Monday, February 5, 2007

Mwanadamu Aliyepuuzwa


MWANADAMU ALIYEPUUZWA NA MAPINDUZI YA ZANZIBARNa William Shao

USIKU wa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 11-12, 1964, kulitokea mapinduzi yaliuouondoa madarakani utawala wa Kisultani katika visiwa vya Zanzibar.

Ingawa huo ni ukweli wa kihistoria, ile sehemu ya historia inayozungumzia Mapinduzi ya Zanzibar imembagua mwanadamu mmoja tu muhimu sana ambaye ndiye hasa aliyefanya mapinduzi hayo—‘Field Marshal’ John Okello.

Marejeo mengi yanaonyesha kuwa aliyefanya Mapinduzi ya Zanzibar ni raia wa Uganda aliyeitwa John Okello aliyekuwa Unguja, na wala si Abeid Karume, ingawa Karume hatimaye alitokea kuwa Rais wa Zanzibar mara baada ya mapinduzi.

Inaelekea kuna mambo yaliyofichwa katika historia hiyo. Swali ni kwanini hata yafichwe? Hata kama Okello hakufanya mapinduzi hayo, kwanini hatajwi na wanahistoria wengi wa Tanzania kuwa alihusika, au angalau tu kushiriki, katika mapinduzi hayo? Historia ya Zanzibar inasababisha maswali mengi kuliko majibu.

Wanasiasa wengi—hasa wale Zanzibar—wanasema John Okello siye aliyefanya Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini baadhi yao wanashindwa kukanusha kuwa Okello alikuwa Zanzibar wakati wa Mapinduzi hayo yakifanyika.

Miongoni mwa waliokana ukweli huo ni Hayati Khamis Daruwesh. Hata hivyo na yeye alikiri kuwa John Okello alikuwa na “…mvuto" huko Zanzibar (rejea RAI, Aprili 14—20, 2005).

Hata hivyo, katika picha ya pamoja ambayo ‘wanamapinduzi’ walipiga Jumatatu ya Januari 12, 1964, Okello anaonekana amekaa mkao wa kiongozi mbele ya wengine, tena akiwa amezungukwa na wanachama wa Baraza la Mapinduzi walioshiriki katika mapinduzi hayo.

Miongoni mwa wote hao ni yeye peke yake anaonekana tofauti kabisa na wengine wote akiwa amevalia nguo ama za kijeshi au za polisi. Wengine wote wamevalia nguo za kawaida tu.

Wengine katika picha hiyo ni pamoja na Yusuf Himid, Said Abdallah Natepe, Ramadhan Haji, Said Buvai, Said wa Shoto, Muhammed Abdallah, Pili Hamis, Hamis Darwesh, Khamis Hemed, Hafiz Suleiman na Hamid Ameir.

Ni watu watatu tu walikuwa wamepewa viti na kukaa mbele ya wengine. Wengine wote, akiwemo Daruwesh mwenyewe, walisimama nyuma ya Okello, na katikati ya wote hao ndipo alipokaa “Jemadari Mkuu” John Okello.

Ingawa wanajitahidi kuficha kuhusika kwa Okello katika mapinduzi ya Zanzibar, historia inasimama kama shahidi. Gazeti Tanganyika Standard (Jan. 13, 1964), katika ukurasa wake wa mbele liliandika hivi: “Wapigania uhuru waliokuwa na silaha wamekitwaa kisiwa cha Zanzibar.

“Wamekamata majengo yote muhimu ya serikali kwa muda usiozidi saa 24 …usiku kiongozi wa mapinduzi alitangaza muundo wa serikali mpya ya ‘Jamhuri ya Zanzibar na Pemba’ Sheikh Karume akiwa kama Rais na Bw. Kassim Hanga kama Waziri Mkuu…”

Watu hawa waliopewa uongozi wa nchi—Karume, Hanga na baadhi ya wengine—hawakuwa Unguja wakati Okello akitaja vyeo vyao. Walikuwa wamekimbilia Dar es Salaam kujificha, wakihofia kuwa ikiwa mapinduzi yangeshindwa wangekamatwa na kutiwa kizuizini.

Gazeti hilo liliandika kuwa mtangazaji huyo ni “kiongozi wa mapinduzi” na kwamba ndiye “alitangaza muundo wa serikali mpya ya ‘Jamhuri ya Zanzibar na Pemba’.”

Kwa namna Okello alivyopanga mapinduzi hayo na kuyafanikisha, walioyashuhudia na walioyasikia yalivyofanyika hawakuamini kama kweli mtu huyo alikuwa wa kawaida. Maswali mengi kumhusu Okello yalianza kuulizwa. Wengine walidhani kuwa aliwahi kupata mafunzo ya kijeshi katika Uchina au Cuba.

Maswali na uvumi wa aina hiyo ulisambaa sana kila kona kiasi cha kulisukuma gazeti Tanganyika Standard kwenda kumuuliza maswali hayo. Baadaye gazeti hilo liliripoti hivi: “Field Marshal John Okello leo amesema yeye ni mtu thabiti wa mapinduzi ya Zanzibar na ni yeye aliyemteua Sheikh Abeid Karume kuwa Rais. Kiongozi huyo wa maasi mwenye umri wa miaka 27, …amesema anachoitakia Zanzibar ni ‘demokrasia na uhuru’.

“Field Marshal amefanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari katika ofisi za kurushia matangazo ya redio ambazo zilikuwa zimechukuliwa kama makao makuu mapya ya Serikali. Lundo la bastola aina ya .22 lilikuwa mbele ya meza yake. Walinzi waliokuwa na bastola na bunduki mbalimbali walisimama kumzunguka.

“Kiongozi huyu wa waasi aliye mfupi amesema hakuwahi kuwa na mafunzo yoyote yanayohusiana na uasi nje ya nchi na kukanusha taarifa kuwa aliwahi kwenda Cuba au Peking (China). Alisema alipanga kuiangusha Serikali ya Zanzibar akisaidiana na Kamati Kuu yake ya watu waliopewa siku 14 tu ya mafunzo msituni…”

Hiyo ni sehemu tu ya taarifa iliyotolewa na chombo cha Serikali ya Tanganyika—Tanganyika Standard. Taarifa hiyo haimtaji Karume kama mwanamapinduzi, bali John Okello.

Tanganyika Standard haikutoa kielelezo chochote kinachodokeza kwamba Abeid Karume au mtu mwingie yeyote, isipokuwa Okello, ndiye aliyefanya mapinduzi ya Zanzibar. Kwamba Karume ndiye kiongozi wa Mapinduzi ni historia iliyogeuzwa baada ya John Okello kufanyiwa njama za kumwondosha Zanzibar.

Ingawa historia inaonesha kuwa John Okello alihusika sana na Mapinduzi ya Zanzibar kuliko Mzanzibari au Mtanzania yeyote—awe Sheikh Karume, Thabit Kombo, Kassim Hanga, Abdulrahman Babu au Mwalimu Julius Nyerere—hapewi sifa hiyo, angalau hata kutajwa tu kwamba alikuwepo Zanzibar wakati mapinduzi hayo yanafanyika, hata kama hakushiriki katika kufanya mapinduzi.

Wala hatamkwi kwamba yeye ndiye aliyetangaza ushindi. Hakuna kumbukumbu za kihistoria zilizoachwa kwa ajili ya vizazi vya baada ya mwaka 1964 zinazotosha kuvihamasisha kuvutiwa na mambo ya Okello. Habari zake zinaepukwa hata wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi Zanzibar inayojulikana kama ‘Januari 12’.

Madai kwamba “Mapinduzi ya Zanzibar ni mapinduzi ya Okello” yalichapishwa pia na gazeti la chama cha TANU, The Nationalist & Freedom (Jan. 12, 1965), mwaka mmoja barabara baada ya kufanyika kwa mapinduzi hayo.

Magazeti mengi ya ndani na nje ya Tanganyika, hususan The Standard la Tanganyika, yaliyochapishwa katika siku zile ambazo mapinduzi yalifanyika, yaliandika sana kuhusu habari za Okello na jinsi alivyofanya mapinduzi hayo.

Pamoja na hayo, nadharia nyingine—ambazo hazina uhakika wa kihistoria—zinadai kwamba kiongozi na mwanamapinduzi wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar aliuawa mwanzoni kabisa mwa mapinduzi hayo na hivyo Okello akatwaa usukani wa kuendesha Mapinduzi.

Ingawa nadharia hiyo inakataa kwamba Okello hakuwa kiongozi wa mapinduzi hayo tangu pale mwanzoni, angalau inakubali kuwa alishiriki mapinduzi hayo na hata akawa kiongozi wake baada ya “kiongozi na mwanamapinduzi wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar” kuuawa mwanzoni kabisa mwa mapinduzi hayo.

Nadharia hiyo inajaribu kukataa kwamba Okello hakuwa kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar, lakini inashindwa kumkana. Ikiwa kiongozi na mwanamapinduzi wa kweli aliuawa mwanzoni kabisa mwa mapambano, basi hakuwa mpambanaji mzuri.

Lakini yule aliyechukua usukani na kuendeleza mapambano hadi kufanikisha lengo lake, huyo ndiye anayepaswa kuwa mpambanaji na mwanamapinduzi wa kweli.

Ni nani mshindi wa kweli wa mapinduzi kati ya kiongozi aliyeanzisha mapambano na kisha akauawa mwanzoni mwa mapambano hayo na yule aliyepokea usukani akapambana hadi mwisho na kupata ushindi?

Hata kama itakubalika kwamba Okello hakuwa kiongozi wa mapinduzi pale mwanzoni, inaeleweka kuwa anayepata ushindi ndiye mshindi. Haijulikani ni nani aliyetengeneza nadharia hiyo ya udanganyifu na, la maana zaidi, haijulikani kwanini nadharia hiyo ikatengenezwa na ni kwa maslahi ya nani.

Magazeti ya The Standard na The Nationalist & Freedom lililozinduliwa na Mwalimu Julius Nyerere Alhamisi ya Aprili 16, 1964, yaliripoti sana habari za Okello na jinsi alivyoshiriki kikamilifu katika Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika habari zote kuhusu jambo hilo katika kipindi cha mwanzo cha 1964, magazeti hayo hayakueleza kama kulikuwa na kiongozi wa mapinduzi aliyeuawa na, kama matokeo ya kuuawa huko, Okello akachukua usukani.

Lakini iliwashangaza wasomaji wengi madai hayo yalipotolewa mwaka mmoja baadaye kwamba Okello hakuwa kiongozi, bali alichukua uongozi baada ya kiongozi wa kweli wa mapinduzi hayo kuuawa katika mapigano.

Mwandishi Keith Kyle wa Uingereza aliyeandika makala mbili tofauti kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar katika matoleo mawili tofauti ya gazeti The Spectator, alikuwa sahihi kwa sababu alichoandika kinafanana na maelezo mengi yaliyoonekana katika machapisho mengine ya ndani na nje katika kipindi cha Januari na Februari 1964.

Zaidi ya hilo, mwandishi Kyle alikuwepo Zanzibar wakati wa matukio ya Januari 11-12, 1964, akithibitisha kushiriki kwa Okello katika Mapinduzi ya Zanzibar. Imani ya Kyle inadokeza kuwa matangazo ya redio yaliyotolewa na Okello mara tu baada ya Mapinduzi na habari nyingine kumhusu mwanamapinduzi huyo zinathibitisha kuwa alishiriki moja kwa moja katika Mapinduzi hayo.

Baada ya kukidhibiti kisiwa cha Unguja, John Okello alimwalika Abeid Karume kurudi Zanzibar kuchukua nafasi ya Urais,” kinasema Wikipedia Encyclopedia. Kinaongeza kusema hivi: “(Abeid) Karume hakuwa Zanzibar usiku ule Mapinduzi yalipofanyika.”

Michael F. Lofchie, katika kitabu chake, Was Okello's Revolution a Conspiracy? © 1967 (uk. 36-42), aliandika hivi: “…Okello alifanya Mapinduzi ya Zanzibar…” Lakini anaongeza kuandika: “Njama za kumwondoa Zanzibar ni za kuficha ukweli unaochukiza...”

Okello ameelezwa sana katika kitabu Revolution in Zanzibar (1967) kilichochapishwa mjini Nairobi. Alitajwa sana katika gazeti The Standard la Tanganyika/Tanzania kwamba yeye ndiye aliyefanya mapinduzi katika Zanzibar.

Hata waliokuwa viongozi wa serikali ya Sultani wanakiri ukweli kwamba Okello ndiye aliyefanya mapinduzi na wala si Karume. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Sultani, Ali Muhsin Ali Barwan, ambaye alikuwa Zanzibar wakati serikali yake ikipinduliwa, Jumanne ya Oktoba 21, 1997, akiwa Dubai katika Falme za Kiarabu, aliukiri ukweli huo.

Alisema: “…John Okello, askari mamluki, aliongoza mauaji ya kinyama, …watu 12,000 walichinjwa. Lakini msingi wenyewe uliwekwa mwaka 1957 wakati vyama vya Shirazi Association na African Association vilipoungana na kuunda Muungano wa Afro-Shirazi chini ya ushawishi na uongozi wa Julius Nyerere.” (kitabu Conflicts and Harmony in Zanzibar © 1997)

Kwa wale wasiotaka kupotosha mambo wanakiri kwamba Abeid Karume hakufanya mapinduzi kama inavyodaiwa, bali ni Okello akisaidiwa na baadhi ya wale aliowaita ‘wapigania uhuru.’

Kitabu Mwalimu: The Influence of Nyerere © 1995 (uk. 172), kinasema: “Uhuru wa Zanzibar ulipatikana (Alhamisi ya) Desemba 10, 1963, sultan akiwa Mkuu wa Nchi (Zanzibar) na kupewa mamlaka ya kumteua mrithi wake …Ndani ya majuma matano tu Serikali hiyo na mtawala wake walipinduliwa na ‘masiha mjinga’ ambaye ni kiongozi wa wanaharakati, John Okello. Baada ya kipindi kifupi cha vurumai na mauaji, Okello alisimika Baraza la Mapinduzi chini ya uongozi wa (Sheikh Abeid) Karume.”

Hayo yaliandikwa na Profesa Haroub Othman ambaye ni mtaalam wa mambo ya siasa za ulimwengu na Mzanzibari anayejua mambo mengi kuhusu historia ya visiwa hivyo. Lakini kinachotatiza ni kwanini Okello hatajwi kabisa wakati suala la Mapinduzi ya Zanzibar linapozungumzwa?

Hata hivyo, jarida la African Studies Review, katika pitio lake la vitabu la Septemba 2003 ambalo Jennifer Betowt alikifanyia kitabu Revolution in Zanzibar: An American's Cold War Tale, alidai kuwa habari nyingi kuhusu Okello hazina uhakika.

Gazeti lichapishwalo mjini London, Uingereza, The Spectator (Feb. 7, 1964) chini ya makala Gideon’s Voice, pamoja na lile la (Feb. 14, 1964), chini ya makala How it Happened, linaelezea kuhusika moja kwa moja kwa Okello katika Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika magazeti hayo Okello anafafanuliwa kuwa mhusika mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar, na kwamba yeye ndiye aliyewavuta wengine wote waliokuja kushirikiana naye katika kufanya mapinduzi hayo.

Majira ya saa moja asubuhi ya Jumapili ya Januari 12, Okello alianza kutoa moja ya matangazo yanayojulikana Zanzibar kuwa ni mabaya zaidi. Hapa ndipo Okello alipotamka kwa mara ya kwanza kabisa kuwa yeye ni "Field Marshal wa Wapigania Uhuru." Awali hakutaja jina lake, lakini saa chache baadaye alitamka jina lake likitanguliwa na cheo alichojipachika — Field Marshal John Okello. (Gazeti Tanganyika Standard, Jan. 13, 1964)

Akitumia jina lake kupitia matangazo ya redio, mchana wa siku hiyo Okello, akitumia redio, alisema: “Amkeni ninyi mnaojiita wafalme, hakuna tena serikali ya kifalme katika kisiwa hiki. Sasa hii ni serikali ya wapigania uhuru. Amkeni nyie watu weusi, na kila mmoja wenu abebe bunduki na zana za vita na kuanza kupigana.”

Baada ya kuridhika na mipango yake, mchana wa Januari 12, 1964, Okello alitangaza jamhuri—Jamhuri ya Zanzibar—yeye mwenyewe akajitangaza kama “Waziri wa Ulinzi na Utangazaji na Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi.”

Sheikh Abeid Karume alitangazwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Kassim Hanga akatangazwa kuwa Makamu wa Rais, na Abdulrahman Babu pamoja na viongozi wengine wa ASP wakawa mawaziri katika serikali mpya.

Aboud Jumbe alitengewa nafasi ya uongozi. Alipewa Uwaziri wa Afya na Huduma za Jamii. Othman Sharif aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu; Hasnu Makame, Waziri wa Kilimo; Idris Abdul Wakil, Waziri wa Biashara na Abdulrahman Babu, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Katika matangazo mengine ya redio, Okello alimteua tena Hasnu Makame kuwa Waziri wa Fedha na Saleh Sadalla kuwa Waziri wa Kilimo.

Siku iliyofuatia, Jumatatu ya Januari 13, Okello, akiwa ameshika hatamu za serikali ya Zanzibar na kuwateua mawaziri wake, (rejea magazeti ya Tanganyika Standard, Jan. 14, 1964) alikuwa na kukurukakara nyingi.

Alionekana akipita hapa na pale kama mtu aliyekuwa akitafuta jambo fulani asilipate. Mipango yake ilikuwa haijamalizika, badala yake ilizidi kuwa mingi. Aliwateua maofisa wengine zaidi wa serikali yake, wengi wao wakiwa ni wahamiaji wa kutoka bara waliohamia Unguja siku za karibuni.

Baada ya kupanga safu ya serikali yake huku watu wengi kisiwani Unguja na duniani kwa ujumla wakiwa hawajawa na uhakika wa kitakachotokea baadaye, sauti ya Okello ilisikika redioni ikisema: “...Serikali sasa inaendeshwa nasi—Jeshi. Ni juu ya kila raia, mweusi, maji ya kunde au mweupe, kutii amri. Ukiwa mkaidi au kudharau amri, nitachukua hatua kali mara 88 zaidi ya hatua nilizochukua sasa hivi (kuangusha serikali ya Sultan).

Vitisho na uwezo wake wa kuvitekeleza viliwashtua sana raia wengi. Kesho yake, Jumanne, Januari 14, 1964, alitoa tangazo lingine lililokuwa na maneno makali hata zaidi. Alisema:

"Huyu ni Field Marshall (Jemadari Mkuu) wa Zanzibar na Pemba …Ninafikiria kwenda (kijiji cha) Mtendeni kukiangamiza ikiwa watu wa huko hawataki kutii amri. Baada ya dakika 40 nitakuja kuwamaliza nyiye wote, hasa Wacomoro.”

Huyu ni mwanadamu ambaye waliosikia habari zake na yale aliyoyafanya huko Zanzibar wanashangaa ni kwanini hatamkwi kabisa katika historia ya Zanzibar. Lakini kwa waliosoma kazi za Michael Lofchie, hasa kitabu chake, Was Okello's Revolution a Conspiracy? hawatashangaa kusoma kwamba “Njama za kumwondoa Zanzibar ni za kuficha ukweli unaochukiza...”

********************************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754 989 837. E-mail: shao2020@yahoo.co.uk., Blog: willyshao.blogspot.com.
********************************************************

No comments: