Monday, February 5, 2007
HABARI PEKE YAKE HAZIHEKIMISHI
HABARI NYINGI HUELIMISHA AU HUPUMBAZA?
Na William Shao
Katika kipindi cha karne moja iliyopita kumekuwa na habari nyingi zisizo na kifani, iwe ni kwa chapa, redio, televisheni, internet, au kwa njia nyingine yoyote. Kwa ujumla dunia imejaa habari kuliko wakati mwingine wowote katika historia. Watu wanaoishi katika enzi hii ya habari wana hekima zaidi kuliko wale walioishi enzi ya ujima? Je, hizo ni habari nyingi kupita kiasi?
Katika kitabu chake, Data Smog—Surviving the Information Glut, David Shenk anaandika hivi: “Habari nyingi kupita kiasi zimekuwa tishio halisi …Sasa tunakabiliana na matazamio ya kujazwa habari nyingi kupita kiasi.” Anamaanisha nini?
Utafiti wa gazeti hili umegundua kwamba toleo moja la gazeti Mtanzania, au The African, lina habari nyingi kuliko zile ambazo mtu wa kawaida angeweza kuzipata katika muda wote wa maisha yake katika karne ya 14 au 15 nchini Uingereza.
Haishangazi kwamba kuna karibu majarida milioni moja ya kisayansi duniani pote, na internet ina maktaba nyingi sana za habari kwa watumiaji wa kompyuta. Lakini kuna mamilioni mengine ya majarida na magazeti.
Utafiti wa Richard Wurman aliouchapisha katika kitabu Information Anxiety, umegundua hivi: “Mashirika ya utangazaji wa biashara yametangaza vita dhidi ya hisia zetu …Dunia inaitikia habari za vyombo vya habari ambazo kwa hakika ni sehemu tu ya kiwakilishi cha mambo ya hakika na matukio, si habari kamili.”
Ingawa matokeo ya utafiti wake hayako dhahiri sana, wasomaji wa historia ya hivi karibuni watakumbuka kwamba habari ilikuwa ni orodha tu ya mambo ya hakika au ‘data’ ikitueleza kinaganaga kama vile nani, wapi, nini, lini au vipi. Huo ndio msingi wa habari. Hakukuwa na lugha au msamiati maalum wa habari. Kile tu tulichohitaji kufanya ni kuomba kupata habari au kuitafuta sisi wenyewe.
Lakini sasa watu wamebuni maneno mapya mengi sana yanayohusiana na habari kiasi kwamba maneno yenyewe yanatosha kusababisha vurugu. Leo dunia imepatwa na ugonjwa unaojulikana kama infomania, yaani imani ya kwamba kadiri mtu anavyokuwa na habari nyingi zaidi ndivyo alivyo na faida zaidi kuliko yule ambaye hana habari nyingi au asiyeweza kuzipata kwa urahisi.
Neno ‘mania’ linamaanisha ‘wazimu’. Hivyo ‘infomania’ ni ‘kichaa cha habari’. Kichaa hiki kinaongezewa na mafuriko ya mifumo mingi ya mawasiliano. Hii imesababisha kipindi hiki cha wakati kuitwa ‘enzi ya habari’ (information age).
Kwa kuwa enzi ya habari imegeuza kabisa namna watu wanavyoishi na kufanya kazi, imefanya watu wengi wateseke kutokana na ‘kuhangaikia habari’. Lakini kwanini wanahangaika?
Utafiti wa gazeti hili umegundua kwamba kuhangaikia habari kunasababishwa na pengo linalozidi kuongezeka kati ya yale tunayoelewa na yale tunayofikiri kwamba tunalazimika au kupaswa kuelewa. Kuhangaikia habari kunasababishwa na kinachokosekana kati ya data na ujuzi.
Richard Wurman katika kitabu chake, Information Anxiety, anaiona hali hiyo kwa njia tofauti. Anaandika hivi: “Kwa muda mrefu watu hawakutambua kiasi cha mambo ambayo hawakujua. Hawakujua kuwa kulikuwa na mambo mengi ambayo hawakujua. Lakini sasa watu wanajua kwamba kuna mambo ambayo hawajui, na hilo ndilo linalowafanya wahangaike.”
Matokeo yake ni kwamba wengi wanahisi kuwa wanapaswa kujua mengi kuliko yale wanayojua. Kukiwa na habari nyingi sana tunazoletewa na vyombo vya habari, tunachukua sehemu ndogo sana za data. Lakini mara nyingi hatuna hakika tufanye nini na hizo data. Na wakati huo huo, huenda mtu mmoja akafikiri kwamba kila mtu mwingine, isipokuwa yeye, anajua na kuelewa mengi zaidi kuliko yeye. Na huo ndio mwanzo wa kuhangaika.
Hata hivyo, David Shenk katika kitabu kilichotajwa hapo juu, Data Smog—Surviving the Information Glut, anasema: “Habari zikizidi mno huchafua data na kuzitia ukungu. Ukungu wa data huzuia; hautoi nafasi ya dakika chache za ukimya na kutafakari, na unazuia kufikiria kwa makini kunakohitajiwa sana …unatusababishia mkazo wa akili.”
Ni kweli kwamba habari nyingi kupita kiasi, kama ilivyo kwa mambo yote yanayopita kiasi, husababisha usumbufu. Lakini kwa kutazama mambo bila upendeleo, ni bora zaidi kuwa na habari nyingi kuliko kutokuwa na habari zozote, au ni bora zaidi kuwa na habari nyingi kuliko kutokuwa na habari za kutosha.
Lakini inakuwa mbaya zaidi tunapokuwa na habari tunazofikiri kwamba zinatosha, kumbe ni uongo. Mwandishi wa kitabu cha Megatrends anaonya hivi: “Tumetumbukia katika wingi wa habari lakini tuna njaa ya kujua.”
Binadamu yeyote anahitaji kuarifiwa vizuri, lakini kuwa na kiasi kikubwa sana cha habari hakuelimishi, kwa sababu nyingi ya zile habari zinazoonekana kuwa habari huhusisha tu mambo matupu au data zisizokamilika, au isiyohusiana na mambo ya kweli na yaliyo halisi.
Kwa mujibu wa utafiti wa safu hii, habari peke yake haielimishi. Hatuwezi kufafanua ni ipi habari iliyokosewa, au iliyo kinyume, au propaganda katika mazingira yanayotawala habari. Ni mara ngapi habari za magazeti zimekanushwa na kisha magazeti hayo kuomba radhi? Hilo linamaanisha habari hizo hazikuwa sahihi zilipoandikwa kwa mara ya kwanza.
Utafiti wa Joseph Esposito, msimamizi wa uchapaji wa The New Encyclopedia Britannica, uligundua kuwa, “Habari nyingi za Enzi ya Habari hutumiwa vibaya tu; ni kelele tu zisizofaa. Ongezeko kubwa la habari huzuia uwezo wetu wa kusikia mengi yanayofaa. Na ikiwa hatuwezi kusikia, hatuwezi kuona.”
Mtafiti mwingine, Dk. Frederick Cohen, katika kitabu chake, Protection and Security on the Information Superhighway, anaona kwamba, “…Hakuna yeyote anayejua ni kiasi gani cha mawasiliano ya umma ambacho ni habari za uongo, ambazo zinadai kuwa zinasema jambo fulani lakini kwa hakika hazisemi jambo lolote.”
Ni kweli kwamba kuwa na habari ni jambo bora, lakini kuwa na habari nyingi kuna faida siku zote? Ingawa habari nyingi zaidi hutoa nafasi nyingi zaidi, zinaweza kumfanya mtafutaji ahangaike sana, akijiuliza ikiwa amechunguza au amepata habari yote inayoweza kupatikana.
Utafiti wa kitabu cha Logic or the Art of Thinking umegundua kwamba, “…habari si njia ya kuelekea kuelimika. Habari yenyewe haitoi nuru kuhusu maana ya maisha yetu. Habari haihusiani sana na kupata hekima. Habari peke yake haihekimishi.”
Kitabu Introduction to the Philosophy of Mind (Lowe) kina mtazamo mwingine kuhusiana na habari. Kinasema: “Kwa kweli, kama mali nyingine, habari yaweza kwa hakika kuzuia hekima. Tunaweza kujua mengi mno kama vile tunavyoweza kuwa na vitu vingi mno, halafu tusiweze kuvitumia.”
Habari nyingi zinazopatikana na namna zinavyotolewa inafanya habari nyingi zisiwe na faida kwetu. Ni sawa na mtu mwenye kiu aliyepewa kikombe akinge maji kutoka katika bomba la maji la kuzimia moto. Habari zinazotosha zinapaswa kukadiriwa, si kwa wingi, bali kwa ubora na manufaa yake kwetu. Kwanini ni vizuri kukadiria kwa ubora na si kwa wingi?
Andrea Griffiths na Bob Norton katika kitabu chao, Handling Information Overload In a Week, wanasema jamii ina maoni ya habari ambayo, “zijapovutia sana, hatimaye zinazuia lengo lililokusudiwa.”
Kitabu cha Stuart MacDonald, Information for Innovation: Managing Change From an Information Perspective, kinatoa mwongozo huu: “…Jiulize, je, habari hii ni muhimu katika kazi yangu au maisha yangu? Je, nahitaji kweli kujua habari zote zisizo na maana na porojo kuhusu watu wengine? Maisha yangu yangebadilikaje ikiwa nisingetazama kipindi hiki cha televisheni, nisingesoma kitabu hiki au gazeti lile, au nisingetumia wakati mwingi sana nikisoma gazeti?
Labels:
Uchambuzi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment