Monday, February 5, 2007
UKWELI KUHUSU SEPTEMBA 11
UKWELI KUHUSU SEPTEMBA 11 NI NANI AUJUAE?
William Shao
KUNA mambo mengi yanayotendeka duniani, yakiwa na makusudi maalumu kwa malengo maalumu ili kutimiza shabaha maalum. Lakini kiasi tunachokijua kuhusu mambo hayo ni kidogo mno kama vile chembe ya mchanga mbele ya fukwe kubwa za bahari za dunia.
Richard Wurman katika kitabu chake, Information Anxiety anaandika hivi: “Kwa muda mrefu watu hawakutambua kiasi cha mambo ambayo hawakujua. Hawakujua kuwa kulikuwa na mambo mengi ambayo hawakujua. Lakini sasa watu wanajua kwamba kuna mambo ambayo hawajui, na hilo ndilo linalowafanya wahangaike.”
Hata hivyo, wengi wetu tunafikiri kuwa sasa tunajua, kumbe tunachojua ni kutojua kuwa hatujui. Hata kujua peke yake hakutoshi. Kinachotakiwa ni kujua kati ya uongo na ukweli, na kati ya ukweli na yale tunayoambiwa tuyaamini kuwa ni ya kweli.
Mwandishi mwingine, David Shenk, akaenda mbali zaidi. Katika kitabu chake, Data Smog—Surviving the Information Glut, anasema: “Habari zikizidi mno huchafua data na kuzitia ukungu. Ukungu wa data huzuia; hautoi nafasi ya dakika chache za ukimya na kutafakari, na unazuia kufikiria kwa makini kunakohitajiwa sana …unatusababishia mkazo wa akili.”
Ni kweli kwamba habari nyingi kupita kiasi, kama ilivyo kwa mambo yote yanayopita kiasi, husumbua sana. Lakini kwa kutazama mambo kwa uangalifu, ni bora zaidi kuwa na habari nyingi kuliko kutokuwa na habari zozote, au ni bora zaidi kuwa na habari nyingi kuliko kutokuwa na habari za kutosha.
Lakini inakuwa mbaya zaidi tunapokuwa na habari tunazofikiri kwamba zinatosha, kumbe ni habari za uongo au kumbe tumedanganywa. Tatizo ni kwamba sisi wanadamu tumetumbukia katika wingi wa habari lakini tuna njaa ya kujua. Tuna habari nyingi lakini hatujui mambo mengi.
Habari peke yake hazielimishi. Hatuwezi kufafanua ni ipi habari zilizokosewa—kwa bahati mbaya au kwa makusudi, au iliyo kinyume, au propaganda katika mazingira yanayotawala habari.
Ni mara ngapi habari za magazeti zimekanushwa na kisha magazeti hayo kuomba radhi? Hilo linamaanisha habari hizo hazikuwa sahihi zilipoandikwa kwa mara ya kwanza.
Tukiingia moja kwa moja katika mada yetu ya leo, tutazame mazingira ya kile kilichoitwa ‘September 11th’. Habari zinazolizunguka tukio hilo ni za kutatanisha kuliko dunia ilivyo tayari kukiri.
Nani aliyefanya mashambulizi dhidi ya Marekani Septemba 11, 2001? Na la maana zaidi, mashambulizi hayo yalikuwa na lengo gani? Kwanini yalifanyika Septemba 11 badala ya tarehe nyingine yoyote? Kuhusiana na tukio hilo kuna maswali mengi kuliko majibu. Na maswali mengi ya msingi hayajawahi kujibiwa.
Kuna kile kilichoitwa Nadharia ya Kigwena (Conspiracy Theory). Nadharia hii hujaribu kueleza chanzo au asili ya tukio (hususan la kisiasa, kijamii au la kihistoria) kana kwamba limefanywa kwa siri, hila na njama na watu au kikundi fulani cha watu kutimiza malengo fulani.
Ingawa inasemekana kuwa watu huamini kile wanachoona, saikolojia halisi haikubaliani na hekima hiyo. Badala yake saikolojia hiyo inasema kwamba watu “huona kile wanachoamini” na wala si kwamba “huamini kile wanachoona”. Tofauti hiyo ni ndogo, lakini ni ya maana sana.
Tukio la Septemba 11, 2001 limejengewa nadharia za aina hiyo. Wapo wanaodai kuwa Rais wa Marekani, George W. Bush na watu wake ndio waliofanya mashambulizi hayo kuwapumbaza watu ili atimize shabaha zake zilizoanzishwa na familia yake miongo mingi iliyopita.
Lakini wengi wanaamini aliyefanya ni Osama Bin Laden na kundi lake. Wengine wanaamini kuwa ni Waisrael walifanya shambulizi hilo.
Inawezekana kuwa nadharia zote hizo hazisemi kweli. Na ikakubalika Osama bin Laden na kundi lake la kigaidi ndiye aliyefanya tendo hilo. Bila kuchambua nadharia hizo, tutazame yale mambo ya kihistoria na ya kimantiki tunayoweza kukubaliana.
Namba 11 ni ishara inayotumiwa sana kwa malengo fulani. Kisha kuna 911, ambayo nayo ina namba 11. Hii, kwa wale wanaofuata mambo ya unajimu, wanaweza kudhani kuwa ninachoandika hapa ni falaki. Huu sio unajimu, ni uhakika.
Ukitazama majengo yaliyoangushwa Marekani jinsi yalivyokuwa yamesimama, utaona namba 11 kwa sababu ni minara miwili iliyokaa sambamba, na ndege ya kwanza kugonga majengo hayo Septemba 11 ni ‘Flight 11’.
Kutokea mara kwa mara kwa hii namba 11 katika tukio la Septemba 11 ni jambo la ajabu kwa wengi, lakini si kwa wale wanaojua maana ya namba hiyo na ishara zake na ni kwanini wao huitumia.
Hadi Jumanne ya Septemba 11, 2001 ilikuwa imepita miaka 11 barabara tangu George Bush (baba wa Rais wa sasa) kuhutubia Bunge la Marekani Jumanne ya Septemba 11, 1990 akizungumzia Vita ya Ghuba na kutamka shabaha ya tano ya Marekani aliyoitaja kama “New World Order” ambayo wachambuzi wa mambo huitafsiri kuwa ni mpango wa Marekani wa kuitawala dunia.
Makao Makuu ya jeshi la Marekani (Pentagon), ndiyo yaliyozungukwa zaidi na ‘muujiza’ huu wa namba 11, hasa Septemba 11, au tuseme 911. Ndege inayodaiwa kugonga Pentagon ni ‘Flight 77’. Ukiigawa 77 kwa 7 utapata 11, na katika hiyo 7-1-1=5. Namba tano ndiyo namba halisi ya The Pentagon. Tafsiri ya pentagon ni kitu chenye pembe 5.
Hilo huenda halitoshi. Lakini kuna ukweli mwingine wa kihistoria. Ujenzi wa jengo la The Pentagon ulianza rasmi Alhamisi ya Septemba 11, 1941, na miaka 60 barabara baada ya ujenzi wake kuanza jengo hilo likashambuliwa.
Jengo la Pentagon lilianza kujengwa kutokana na maombi ya Brigedia Jenerali Brehon B. Sommervell alilolitoa Julai 1941. Hatimaye jiwe la msingi likawekwa Septemba 11, 1941.
Jumanne ya Mei 22, 1962, (22 inahusiana moja kwa moja na namba 11) ndege ya shirika la ndege la Continental, ‘Flight 11’, 707, ilikuwa ndege ya kwanza kuhujumiwa wakati bomu lilipolipuka ndani yake ikiwa angani na kuua watu wote 45 waliokuwamo ndani yake. Tazama hizo namba, 11, 22, na 707, au 77 zilivyo.
Namba 11, 22, na 77 zitajirudia katika mambo mengi. John Kennedy, aliyekuwa Rais wa Marekani kupitia chama cha Democrat, aliuawa kwa kupigwa risasi Ijumaa ya Novemba 22, 1963. Ukipanga tarehe hizo katika tarakimu zitasomeka hivi: 22.11.1963.
Septemba 11, 1970, na siku mbili zinazoizunguka siku hiyo, ndege nne zilizokuwa zikielekea Marekani zilitekwa nyara katika anga la Ulaya zikalipuliwa katika jangwa la Jordan. Ndege ya mwisho katika hizo ilitekwa Septemba 9.
Septemba 11, 1972, Rais Richard Nixon wa Marekani aliunda jopo la watu kuandaa la kutengeneza mikakati ya kulilinda taifa la Marekani dhidi ya matendo ya kigaidi. Mmoja wa waliokuwa katika jopo hilo ni Henry Kissinger ambaye baadaye akaja kuwa kiongozi wa Tume ya kuchunguza tukio la Septemba 11, 2001.
Jopo hilo liliundwa na Rais Nixon mara baada ya makomando wa Palestina kuwachinja Waisrael 11 waliokuwa wakishiriki Michezo ya Olimpiki mjini Munich, Ujerumani.
Septemba 11, 1973, majeshi ya Chile, yakiongozwa na Jenerali Augusto Pinochet, ambaye inadaiwa alikuwa akisaidiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani, CIA, aliipindua serikali ya Rais Salvador Allende.
Septemba 11, 1997, Kampuni ya ulinzi ya Stratesec ambako mtoto wa ‘Baba’ George Bush, Marvin, ni mwanachama wa bodi, ilitangazwa rasmi. Kampuni hiyo yenye mkataba wa ulinzi na Uwanja wa Ndege wa Dulles, United Airlines na Los Alamos National Laboratories, ilikuwa na mkataba wa ulinzi kama huo na majengo ya WTC yaliyopigwa na ndege Septemba 11, 2001.
Kampuni hiyo ilipoanzishwa ilijulikana kwa jina la Securacom. Marvin Bush aliendelea kuchaguliwa kuwa mjumbe katika bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo kila mwaka hadi Juni 2000.
Septemba 11, 1998, mwanasheria Kenneth Starr alituma taarifa iliyojulikana kama 'The Starr Report' kwenda Bunge la Marekani ikimshutumu Rais Bill Clinton kwa makosa 11 yaliyokuwa na uzito wa kutosha kumwondosha madarakani.
Mwaka 1967 nchini Marekani ilipendekezwa kubuniwa namba moja ambayo ingekuwa ya dharura kwa taifa lote la nchi hiyo. Kampuni ya Simu ya Marekani (AT&T), mwaka 1968, ilitangaza kuanzisha namba 911, au tisa-moja-moja au tisa-kumi-na-moja (nine-eleven).
Kuanzia wakati huo, Septemba 11 ilikuwa ikitazamwa kama siku ya dharura katika taifa hilo. Mambo hayo yalibadilika mara baada ya mashambulizi ya Septemba 11. Canada nayo, mwaka 1980, ilianza kutumia namba hiyo ya dharura, 911.
Mbali na namba 911, kuna nyingine kama 211 kwa ajili ya habari za utabiri wa hali ya hewa na 411 kwa ajili ya kupata habari nyinginezo. Zote hizo zina namba 11 mwishoni. Ili kupata namba ya dharura, Marekani iliamua kuongeza namba 9 na kupata 911.
Hayo yote ni mambo ya hakika. Lakini je, ni jambo la bahati mbaya kwamba namba 11 na 9 pamoja na zile nyingine kama 22, 33, 44, 55, 66 na 77 zinajirudia-rudia? Kama unadhani huu ni unajimu, au falaki, tafakari kwa makini zaidi.
Tarehe ya mashambulizi ya Marekani: 9/11 - 9 + 1 + 1 = 11. Septemba 11 ni siku ya 254 ya mwaka: 2 + 5 + 4 = 11. Baada ya Septemba 11 kuna siku 111 zilizobaki hadi kumalizika kwa mwaka. 119 ni namba ya mwito wa simu wa Iraq na Iran kama Tanzania ilivyo na 255. Na 1 + 1 + 9 = 11.
Majengo ya WTC, yakiwa yamesimama sambamba huonakana kama namba 11. Ndege ya kwanza kugonga jengo la kwanza ilikuwa ni ‘Flight 11’.
Lakini kuna mengi zaidi ya hayo. Jimbo la New York ni la 11 kuingizwa katika taifa la Marekani. Na ukisoma vyema herufi za neno ‘New York City’ utagundua kuwa ziko 11.
Neno ‘Afghanistan’, ambayo inahusiana moja kwa moja na Septemba 11, ina herufi 11. Neno ‘The Pentagon’ nalo lina herufi 11. Jina la ‘Ramzi Yousef’, anayedaiwa kuendesha mashambulizi ya WTC mwaka 1993, lina herufi 11. ‘Flight 11’, ikiwa na abiria 92 ndani yake, hesabu lake ni (92) 9 + 2 = 11. Ndege ‘Flight 77’, ikiwa na abiria 65 ndani yake, ukipanga tarakimu zake utapata 6 + 5 = 11.
Tutazame mahesabu mengine. Tarehe ya mashambulizi: 11/9; 11 - 9 = 2. September 11 = 1 + 1 = 2. Septemba 11 ni siku ya 254 ya mwaka: 2 + 5 + 4 = 11, na 11 ni sawa na 1 + 1 = 2. Majengo ya ‘World Trade Center’ ilikuwa na minara miwili (2) na iligongwa na ndege mbili (2).
Namba 11 imehusishwa na nguvu za miujiza au za siri tangu zamani za kale. Aina zote za utafiti wa namba, ikiwemo elimu ya namba, ‘Numerology’, zote zinatoa umuhimu fulani kwa namba 11 na zile zinazohusiana nayo kama 22, 33, 44, 55, 66, 77, 88, na 99.
Namba 11 hufikiriwa kuwa kuu zaidi ya zote. Vita Kuu ya Kwanza ilimalizika saa ya 11, siku ya 11 katika mwezi wa 11 wa mwaka 1918. Hadi leo, ingawa imeshaanza kusahaulika, waliopigana vita hiyo huenziwa Novemba 11.
Kwa baadhi ya Wamarekani wanaojua umuhimu wa namba 11 ulivyo kwao, hata kusherehekea mwaka wa 111 wa kuzaliwa kwa mtu wao huepuka sherehe hiyo. Namba 11 ni muhimu sana kwao.
Kuna mambo mengi yaliyojificha kuliko yale tunayodhani kuwa tunayajua. Tukio la Septemba 11 lina utata ambao ni vigumu kuutatua. Vyombo vingi vya habari vimeandika tu yale ambayo watawala walitaka yaandikwe. Lakini ukweli wote wa yaliyotokea ni Mungu peke yake anayeujua.
Mwandishi wa makala haya ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754-989837 au E-mail: shao2020@yahoo.co.uk.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment