Monday, February 5, 2007

Unajimu na SayansiKUNA UHUSIANO WOWOTE KATI YA SAYANSI NA UNAJIMU?
Na William Shao

MAMILIONI ya watu hutafuta ushauri kutokana na mambo ya nyota kila siku duniani. Je, unajimu ni sayansi—au angalau una uhusiano wowote na sayansi? Kuna uhusiano wowote wa kweli kati ya nyota na maisha ya binadamu ya kila siku? Ikiwa kuna uhusiano wowote wa kweli, binadamu huathirika jinsi gani kutokana na unajimu huo? Nyota hutimiza makusudi gani? Inawezekana kwa vyovyote kwa nyota kuongoza maisha ya watu?

Kwa kutazama matukio ya kidini na kijamii, unajimu unao historia ndefu tangu mwanzo mdogo kabisa wa historia ya mwanadamu.

Haishangazi kwamba watu wengi hupendezwa sana na wakati wao ujao na wakati ujao wa wenzao, hasa wanapofikiria kutukia kwa matukio yanayovuta sana fikra zao kama vile kuzuka na kumalizika kwa Vita Kuu I na II ya Dunia, kuzama meli ya Titanic Aprili 1912 na MV. Bukoba Mei 1996 na matetemeko ya ardhi pamoja na matatizo mengine ya kawaida lakini yanayosumbua maisha ya watu ya kila siku pamoja na mambo yanayohusiana na maisha hayo.

Kulingana na ripoti moja kutoka Chuo Kikuu cha Hamburg ambayo ilichapishwa katika gazeti ‘International Herald Tribune’, “…1992 ulikuwa ni mwaka wa ugomvi zaidi kuliko mwaka mwingine wowote katika karne ya 20 …ulikuwa na vita vingi mahali pengi duniani kuliko wakati mwingine wowote katika historia.”

Ingawa vita hivyo vinavyotajwa na gazeti hilo havikuwa na uzito ule ule uliokuwa wa Vita Kuu I na II ya dunia, kwa takwimu za kawaida tu, viligharimu idadi kubwa zaidi ya maisha ya watu na mali kwa kipindi cha mwaka mmoja tu ikilinganishwa na Vita Kuu II. Hakuna aliyetazamia hivyo.

Kwa hakika, ulikuwa ni mwaka wa peke yake ambao wanajimu hawakuweza kuuona kabla ya hapo. Kitabu ‘Britanicca Book of the Year’ (1993), katika utangulizi wake, kinasema: “Ni mwaka uliokuwa na zaidi ya vita 52 vya silaha kali katika nchi tofauti-tofauti…” na mamilioni ya watu walikufa kutokana na athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na vita hivyo.

Basi, kutokana na hali hiyo, wale wapenda amani wamekuwa wakijiuliza “ni wapi tunapoweza kupata uthabiti, amani na utulivu?” Hata wale wasio wapenda amani, lakini wanaojali sana wakati ujao wa maisha yao na wa maisha ya wenzao pia, wamevutwa sana na unajimu na kuutegemea kwa utabiri wake.

Wao wanaona kuwa kupata amani, uthabiti na utulivu wa maisha yao ni kujua wazi mambo yajayo. Hata kama si kujua mambo ya wakati ujao ulioko mbali sana, basi angalau ule wakati ujao ulio karibu zaidi, hata kama chache tu zijazo.

Kukosa uhakika juu ya matukio ya wakati ujao ndiko kulikosababisha kuvuma sana kwa aina mbalimbali za utabiri ambazo nyingine hudaiwa kuwa ni sayansi. Na kwa kuwa watu wengi wanapenda kujua mambo yao ya wakati ujao, basi watabiri (wa kweli au wa uongo) hupewa aina fulani ya heshima ya pekee. Katika mambo ya utabiri, labda unajimu ndiyo aina inayojulikana zaidi ya utabiri siku hizi.

Kitabu ‘The International Encyclopedia of Astronomy’, kinasema: “Katika China ya kale …ishara za angani na vilevile misiba ya asili zilifikiriwa kuwa zilionyesha matendo mazuri na hodari na matendo mabaya ya Maliki na serikali yake."

Kulingana na kitabu hicho, unajimu, ambao ni tofauti na elimu ya sayansi ya nyota (astronomy), ni “…kufanya uaguzi juu ya athari ambazo nyota na sayari nyingine hudhaniwa kuwa nazo juu ya maisha ya binadamu ambayo ni matukio yaliyo nje ya uwezo wake kwa kutegemea mahali nyota hizo zilipo na jinsi zilivyokaa kuhusiana na jua.” Leo, mamilioni ya watu wanashindwa kujizuia kusoma falaki (maarifa ya kubahatisha matukio kulingana na elim ya nyota) ili kupata madokezo ya wakati wao ujao.

Maeneo mengine ambamo wanajimu hudai kwamba huwa wanatabiri wakati ujao ni pamoja na matokeo magumu ya ndoa, matatizo ya afya, kuinuka na kuanguka kwa viongozi wa kisiasa, tarehe nzuri kabisa ya kufungua biashara mpya au kufunga biashara ya zamani pamoja na tarakimu za kutumia ili kushinda mchezo wa bahati nasibu au mchezo mwingine wowote.

Hata hivyo, kitabu ‘New Catholic Encyclopedia’ kinasema kwamba “unajimu ulitumiwa zamani na Papa Julius II [1503-13] ili kupanga siku ya kutawazwa kwake na ukatumia na Papa Paul III [1534-49] kuamua wakati halisi wa kuitisha Mkutano wa Kuzungumzia Masuala Mazito.”

Kitabu ‘The Thunder of Stars’ kimeandika kuhusu Bw. Alfred Hug ambaye ni mkurugenzi wa shirika moja la Uswisi ambalo mara nyingi hutumia unajimu kuwashauri watu wanaoweka akiba katika soko la hisa. Mnajimu huyo huwathibitishia watu mafanikio. Yeye Hug, alipoulizwa kuhusu utabiri anaofanya, alisema, “hayo yameandikwa katika nyota.”

Jambo la wazi ni kwamba wengi huhisi kwamba nyota huathiri maisha yao. Tofauti na inavyofikiriwa, mazoea ya kutazama nyota si mapya. Kitabu ‘The World Book Encyclopedia’ kinadokeza hivi: “Maelfu ya miaka iliyopita wakulima walizitazama nyota kujua wakati wa kupanda mimea yao. Wasafiri (nao) walijifunza namna ya kutumia nyota ili kuelewa upande wa kuelekea.”

Kulingana na mfululizo wa vitabu vya kujifunza Kiarabu, ‘Arabic by Radio’, baharia maarufu wa Oman, Ibn Majid, aliongoza chombo baharini kwa kuangalia nyota. Inasemekana kuwa huyu Majid aliwaongoza Wareno, akiwemo Vasco da Gama, kwa kutumia nyota (unajimu) kuja Afrika Mashariki kufanya ziara zao za upelelezi.

Hata hivyo, kwa kuzitazama zikiwa angani, idadi na ukubwa wa nyota ni mambo yanayoweza kushangaza sana. Inakadiriwa kuwa kuna makundi makubwa sana ya nyota (galaxy) kiasi cha bilioni 10 angani, kinasema kitabu ‘Encyclopedia Britanicca’.

Kitabu cha ‘International Encyclopedia of Astronomy’ kinasema: “…Hiyo ndiyo hesabu ya punje ndogo sana ambazo zingeweza kuingizwa katika jumba kubwa sana la wastani …Galaxy mojawapo ambayo mfumo wetu wa jua ni sehemu yake, inakadiriwa kuwa na angalau nyota nyingi kadiri hiyo.”

“…Nyota iliyo karibu zaidi na Dunia (ukiondoa jua), ambayo ni ya kikundi cha ‘Alpha Centauri’, iko umbali ambao mwanga unaoingia ndani ya jicho la binadamu unakuwa umetoka katika nyota hiyo kwa miaka 4.3 ukiwa bado unasafiri kwa mwendo wa kilomita 299,792 kwa sekunde moja (sawa na kilomita milioni 1,079.25 kwa saa moja).” Hata hivyo, kulingana na kitabu hicho, hiyo ni ile nyota iliyo karibu zaidi tu.

Nyota nyingine ziko mbali zaidi. Umbo kama nyota ambalo liko karibu zaidi na dunia ni mwezi, ambao, nao umetajwa mara kadhaa kuwa unahusiana na mawimbi ya bahari kwa namna fulani.

Mwezi huo huwa na athari ya wazi juu ya dunia yetu, “…hata uvutano wake husababisha tofauti ya zaidi ya mita 15 kati ya kujaa na kupwa kwa bahari mahali fulani-fulani,” chasema kitabu ‘International Encyclopedia of Astronomy’.

Kulingana na wanasayansi watatu wa Ufaransa, ingawa walionesha wasiwasi fulani ambao haukuwa dhahiri, wakati fulani waliliambia gazeti la ‘Nature’ (Feb. 18, 1993) hivi: “Uvutano wa mwezi sasa (kwa dunia) ndio unaoweka ‘mwinamo’ wa dunia katika ‘mlalo’ wa nyuzi (degree) 23,” na hivyo kuhakikisha kuna badiliko la kawaida la majira (ya mwaka).

Ripoti moja kutoka katika Kituo cha Utafiti wa Kisayansi cha Taifa cha Ufaransa (CNRS) sasa kinathibitisha kwamba mwezi una matokeo kama hayo juu ya uso wa ardhi ya dunia.

Kwa njia ya chombo cha uchunguzi kilichowekwa kwenye dimbwi la maji ya chumvi katika pango lililozibwa lililoko meta 1,000 (kilometa moja) chini ya ardhi, watafiti waliweza kugundua hali ya kuinuka na kuanguka kwa vitu vilivyokuwamo ndani ya pango hilo saa 12.

Mwendo huo, ulisababishwa na kupanuka na kusongamana kwa kuta za pango hilo. Kulingana na mwendo wa mwezi kuzunguka dunia nao huthibitissha kwamba kwelikweli mwezi ndio chanzo cha kile ambacho wataalamu katika kituo hicho cha CNRS hukiita "kupumua kwenye kushangaza chini ya ardhi."

Sasa, kufikia hapo, wale ambao walipata kuyajua hayo, walianza kujiuliza hivi: “Kwa kuwa mwezi una athari nyingi kiasi hicho juu ya sayari (dunia) yetu, ni namna gani basi yale mabilioni ya nyota?

Na kama kila nyota ina athari zake kwa dunia, kutakuwapo na mabilioni mangapi ya athari? Ndipo wengine wakaamua kwamba kwa kuwa hivyo ndivyo mambo yalivyo, kama mwezi huiathiri dunia, basi si tu kwamba nyota nazo huathiri dunia tu, lakini pia hata kile kinachohusiana na dunia hiyo.

Hata hivyo, mwandishi mmoja, Edwin Way Teale, katika kitabu chake ‘When Were You Born’, aliandika: “Nyota zisizo na uhai zinaweza kutuambia jambo fulani ikiwa tuko tayari kuzisikiliza, lakini si wakati tusipotaka kuzisikiliza …Nyota zinasema juu ya udhaifu wa binadamu katika muda fulani wa wakati.”

Mwanastronomia wa Ujerumani aliyeishi kati ya mwaka 1571-1630 alisema “unajimu ni kitu cha ziada tu (kisicho na ulazima wowote) na kishiriki cha astronomia.”

Mwanachuo mmoja wa Kiyahudi aliyeishi Enzi za Kati kati ya mwaka 1135-1204, Moses Maimonides, kwa mujibu wa kitabu ‘Guide for the Perplexed’, aliliona hilo kwa njai nyingine. Alisema: “Unajimu ni ugonjwa, si sayansi …Ni namna ya mti ambao chini ya kivuli chake namna zote za ushirikina na washirikina hushamiri.”

C. A. Ronan, ambaye ni mratibu wa mradi wa Historia ya Sayansi ya Asia Mashariki, Cambridge, Uingereza na mchangiaji wa habari katika kitabu ‘The International Encyclopedia of Astronomy’, alisema hivi:

“Sayansi ya kizamani ambayo hudai kwamba inaweza kukadiria utu na mwenendo wa mtu na kutabiri mwelekeo na matukio ya wakati ujao kutokana na jinsi maumbo ya sayari zilivyokaa mbinguni …labda katika karne ya sita—Wakaldayo walioishi kusini mwa Iraq hufikiriwa kuwa ndio walioanzisha falaki (maarifa ya kubahatisha matukio kulingana na elimu ya nyota). Hiyo ilihusiana na athari zilizosababishwa wakati wa kuzaliwa na nyota zilizokaa mahali pamoja, na pia Jua, Mwezi na Sayari tano.

“…Taratibu za unajimu na ule utaratibu wa kufasiri wa falaki hutegemea mawazo ambayo wanaastronomia na wengi wa wanasayansi wengine huyaona kuwa ni ya watu binafsi na yasiyokubalika.”

Katika kitabu hicho, Ronan aliyetajwa hapo juu anaeleza kwamba ingawa akili za watu wa nchi za Magharibi huchukulia kwamba ile sayari nyekundu inahusiana na vita na hali ya kutaka ugomvi, kwa Wachina, wekundu ni rangi ya bahati, na hutiliwa maanani kuwa ni ishara ya wema.”

Tofauti na hivyo, hadithi za Magharibi huihusisha Zuhura weupe pamoja na uzuri au bahati. Kwa Wachina, kulingana na kitabu ‘The International Encyclopedia of Astronomy’, rangi nyeupe huchukuliwa kuwa ni rangi ya kifo, misiba na maangamizi” na hivyo wao huitaja Zuhura kuwa ni “ile sayari ya ugizagiza na vita.”

Ronan anaendelea kusema kwamba “ingawa unajimu una asili ya sayansi ya kizamani, katika nyakati za mapema ulishiriki sehemu iliyokuwa na mafanikio sana katika kuendeleza astronomia na kuandaa fedha za kuutekeleza.”

Kitabu ‘The World Book Encyclopedia’ kinasema washindi 19 wa Tuzo la Nobel, pamoja na wanasayansi wengine, katika mwaka 1975 walitoa tangazo rasmi lililokuwa na kichwa cha habari ‘Kukanusha Unajimu—Taarifa ya Wanasayansi Mashuhuri 192’. Taaarifa hiyo lilitangaza hivi: “Katika nyakati za kale watu hawakuwa na wazo lolote juu ya umbali mkubwa sana uliopo kutoka duniani hadi kwenye zile sayari na nyota.

“…Kwa kuwa sasa umbali huo unaweza kuhesabiwa na tayari umeshahesabiwa na unaendelea kuwa rahisi zaidi kuhesabiwa, tunaweza kuona jinsi zilivyo ndogo sana zile nguvu za uvutano na matokeo mengine yanayosababishwa na hizo sayari za mbali na nyota zilizo mbali hata zaidi.

“…Ni kosa kuwazia kwamba athari za nyota na sayari wakati wa kuzaliwa zinaweza kwa njia yoyote na kwa vyovyote kuamua mapema, kubashiri na hata kujua nyakati zetu zijazo zitakavyokuwa.”

Mwanzoni mwa mwaka 1993, Shirika la Utafiti wa Kisayansi wa Mambo Yasiyojulikana na Sayansi nchini Ujerumani lilikusanya utabiri 70 uliofanywa na wanajimu kisha likakadiria matokeo mwishoni mwa mwaka.

“Walisema uongo mtupu,” likaripoti jarida ‘New Scientist’, likimkariri msemaji mmoja wa shirika hilo. “Wanajimu wengi hawaamini hata utabiri wao wenyewe.”

Wanasayansi wanaonyesha kwamba kama kweli nyota zilizo katika mbingu zinakuwa na matokeo yoyote juu ya watu mmoja mmoja, matokeo hayo ni kidogo sana. Kwa hakika, wazo lenyewe ambalo lilitegemewa ili kuanzisha unajimu, la kwamba dunia ndiyo mahali pa katikati pa ulimwengu mzima, na kwamba jua na sayari zinazunguka-zunguka dunia, “limethibitishwa na sayansi kuwa ni la uongo,” kikasema kitabu cha ‘The Encarta Encyclopedia Delux Edition’.

Ingawa kuna mashaka juu ya kama kutabiri mambo ya kutazama nyota kunasaidia, mtu anaposoma safu zinazohusu kutazama nyota, ana hatari ya kupoteza uwezo wa kufanya maamuzi ya maana, au kama vile mtaalam wa kuchunguza nyota, Roger Culver alivyoeleza: “Hatari ni kwamba unaweza kujiondolea lawama na kusema nyota ndizo zilizokufanya utende vile.”

Ni kweli kwamba huenda mtu akasoma safu kama hizo kwa makusudi ya kujifurahisha tu, lakini, kwa mfano, tukio fulani maishani mwake linalingana bila kutazamiwa na jambo alilosoma katika maelezo ya nyota hizo, anaweza kushawishika bila kutambua na kumfanya aamini kwamba kuna ukweli fulani katika utabiri wa nyota hizo, na hatimaye atashawishiwa zaidi kujiingiza katika unajimu.

Ikiwa ndivyo, jambo fulani lililo zito zaidi linaweza kutukia. Jambo lililoanza kama hamu tu ya kutaka kujua jinsi mambo yalivyo lingeweza kugeuka liwe mazoea yanayokuwa na nguvu zaidi ya mambo mengine ya maana zaidi.

Katika jarida ‘Nature/Science Annual’, Dk. Alan Rosenburg, daktari wa magonjwa ya akili, aliandika: “Watu wamevurugika mawazo. Wanataka msaada wa kufanya maamuzi yanayohusu pesa, uhusiano wao na watu wengine na kazi ya kuajiriwa.

“Dini haitimizi haja zao hizo kama ilivyokuwa zamani, na udaktari wa magonjwa ya akili unapungukiwa katika mambo fulani. Kwa hiyo …wakiwa katika jaribio la kutaka kushikamana na jambo linaloonekana kuwa na uwezekano wa kisayansi, wao wanazidi kugeukiwa wanajimu kwa wingi kutatua matatizo yao…”

Katika hatua moja, Halmashauri ya Uchunguzi wa Kisayansi ya Madai ya Maajabu ya Visivyoonekana nchini Marekani, Novemba 16, 1984 ilidokeza kwamba “matabiri yanayofuata ya unajimu yapaswa kusomwa kwa faida za kujifurahisha tu. Matabiri hayo hayana msingi wa kutegemeka wenye ukweli wa kisayansi.”

No comments: