Tuesday, January 16, 2007

Tuogope silaha za kibaiolojia?


Silaha za biolojia ni hatari kiasi gani?

Na William Shao


Silaha za baiolojia ni hatari kiasi gani? Kuna haja ya kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na matumizi ya silaha za kibaiolojia? Hizo ni silaha hatari kuliko nyingine?

Mara baada ya mashambulizi ya World Trade Center huko New York na makao makuu ya kijeshi ya The Pentagon, Washington, DC. kile ambacho awali kilifikiriwa kuwa ndoto kilibainika kuwa kingeweza kuwa kweli, na kimekuwa kweli—yaani matumizi ya silaha za kibaiolojia. Baada ya hapo kuliibuka mashambulizi ya kutumia ‘vimeta’.

Wakati mmoja, jarida la ‘New Scientist’ lilikuwa na habari hii ya kushtua: “Shirika la Afya Duniani (WHO) linatambua hatari inayozidi kuwa kubwa ikiwa silaha za kibaiolojia zitatumiwa kuwashambulia watu …na kusambaa duniani pote.”

Jarida hilo liliendelea kuonya hivi: “Mataifa yote yamo hatarini. Shambulio la kutumia viini vya ugonjwa wa ndui, tauni na kimeta linaweza kuwa hatari sana kwa sababu litaleta magonjwa na vifo, na woga utakaowakumba watu utalifanya tatizo hilo kuwa kubwa na baya zaidi.”

Utafiti mmoja wa kisayansi uliochapishwa katika jarida la ‘Scientific American’ umegundua kuwa, “Tofauti na mabomu, kwa kawaida shambulio la kibaiolojia huwa la siri.” Kwanini?

Wanasayansi waliofanya utafiti huo wanatambua kwamba ugonjwa huenea bila kugunduliwa. Dalili zake huwatatanisha madaktari, na mara nyingi hufanana na zile za magonjwa ya kawaida. Na kabla wataalam wa tiba hawajajua kinachoendelea, maeneo makubwa yatakuwa yameshaambukizwa.

Dk. Devra Davis, akikaririwa na gazeti la ‘Science News’, alisema: “…Ikiwa watu watashambuliwa na viini vya ugonjwa wa ndui leo watu wengi duniani hawatakuwa na kinga.”

Dk. Davis ana wasiwasi kwamba ikiwa hilo litatokea, “…karibu watu bilioni mbili (2,000,000,000) watakufa, kwa sababu ugonjwa huo huua asilimia 30 ya wale walioambukizwa viini vyake.”

Taarifa hizo ni za kutisha. Hiyo inadokeza kuwa ingawa sayansi imefanya mambo mengi, haina nguvu ya kutosha kuzuia maafa yasitokee ikiwa kutakuwa na watu watakaoamua kuitumia sayansi hiyo kusababisha maafa duniani.

Hata hivyo, juhudi za kuwaua watu vitani kwa kutumia viini vya magonjwa hatari si jambo jipya. Katika karne ya 14, kwa mujibu wa kitabu cha ‘The Hundred Years War: The English in France, 1337-1453’ cha Desmond Seward, huko Ulaya mashariki, “…maiti za watu waliouawa kwa tauni zilitupwa ndani ya jiji lililozingirwa.”

Karne nne baada ya hapo, maafisa wa Uingereza waliwapatia Wahindi Wekundu Waamerika mablanketi yaliyotiwa viini vya ugonjwa wa ndui katika ule mkutano wa amani wakati wa vita ya Ufaransa na Wahindi. Kwa njia hiyo, Wahindi walisalimu amri. Lakini hilo halikugunduliwa haraka—angalau na waathirika.

Mwishoni mwa karne ya 19 ikagunduliwa kwamba magonjwa ya kuambukiza husababishwa na viini. Kugundua huko kukafungua njia ya kutumia ugonjwa kama silaha.

Kwa kuutazama ukweli huo wa kihistoria, maendeleo ya sayansi ya tiba yamesaidia sana kuvumbuliwa kwa dawa na chanjo mbalimbali ambazo zimesaidia sana kuzuia na kutibu magonjwa mengi—si yote.

Ingawa kuna maendeleo hayo, magonjwa ya kuambukiza yameendelea kuwa tishio kwa mwanadamu, huku yakiua karibu watu milioni 20 kila mwaka—kwa mahesabu ya kawaida, hiyo ni zaidi ya watu 54,000 kila siku. Kwa kutafakari kijuujuu, ni vigumu kuziamini tarakimu hizo.

Wakati kukiwa na watu wenye bidii na kutoa maisha yao kwa ajili ya kupambana na maradhi na kuyatokomeza, wengine wanajitahidi zaidi kutafuta namna ya kuwashambulia wengine kwa magonjwa.

Kwa karibu miaka 30 iliyopita, Marekani, Urusi na mataifa mengine moja moja yalitumia muda na sehemu fulani ya pesa zao zote kwa ajili ya kutengeneza silaha za kibaiolojia, ingawa yalikubaliana kupiga marufuku silaha hizo mwanzoni mwa miaka ya 1970. Pamoja na kwamba kupigwa marufuku huko kulifanyika kwa njia ya wazi, mataifa mengine yaliendelea kufanya tafiti zao kwa siri.

Hata hivyo, katika miaka hiyo ya 1970, ingawa ilijulikana kuwa silaha za kibaiolojia ni hatari sana, hazikuwa na matokeo mazuri zilipotumiwa vitani, kwa sababu, kwanza, matokeo yake hayaonekani mara moja.

Sababu ya pili ni kwamba matokeo yake hutegemea mabadiliko ya upepo na hali ya hewa. Kwa kuwa muhtasari wa utafiti huo wa kisayansi ulitolewa mwaka 1970, inawezekana kwamba kule kupigwa marufuku kwa silaha hizo mwaka 1972 kulichochewa na utafiti huo.

Kupigwa marufuku kwa silaha hizo kulitokea katika ule mkutano wa mataifa 100 ambayo yalitia saini mkataba wa kimataifa uliopiga marufuku kubuni, kuunda na kuhifadhi silaha za biolojia. Mkataba huo uliitwa ‘Biological and Toxin Weapons Convention’ (BTWC).

Ulikuwa ni wa kwanza kupiga marufuku silaha zote za aina moja. Kwa kuwa hawakuwa na hakika kama mkataba huo uliheshimiwa au la, wajumbe wa nchi kadhaa walianza kujadili mkataba mwingine mwaka 1995 kuchunguza kama maamuzi yao ya mkutano wa 1972 yaliheshimiwa.

Desemba 7, 2001, karibu miaka 30 baadaye, mkutano wa wiki tatu uliohudhuriwa na mataifa 144—miongoni mwa hayo ni yale yaliyotia saini mkataba wa 1972—ulimalizika kwa vurugu. Chanzo cha vurugu hiyo ni Marekani ilipopinga mapendekezo kadhaa yaliyotolewa katika mkutano.

Hata hivyo, haielekei kwamba sababu hizo mbili—kule kukosa matokeo mazuri na kutegemea mabadiliko ya upepo na hali ya hewa—zinaweza kuwazuia watu wenye chuki dhidi ya wengine kuzitumia silaha hizo, kama inavyotokea kwa magaidi. Wanaotamani kuua wanatamani sana kutumia silaha hizo ikiwa zitatimiza malengo yao.

“Silaha za kibaiolojia zinaweza kuundwa na kutumiwa kwa siri,” anasema Frederic J. Brown katika kitabbu chake, ‘Chemical Warfare: A Study in Restraints’. Brown anasema inawezekana yule anayezitumia asijulikane. “Hata akijulikana, ni vigumu zaidi kuadhibu makundi ya kigaidi yenye makao yao katika nchi nyingi.”

Lakini fikra peke yake juu ya matumizi ya silaha za aina hiyo zinatisha hata zaidi. Robert Harris na Jeremy Paxman, katika kitabu chao, ‘A Higher Form of Killing: The Secret Story of Chemical and Biological Warfare’ © 1982, wanasema:

“Shambulio la kibaiolojia lililofanywa kimya-kimya, lisiloonekana, linaloendelea kwa muda fulani, na ambalo ni hatari, linaweza kuwapa watu kiwewe cha ghafla. …Kushambulia mimea na mifugo kutasababisha kuzorota kwa uchumi na kupungua kwa chakula.”

Lakini kuna jambo lingine linalowavutia watu kutumia silaha za aina hiyo. Ni kwa sababu ya gharama yake nafuu kwa kulinganisha na silaha nyingine wanazohitaji kutimiza malengo yao.

Uchunguzi mmoja, kwa mujibu wa Jeanne McDermott katika kitabu chake, ‘The Killing Winds’, ulilinganisha gharama za kuua raia waliochoka kwa kutumia silaha mbalimbali katika eneo la kilometa moja ya mraba ukagundua kuwa gaharama ya kutumia silaha za kawaida ilikadiriwa kuwa dola 2,000 za Marekani, silaha ya nyuklia dola 800, gesi ya mishipa ya fahamu dola 600 na silaha za kibaiolojia dola moja tu.

Taarifa za vyombo vya habari zinaonesha kuwa makundi fulani ya kigaidi yamejaribu kutumia silaha za kibaiolojia. Hata hivyo, kama Jeanne McDermott anavyosema katika chapa mpya ya kitabu cha ‘The Menace of Biological Warfare’, “Kuna tofauti kubwa kati ya kujaribu kutumia silaha za baiolojia na kufanikiwa kuzitumia.”

Ili gaidi afanikiwe kuzitumia silaha hizo, lazima afanikiwe kuijua teknolojia yake. Ni lazima viini hatari vipatikane, na ni sharti ajue jinsi ya kuvihifadhi vizuri na kuvitumia kwa usalama. Jambo lingine ambalo gaidi anapaswa kulijua ni namna ya kutengeneza viini vingi vya aina hiyo.

Donald Worsten, katika kitabu chake, ‘Nature’s Economy’ © 1984, anasema: “Kiasi kidogo cha viini kinaweza kuharibu kabisa shamba nzima la mimea, kuteketeza kundi kubwa kabisa la mifugo, au mji mzima uliojaa watu, vikitumiwa inavyotakiwa.”

Hata hivyo, “…Viini havinawiri vizuri nje ya maabara,” akaandika Sterling Seagrave katika kitabu chake, ‘Yellow Rain: A Journey Through the Terror of Chemical Warfare’. “Kwa sababu kiasi kidogo tu cha viini ndicho ambacho huwafikia watu waliokusudiwa,” akaandika Seagrave, “ni lazima kiasi kikubwa mno kitengenezwe ili kuangamiza watu wengi.”

Kulingana na wanasayansi, kuna mambo mengi sana ya kuzingatiwa katika jambo hili. Brown aliyetajwa hapo juu, katika kitabu cha ‘Chemical Warfare: A Study in Restraints’ anasema:

“Ni sharti gaidi ajue jinsi ya kuhifadhi viini vikiwa hai na katika hali ya uhai wakati anapovisafirisha kutoka mahali vilipotengenezewa hadi mahali anapokusudia kuvitumia.

“Mwishowe, ni lazima ajue jinsi ya kuvisambaza viini hivyo kwa njia inayofaa, hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba viini vilivyo na ukubwa unaofaa vinawafikia watau waliokusudiwa, vinasambazwa katika eneo kubwa kiasi cha kutosha na vinaweza kuwaambukiza watu wengi.”

Watafiti wa silaha za baiolojia kama Jeremy Paxman waliobobea walitumia miaka zaidi ya kumi kukamilisha mfumo unaotegemewa wa kutumia silaha hizo. Kwa mujibu wa kitabu chake, viini hivyo kufa vinapotupwa hewani kutokana na mwanga wa jua na kubadilika-badilika kwa hali joto. Kwa sababu hiyo, ili mtu aweze kutumia viini vya magonjwa vitani ni lazima kwanza ajue hali ya viini hivyo vikiwa hewani.

Kwa mujibu wa utafiti mmoja wa kisayansi, kwa kuzingatia matatizo mengi ya teknolojia ya kutumia silaha za biolojia, haishangazi kwamba kumekuwa na mashambulizi machache sana ya silaha za aina hiyo.

Hata hivyo, ingawa zimetumiwa, mashambulizi ya silaha hizo hayajaleta maafa makubwa. Kiasi cha watu watano walikufa kutokana na shambulio la barua zilizokuwa na viini vya kimeta lililotokea Marekani mara baada ya shambulio la kigaidi la Septemba 11, 2001.

Ingawa lilikuwa tukio baya, halikuleta maafa makubwa kama ambavyo yangesababishwa na bomu dogo la kutupwa kwa mkono au bastola. Lakini wengi walishikwa na kiwewe.

Kwa mujibu wa ‘A Higher Form of Killing: The Secret Story of Chemical and Biological Warfare’ (chapa mpya ya 2000), watafiti wamehesabu watu waliokufa kutokana na mashambulio ya silaha za kemikali na za baiolojia tangu 1975 na kugundua kwamba katika asilimia 96 ya mashambulizi hayo, ni watu watatu tu waliojeruhiwa au kuuawa katika kila shambulio lililofanywa.

Kwa kuzingatia ugumu uliopo wa kushambulia kwa silaha za biolojia, Shirika la Uingereza na Marekani la Habari za Usalama lilisema: “Ingawa serikali zinakabiliana na vitisho vingi kutoka kwa magaidi wanaotumia silaha za kemikali na biolojia, watafiti wanaamini kwamba mashambulizi kama hayo, ingawa yanaweza kutokea, huenda yasiweze kusababisha maafa makubwa.”

Hata hivyo, ingawa huenda mashambulizi kama hayo yasiwepo, matokeo ya shambulio lolote kwa kutumia silaha hizo yanaweza kuwa mabaya kuliko inavyoweza kufikiriwa.

Matatizo ya kiteknolojia na ukweli wa kihistoria vinadokeza kwamba mashambulizi ya silaha za kibaiolojia na kemikali yanayoweza kuleta maafa makubwa huenda yasitokee—haifikiriki kwamba yatatokea. Hata hivyo, mara nyingi, kisichofikirika hutokea.

Lakini historia ni historia. Kwa kawaida ni vigumu kuitegemea historia ili kupata uhakika wa mambo ya siku zijazo. Hakuna historia inayotoa mwingozo wa mambo ambayo hayajatokea mbeleni.

Kazi ya historia ni kuzungumza mambo yaliyopita. Kwa lugha rahisi, historia si utabiri wa mambo yanayokuja. Ingawa historia inasema kuwa mashambulizi ya zamani hayakufanikiwa, haisemi mashambulizi yajayo yatashindwa.

Inaonekana kuwa magaidi wanaoongezeka wameazimia kuua watu wengi kwa njia yoyote rahisi kwao. Wanapata teknolojia nyingi na za kisasa zaidi. Na zaidi ya yote, kuna makundi ya kigaidi yanayopata pesa na ufundi mwingi kuliko serikali fulani fulani.

Kuna uwezekano pia kwamba hata wanasayansi waliobobea katika kazi zao wanaweza kutumiwa na magaidi baada ya kuahidia donge nono. Tayari wanasayansi wanajua namna ya kubadili viini vilivyopo viwe hatari zaidi na rahisi zaidi kutumia.

Kwa mujibu wa ‘New Scientist’, wanasayansi sasa wana uwezo wa kugeuza chembe za viini visivyo hatari na kutengeneza sumu, na viini vinaweza pia kugeuzwa visigunduliwe kwa kutumia njia za kawaida. Zaidi ya hilo, viini vinaweza kubuniwa ili viweze kuhimili bacteria, chanjo za kawaida na tiba.

Mtafiti Rose Kushner katika kitabu chake, ‘Alternatives: New Developments in the War on Breast Cancer’, anasema: “Wanasayansi wanaweza kugeuza chembe za urithi na kusababisha viini vingi ambavyo ni hatari zaidi, sugu zaidi, na ambavyo ni rahisi kuzalisha na kutumiwa.” Hilo linamaanisha kwamba wanaweza kutengeneza silaha nyingi za kibaiolojia kwa kugeuza tu chembe za urithi.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia, kadiri yanavyotia matumaini katika tiba, ndivyo yanavyoondoa matumaini hayo kwa kiasi fulani. Ni kama alivyosema Sterling Seagrave katika kitabu cha ‘Yellow Rain: A Journey Through the Terror of Chemical Warfare’:

“Huu ni mwanzo tu …Ni jambo la kumfanya mtu akae na afikiri anapotambua kwamba maendeleo zaidi yanakuja,”—maendeleo yatakayotumiwa kinyume na watu wenye nia za kuwaharibu binadamu wengine.

Mwisho…


No comments: