafuatayo:-
Mwezi Juni 1965, Oscar Kambona aliingiza kwenye akaunti yake Tshs. 65,800/- ambazo zilikuwa ni kwa pauni ya Uingereza.
Julai 1967 aliingiza Tshs. 60,000/- kwa pauni ya Uingereza.
Februari 1966 aliingiza kiasi cha Tshs. 60,000/ ambazo zilikuwa ni kwa Shilingi ya Tanzania.
Julai 1966 aliingiza kiasi cha Tshs. 60,000/- kwa shilingi ya Tanzania.
Septemba 1966 aliingiza Tshs. 70,000/- kwa shilingi ya Tanzania.
Ilielezwa pia kwamba Kambona alikuwa akilimiki majumba mengi katika maeneo kadhaa ya nchi kabla hajatorokea Nairobi, Kenya, kisha London, Uingereza. Majumba yaliyotajwa Bungeni ni pamoja na:-
Nyumba iliyoko Magomeni kwenye Ploti No. 29, 30 na 31 iliyokuwa na thamani ya Tshs. 30,000/-
Nyumba iliyoko Kunduchi kwenye Ploti No. 28 aliyoinunua kwa jumla ya Tshs. 12,000 na kulipa pesa taslim.
Nyumba iliyoko Msasani Beach, Ploti No. 92 iliyojengwa kwa gharama ya Tshs. 392,612 bila kuhesabu gharama nyingine za vyombo vya ndani.
Nyumba iliyoko Songea, Ploti No. 21 aliyoinunua kwa pesa taslimu Tshs. 15,000
Nyumba iliyoko Morogoro, Ploti No. 89 aliyoinunua kwa pesa taslimu Tshs. 36,000.
Kwa kutazama mtiririko huo wa madai, Jumapili ya Januari 12, 1969, Nyerere alikwenda Zanzibar kuhudhuria sherehe za kuadhimisha miaka minne ya Mapinduzi ya Zanzibar. Alipohutubia katika maadhimisho hayo, alimtaja Kambona kama “…mwizi na mhuni wa kisiasa.”
Baadaye kutaifisha majumba kukatengenezewa sheria yake mwaka 1971—miaka minne baada ya Azimio la Arusha. Lakini majumba mengine yaliyotaifishwa yalianza kurejeshewa wenyewe kwa njia za kutatanisha.
Kwa mfano, Oktoba 1972, jumba moja kubwa mjini Dar es Salaam lililotaifishwa chini ya Sheria ya Kutaifisha Majumba ya Mwaka 1971, lilirudishiwa mwenyewe katika hali ya kutatanisha, na kisha likauzwa kwa bei ya Tshs. milioni 1.5.
Jumba hilo lililoko kwenye kona ya mitaa ya Makunganya na Azikiwe lililokuwa mali ya ‘Haji Brothers & Co. Ltd.’, liligundulika kuwa lilirudishwa kwa Bwana Abdul Haji Oktoba 1972 kwa amri ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini, Thabita Siwale, bila ya kuwako maelezo yoyote ya kuhalalisha hatua hiyo kisheria.
Waziri Siwale alithibitisha kwamba sababu za Abdul Haji hazionyweshi mahali popote katika majalada ya Wizara inayohusiana na jumba hilo, lakini akaongeza kwamba kutokana na hali ya kifedha ya Bwana Haji, haiyumkiniki kuwa alirudishiwa jumba hilo kwa kuhurumiwa kutokana na kutokuwa na njia nyingine ya kujipatia fedha za kumwezesha kuishi. Abdul Haji alikuwa Mwenyekiti wa Kampuni kubwa iliyoitwa ‘Industrial Promotion Services’ (IPS).
Uchunguzi ulithibitisha kwamba Jumatatu ya Oktoba 16, 1972, Bwana Haji alimwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini akimwomba amrudishie jumba lake lililokuwa chini ya Mamlaka ya Msajili wa Majumba baada ya kutaifishwa mwaka 1971.
Siku tano baada ya hapo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alimwandikia Bwana Haji akimwarifu kwamba ameagizwa na Waziri wake kumfahamisha kuwa Waziri ameidhinisha kurudishwa kwa jumba hilo ili kumwezesha Abdul Haji kuliuza kwa Shirika la Nguo la Taifa (NATEX). Haijulikani kama Kambona angeandika barua kama alivyofanya Bw. Haji angekubaliwa na kurudishiwa mali zake.
Ingawa Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Tanzania na Katibu Mkuu wa chama cha TANU, alikuwa ameikimbia nchi tangu mwishoni mwa 1966 au mwanzoni mwa 1967, kiasi cha miezi saba baadaye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilimwandikia barua kumtaka aeleze ni kiasi gani cha pesa alichoibakizia nchi na pia aeleze alikopata fedha za kigeni alizotumia kulipia kodi nchini Kenya kwenye Uwanja wa Ndege wa Nairobi alipokuwa akiondoka yeye na familia yake kwenda Uingereza
Madai hayo ya BoT yalielezwa na Waziri mdogo wa Fedha, Bw. S. Rashid, alipokuwa akijibu swali kutoka kwa Mbunge Mgaza wa Bagamoyo.
Kambona alikuwa mwanasiasa wa Tanganyika na alijua mambo mengi kuhusu Serikali ya Tanganyika na viongozi wanaohusika nayo.
Kwa hivyo inaelekea alijua jambo ambalo lingefuata baada ya tangazo, au tamko, la Azimio la Arusha lililotolewa Jumapili ya Februari 5, 1967. Huenda angekamatwa na kuhojiwa—au jambo baya zaidi kuliko kukamatwa na kuhojiwa lingetokea.
Ingawa alicharukia siasa za Tanganyika hata kabla ya kuzaliwa kwa TANU, jina lake lilianza kusikika zaidi wakati chama cha TAA kilipofanya mkutano wake mkuu Jumamosi ya Oktoba 10, 1953, katika nyumba iliyokuwa mtaa uliojulikana kama New Street mjini Dar es Salaam.
Sasa mtaa huo unaitwa Lumumba kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Congo aliyeuawa, Patrice Lumumba. Wakati huo waliokuwa machachari zaidi katika kutafuta wanachama wa TANU ni Kambona na Bibi Titi Mohamed, pengine kuliko Nyerere mwenyewe (Tanganyika Standard, Sept. 27, 1955)
Mwanzoni mwa 1954 Nyerere na Kambona walikutana kwa mara ya pili wakiwa Dodoma pamoja na mtu mwingine aliyeitwa Kanyame Chiume, ambaye ni Mnyasa.
Kwa mara ya nne Kambona alikutana na Nyerere katika Mkutano Mkuu wa TAA ulioanza Jumapili, Julai 4, 1954, katika chumba kidogo cha makao makuu ya Chama. Wengine waliokuwepo ni pamoja na John Rupia, Abdulwahid Sykes, Ally Sykes na Dossa Aziz.
Katika mkutano huo neno Tanganyika African National Union (TANU) lilibuniwa na Ally Sykes. Mkutano ulipomalizika Jumatano ya Julai 7, 1954, TANU ikawa imezaliwa rasmi. Nembo ya kadi za kwanza za TANU zilizosanifiwa na Ally Sykes.
Juhudi za Kambona na viongozi wengine zilikiwezesha TANU kudumu muda mrefu hadi kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika. Ingawa hivyo, kazi zote alizofanya na matunda yake yote yalifikia kikomo mwaka 1967.
Kutokana na uzoefu wake huo katika siasa za Tanganyika, na kwa kuwa yeye alikuwa katika mfumo wa utawala, inaelekea aligundua mapema hatari iliyokuwa inamjia wakati alipotakiwa kutoa maelezo ya pesa zake na pia aliposikia kuanzishwa kwa Azimio la Arusha.
Baada ya kuyatafakari yote hayo kwa haraka, Kambona hakukawia sana. Aliondoka haraka na kwenda Nairobi, Kenya, na kutokea huko alipanga safari ya kwenda Uingereza.
Kama alivyowaambia baadhi ya Watanzania waliokuwa Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 1970, Kambona aliikimbia nchi aliyoiita, “Tanzania ya Nyerere na Karume.”
Kassim Hanga, ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa kisiasa wa Kambona, kama ilivyokuwa kwa Kambona mwenyewe, naye alipoteza nyadhifa zake katika Serikali ya Muungano.
Ingawa huyu hakufukuzwa wala kutakiwa kutoa maelezo ya madai yoyote ya kweli au ya uongo yaliyomkabili, alijikuta hana wadhifa wakati yalipofanyika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.
Tofauti na Kambona, Kassim Hanga hakukimbia nchi. Pengine alijua kwanini. Pengine hakujua kwanini, na labda hakujua mambo mengi kuhusu Tanzania kama Kambona alivyojua.
Alidhani mambo yangekwisha na yeye abaki salama hata kama hakuwa na wadhifa wowote serikalini. Lakini hali haikwenda kama alivyofikiria. Desemba 1967 alikamatwa na kutuhumiwa uhaini.
Alipotaka kujua sababu ya kukamatwa kwake, alijibiwa kuwa alikula njama za kuwarubuni maofisa wa jeshi ili aweze kuiangusha serikali.
Katika mahojiano aliyoruhusiwa kufanyiwa akiwa rumande, kwa mujibu wa Africa Confidential, Kassim Hanga alikana kuhusika kwa vyovyote na kula njama na maofisa wa jeshi na akasisitiza kwamba siku zote jitihada zake zilikuwa ni katika kutaka kuwapatanisha Kambona na Nyerere.
Mapema mwaka 1969, Kassim Hanga aliachiwa huru kutoka rumande. Badala ya kurejea Zanzibar, aliondoka na kwenda kuishi katika mojawapo ya nyumba zilizomilikiwa na Kambona mjini Dar es Salaam ambayo ilikuwa bado kutaifishwa.
Lakini matatizo yake na serikali za Tanganyika na Zanzibar hayakuwa yamekwisha. Mambo hayakuwa yamefikia mwisho. Pengine ulikuwa mwanzo wa mwisho wake.
Ndipo mwaka huo huo Hanga na Othman Sharif wakakamatwa mjini Dar es Salaam kutokana na shinikizo la Karume. Karume aliwataka watu hao kwa gharama zozote—hata kama ni kuuvunja Muungano.
Nyerere kusikia hivyo, inaelekea alihisi kile ambacho kingewatokea watu hao. Kwa muda fulani Nyerere alikaidi matakwa ya Karume ya kumtaka kuwatoa watu hao ili wapelekwe Unguja ambako pengine aliamini kuwa hakukuwa salama kwa uhai wao.
Pale mwanzoni, jawabu la Nyerere lilikuwa: “…Hili si jambo la ubishi kwa sababu halina uzito wa kubishaniwa. Lakini kama kutakuwa salama, ni vizuri tukajua watu hawa watakuwa salama kiasi gani.”
Haikujulikana kama kweli alikuwa akiwatetea Hanga na Sharif kwa kuhofia usalama wao au ulikuwa ni msimamo wake tu wa kutafuta haki, lakini alikuwa akizungumzia hukumu ya Unguja. Hata hivyo shinikizo kutoka kwa Karume lilikuwa kubwa zaidi na zaidi kadiri siku zilivyopita.
Othman Sharif, msomi kutoka Chuo cha Makerere, alikuwa mmoja wa waasisi wa Afro-Shirazi na kiongozi wa chama bungeni wakati Karume akishikilia Urais wa chama hicho.
Mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kudhani kuwa Othman alikuwa na tamaa ya mamlaka ya kisiasa na uwezekano wake wa kula njama za kuiangusha serikali yake, akisaidiwa na Nyerere, Karume alimwondosha Othman Unguja na kufanywa kuwa balozi.
Kwanza alikuwa Balozi wa Tanzania mjini London, Uigereza, kisha akapelekwa Washington, Marekani. Wakati mmoja, inadaiwa, Othman Sharif aliporudi nyumbani Zanzibar kwa matembezi aliponyoka kuingia katika kucha za Abeid Karume.
Karume alianza kumwandama kama simba anavyoandama windo lake. Kuona hivyo, Nyerere aliingilia kati mara hiyo hiyo akidai kwamba Othman Sharif alikuwa Balozi wa Muungano wa Tanzania, na si Balozi wa Zanzibar.
Kwa kusikia hivyo, Karume akatambua kuwa hakuwa na mamlaka kisheria ya kumdhibiti Othman. Alibadilisha njia ya kumtafuta, lakini Nyerere naye akatambua hilo. Akajaribu kufanya kila mbinu aliyoweza ili Othman asirudi Zanzibar baada ya kupoteza wadhifa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani.
Mwalimu Nyerere aliamua kumtafutia kazi nyingine. Alimteua kuwa afisa uganga wa mifugo mkoani Iringa—mbali na Unguja. Kwa wanahistoria wanaochambua mambo wanadai kuwa Karume hakuwa aina ya mtu ambaye angekubali kunyang’anywa windo lake bila kujibu mapigo.
Karume alimwandama Othman hadi mkoani Iringa na, kwa mujibu wa kitabu ‘Conflict and Harmony in Zanzibar’, Karume aliwashawishi Wazanzibari watatu waliokuwa marafiki wa karibu sana wa Othman wamsaliti.
Watu hao walikubali. Walifikishwa mbele ya Baraza la Mapinduzi, wakatoa ushahidi kwa kiapo na kudai kwamba ni kweli Othman Sharif alikuwa anakula njama za kutaka kuiangusha serikali ya Karume. Watu hao walipelekwa kwa Nyerere kurudia madai hayo hayo.
Uhusiano kati ya Nyerere na Karume ukakaribia kuingia dosari nyingine—tena dosari kubwa. Huo ulikuwa wakati mwingine ambao Muungano wa Tanganyika-Zanzibar uliingia majaribuni.
Huenda katika akili ya Nyerere aliogopa kubadilisha uhai wa watu kwa ajili ya kuulinda Muungano, lakini kama ndivyo akili yake ilivyoona, basi inaelekea kuwa hatimaye aliamua watu hao wawili waondoke ili Muungano ubaki.
Kwa hiyo baada ya kuona kuwa mambo yameshindikana, na kwa kuwa Muungano wa Tanzania ndilo lililokuwa suala kuu katika akili yake, Mwalimu ‘alibwaga manyanga’. Hatimaye akakubali kuwakabidhi Othman Sharif na Kassim Hanga kwa SMZ kama Karume alivyotaka.
Nyerere, bila kupenda, Septemba 1969 akajikuta akiwapa idhini maofisa wake kuwatoa Hanga na Sharif ili wapelekwe Zanzibar kama Abeid Karume alivyotaka.
Walipelekwa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Dar es Salaam (DIA), wakipewa maneno ya kuwafariji, na kisha wakasafirishwa kwenda Zanzibar. Hiyo ikawa ndiyo safari yao ya mwisho—angalau safari ya mwisho kutoka Dar es Salaam.
Walipelekwa Zanzibar ambako inadaiwa waliuawa—huenda kwa kupigwa risasi—ingawa taarifa nyingine zilisema kuwa waliuawa kwa kuzamishwa katika maji. Othman alikamatwa, akapelekwa Zanzibar akiwa amevalishwa pingu.
Lakini, kinasema kitabu Conflict and Harmony in Zanzibar, hata wale waliomsaliti Othman Sharif nao waliuawa mmoja baada ya mwingine. Hayo ndiyo machapisho ya kihistoria.
Katika hotuba aliyoitoa Oktoba 1969, ukiwa ni mwezi mmoja baada ya kufanyika kwa mauaji hayo, Abeid Karume alitangaza kuwa watu wanne waliokuwa wakila njama za kuiangusha serikali yake “…wameuawa kwa kupigwa risasi.”
Lakini mauaji hayo hayakuwa mwisho wa mambo. Inaelekea kuanzia hapo, au kabla ya hapo, kulijengeka utamaduni wa kuwakamata watu, kuwaweka kizuizini na hatimaye wengine kuuawa. Kwa mujibu wa kitabu Zanzibar: Kinyang’anyiro na Utumwa, mwanasiasa aliyekuwa Unguja wakati mambo yote hayo yakitokea, Issa bin Nasser Al-Ismaily, anaandika kuwa mwaka 1970 Wazanzibari tisa “…walitiwa nguvuni na Serikali ya ASP kwa kisingizio cha kutaka kuipindua serikali hiyo.”
Wazanzibari hao ni Salim Ahmed Busaidi, Abdallah Suleiman Riyami, Othman Soud, Aziz Bualy, Hemed Said, Muhammed Juma, Muhammed Hamza, Musa Ali na Said Hamoud. Bila ya kufikishwa mahakamani, Karume aliwahukumu kutupwa gerezani na kupewa kazi ya kuchunga ng’ombe katika uwanda wa “Hanyagwa-Mchana”. Baada ya kifo cha Karume Aprili 1972, “wananchi hao waliuawa wakati wa utawala wa mrithi wa Karume, Aboud Jumbe.”
Kitabu hicho kinaomboleza hivi: “…Mwenyezi Mungu mwenyewe anaelewa namna ya kuihukumu dhuluma hii iliyotendeka…; kwani Mwenyezi Mungu ndiye mjuaji wa yote.” Ni kweli kwamba “Mwenyezi Mungu ndiye mjuaji wa yote” kwa sababu hakuna mwanadamu atakayejua yote yaliyotendeka.
********************************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754 989 837. E-mail: shao2020@yahoo.co.uk., Blog: willyshao.blogspot.com.
********************************************************
Labels:
Uchambuzi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment