Showing posts with label Uchambuzi. Show all posts
Showing posts with label Uchambuzi. Show all posts

Monday, February 5, 2007

USIRIDHIKE NA MTAZAMO WA JUU-JUU TU



TURIDHIKE NA MTAZAMO WA KIJUU-JUU TU?





Na William Shao

NILIPOSOMA makala katika gazeti RAI toleo la 689 yenye kichwa cha habari: PRINCESS DIANA ALIFARIKI DUNIA KWA AJALI YA MUNGU YUPI? Nilisukumwa na hitimisho la mwandishi lililosema: “Kwa vyovyote kifo cha Princess Diana ni ajali iliyotokana na Mungu.”

Mwandishi aliyesema makala hayo yaliandikwa kwa msaada wa “mashirika ya habari”, aliridhika na ripoti ya kurasa 832 ya Lord (Sir John) Stevens iliyoonyesha kuwa Princess Diana alikufa katika ajali ya kawaida “na si kwamba aliuawa na Serikali ya Uingereza ama ukoo wa kifalme.”

Sisemi ripoti ilidanganya, nasema tutazame matukio ya uhakika bila kugusa au kuridhika na ripoti hiyo. Hiyo ni ripoti ya serikali na serikali ingejitahidi isijishutumu yenyewe.

Hata hivyo, udadisi hautoshi kuishia katika ripoti tu. Habari peke yake hazitoshi kutufunua akili bila kwanza kutazama utondoti na mambo mengine madogo madogo yaliyotengeneza habari au ripoti hiyo. Ni kweli Diana alikufa katika ajali ya gari, lakini tunajuaje kuwa ajali hiyo ni “iliyotokana na Mungu” au iliyopangwa na mwanadamu?

Ikiwa wale wanaodai Princess Diana aliuawa ni ‘wenda-wazimu’, Diana mwenyewe alikuwa ‘mwenda-wazimu’ wa kwanza na kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, alikuwa wa pili.

Miezi kumi kabla ya kifo chake Diana aliandika barua iliyosomeka: “Kipindi hiki cha maisha yangu ni cha hatari sana kwangu” na kudai Ufalme wa Uingereza unamwandalia kifo cha ajali ya gari. (Mirror la Uingereza Okt. 20, 2003).

Jumanne ya Septemba 2, 1997—siku mbili baada ya kifo cha Diana—Gaddafi alidai kuwa Serikali ya Uingereza na washirika wake walimuua Diana. Walimwengu tulimchukulia kiongozi huyo kama ‘mpayukaji’.

Ukitazama kwa makini mazingira yanayozunguka kifo cha Diana utaona mambo mawili: Moja ni ‘mazingira ya kisiasa’ na la pili ni ‘mazingira ya ibada za kishetani’. Kwa kuwa nafasi ni finyu, najadili hili la ‘mazingira ya kisiasa’, na hilo la pili naliacha kiporo. Katika mijadala inayokuna kama hii ndipo mtu anapoonekana mwenda-wazimu.

Princess Diana na Dodi Fayed walitumbukia rasmi katika mapenzi Jumanne ya Juni 3, 1997. Siku 38 baadaye, Ijumaa ya Julai 11, 1997, Princess Diana aliwasili kwenye nyumba ya shamba la Mzee Al Fayed yenye bustani kubwa eneo la San Tropez, kusini mwa Paris, Ufaransa, akiwa na watoto wake, William na Harry.

Wakati huo Dodi Fayed alikuwa chumbani kwake na mchumba wake, Kelly Fisher, mwanamitindo wa Mmarekani. Dodi hakuwakutanisha Kelly na Diana. Wakati Baadaye Diana akiwa katika boti, ndege binafsi ilitumwa kwa ajili ya Kelly. Diana na Kelly hawakujuana.

Kelly alikasirika sana alipogundua kuwa Dodi alimzubaisha ili apate nafasi ya kumtongoza Diana. Hatimaye Diana alirejea Uingereza na watoto wake. Ndipo siku 20 baadaye, Alhamisi ya Julai 31, Diana akarejea tena San Tropez, wakati huu akiwa bila watoto wake. Bado hakujua Dodi alikuwa na uhusiano na Kelly hadi aliposikia katika vyombo vya habari.

Siku hiyo, Julai 31, Kelly Fisher alikuwa Los Angeles, Marekani, akijiandaa kwa ajili ya harusi kati yake na Dodi Fayed iliyokuwa imepangwa kufanyika Jumamosi ya Agosti 9, 1997. Lakini siku mbili kabla ya hapo akavisikia vyombo vya habari duniani vikitangaza mapenzi kati ya Dodi na Diana. Huo ukawa mwisho wa Dodi na Kelly.

Jumba hilo la kifahari lilikuwa limefungwa vinasa sauti kufuatilia mazungumzo ya Diana. Kila alichozungumza Diana hakikuwa siri kwa wale waliomfuatilia. “Ulikuwa ni utendaji wa aina ya peke yake,” akasema Henry Porter, mhariri wa jarida Vanity Fair, akimkariri Bob Loftus aliyewahi kuwa mkuu wa usalama wa Mohamed Al Fayed.

Kwanini alikuwa akifuatiliwa kiasi hicho? Ni nani walikuwa wakimfuatilia. Ni siri gani walihitaji kutoka kwake?

Wakati Diana anaanza masaa matatu ya mwisho ya uhai wake, saa 3.47, ulizuka uvumi kwamba alikuwa na mpango wa kufunga ndoa na Dodi. Kisha uvumi huo ukawavuta hata mapaparazi (wapiga picha) kupata picha za wapenzi hao.

Dakika za mwisho za maisha yake zilianzia Hotel Ritz Paris inayomilikuwa na Al Fayed. Ulinzi aliokuwa nao—gari aina ya Range Rover iliyokuwa na watu wa kumlinda ikifuata nyuma ya gari alimokuwamo—uliondolewa. Kwa hiyo ulinzi wake ulipunguzwa.

Kwanini ulinzi ulipunguzwa ikiwa tayari ilijulikana kulikuwa na mapaparazi waliokuwa wakimwandama? Kama ilivyokuwa kwa Diana, hata wakati Rais John Kennedy alipouawa, ulinzi wake ulipunguzwa.

Gari la Kennedy halikuwa na walinzi, lakini lililokuwa nyuma yake lilikuwa na ulinzi mkali. Inasemekana hiyo ndiyo mbinu inayotumika katika mauaji ya aina hiyo. Kennedy alikuwa amepanda gari lililokuwa wazi katika mji uliokuwa hatari bila walinzi.

Wakati mtetezi wa haki za binadamu, Martin Luther King, alipouawa eneo la Memphis, Tennessee, Marekani Alhamisi ya Aprili 4, 1968, polisi mwenye asili ya Kiafrika aliyekuwa akimlinda bila kupenda alilazimishwa kuondoka kazini saa chache kabla King hajapigwa risasi.

Zimamoto wawili wenye asili ya Kiafrika waliokuwa katika kituo karibu na Lorraine Motel alimouawa Luther walihamishiwa kituo kingine cha saa chache kabla ya tukio.

Baada ya mauaji dunia ikaambiwa kuwa James Earl Ray (40) ndiye muuaji wa Luther. Lakini hata familia ya Luther haikuamini kama James Ray alihusika na kifo cha Luther. Hadi leo matokeo ya chunguzi nyingi za kifo hicho zinatatanisha.

James Ray alipofariki dunia Alhamisi ya Aprili 23, 1998, baadhi ya wanafamilia wa Martin Luther waliohudhuria mazishi yake walimlilia Ray, wengine wakisema hawana imani kwamba alihusika na kifo cha Luther.

Wakati mwanasiasa na mwanasheria wa mazingira wa Marekani Robert (Bobby) Kennedy alipouawa Jumanne ya Juni 4, 1968, mara baada ya hotuba yake katika Ambassadors Hotel mjini Los Angeles, Marekani, mpangilio wa ulinzi wake ulivurugwa—ndipo akauawa.

Mipango ilikuwa kwamba baada ya hotuba yake angetoka ukumbini kwenda nje kupita katikati ya kundi la watu, lakini alipomaliza hotuba ‘wasaidizi’ (wauaji!?) wake, hususan Frank Mankiewicz, alisisitiza kuwa ilikuwa ni salama kwake kutoka ukumbini kwa kupitia jiko la hoteli badala ya katikati ya umati wa watu.

Kennedy alipofika jikoni ndipo alipokutana na “muuaji” wake, Sirhan Bishara Sirhan, akiwa na bunduki mkononi. Hata hivyo, upelelezi binafsi unadai kuwa Robert Kennedy aliuawa na walinzi wake, hususan Thane Eugine Caesar.

Wapelelezi wengine wanasema Thane Caesar, ambaye alipaswa kumlinda Kennedy, ndiye aliyemfyatulia risasi tatu zilizohitimisha uhai wake. Upelelezi mwingine ulipoanza kugundua mambo mengine, vielelezo vingi vilifichwa.

Frank Mankiewicz, ambaye alimwongoza Robert Kennedy kwenda jikoni alikouawa, awali alikuwa msemaji wa tawi la Shirika la Kijasusi la Israel (Mossad) nchini Marekani lijulikanalo kama Anti Defamation League.

Wakati Waziri Mkuu wa Israel, Yitzhak Rabin, alipouawa Jumamosi ya Novemba 4, 1995 mjini Tel Aviv, ilidaiwa, kwa mujibu wa filamu ya tukio hilo, ulinzi wake ulisogezwa nyuma kuruhusu muuaji—au wauaji—kumpata mlengwa wao.

Hayo ndiyo yalitokea katika zile dakika, au saa, muhimu sana katika maisha ya Diana. Ama ulinzi uliondolewa au haukuondolewa, lakini hakuwa na ule ulinzi kama wa siku zote alipokuwa Paris. Ulinzi huo ulikwenda wapi? Nani aliuondoa? Kwanini?

Kwa siku nzima ya Agosti 31 alipokuwa jijini Paris, tangu Julai 31, Diana alisafiri katika gari hilo hilo, Mercedes Benz, likisindikizwa kwa nyuma na gari lingine aina ya Range Rover lililokuwa na walinzi. Walinzi hao walikwenda wapi Diana alipoikaribia mauti yake? Kwanini wasiwepo wakati wa kufa kwake?

Mercedes Benz aliyokuwa akisafiria kwa siku nzima siyo Mercedes Benz ile ile aliyopata nayo ajali. Kwanini ilibadilishwa? Jibu la swali hili linaweza kueleza mambo mengi muhimu.

Badala ya Mercedes Benz ambayo Diana alikuwa akiitumia na Dodi hadi mchana wa siku hiyo, lililetwa gari lingine (Mercedes) muda mfupi kabla mauti haijapiga hodi.

Tofauti na lile la mwanzo lililoegeshwa lango la mbele, hili la pili lilipelekwa lango la nyuma la hoteli. Gari hilo ni la kampuni ya kukodisha magari inayojulikana kama Etoile Limousines (inadaiwa inamilikiwa na Al Fayed).

Hili gari lililoletwa baadaye, Mercedes Benz S-280, lilikuwa na vioo vya giza tofauti na Mercedes Benz S-600 waliliokuwa wakitumia tangu alipowasili Paris Julai 31 ambalo halikuwa na vioo vya giza. Magari mengine yangeweza kupatikana kutoka katika kampuni hiyo, lakini hili lilifaa zaidi. Kwanini?

Akihojiwa na wapelelezi wa kifo cha Diana, Mkurugenzi wa Etoile, Niels Siegel, alisema yeye ndiye aliyelipeleka gari hilo lango la nyuma la hoteli ya Ritz badala ya lango la mbele, lakini wapelelezi wengine waligundua kuwa alikuwa akidanganya. Kisha wakaanza kuwa na wasiwasi.

Iligundulika kuwa aliyelipeleka gari hilo siyo Siegel, bali ni dereva aliyeitwa Frederic Lucard. Ilijulikana hivyo baada ya kuonekana katika kamera za hoteli hiyo siku ya tukio. Kama hakukuwa na jambo la kuficha, kwanini mkurugenzi wa Etoile alidanganya?

Lucard alipobanwa na mmoja wa wapelelezi alionyesha kushangazwa sana kwa kampuni “makini” kama Etoile kumruhusu mtu kama Henri Paul (dereva aliyewaendesha Diana na Dodi hadi vifo vyao) kuendesha magari ya kampuni hiyo kwa sababu “hakuwa amefuzu kama dereva...”

Gari hilo likiendeshwa na Henri Paul, likiwa na Diana na Dodi (wakiwa kiti cha nyuma) pamoja na mlinzi wao, Trevor Rees-Jones, liliondoka lango la nyuma la Ritz saa 6:20 usiku.

Kufika katika taa za barabara ya Place de la Concorde, inasemekana kuwa paparazzi mmoja, Romuald Rat, akiwa katika pikipiki, aliiona gari ikisimama kidogo na kisha kupita kwa kasi kwenye taa nyekundu kuelekea barabara ya Cours la Reine kandokando ya Mto Seine. (rejea kiungo hiki cha tovuti: http://www.wethepeople.la/diana13.htm )

Baadaye kidogo gari ilipoteza mwelekeo kisha ikagonga nguzo ya 13 ya barabara ya chini kwa chini ya Ponte de L’Alma. Henri Paul na Dodi Fayed walifariki dunia papo hapo. Diana alifariki dakika kadhaa baadaye.

Ingawa wengi wanaamini kwamba ‘wapenzi’ hawa walikuwa wakielekea katika nyumba ya Dodi iliyoko karibu na Arc de Triomphe wakitokea Hotel Ritz, ukitazama ramani ya Paris (Paris Guide Map) ukweli ni kwamba hawakuwa wakielekea kwa Dodi bali walikuwa wakienda upande ulio kinyume na huo.

Mara baada ya ajali hiyo, mambo mengi yalitendeka hadi Diana alipotangazwa rasmi kwamba amefariki dunia. Upelelezi fulani fulani unaonyesha kuwa alikuwa akiongea hata dakika kadhaa baada ya ajali, lakini haijaelezwa alichozungumza.

Ingawa Diana na Dodi walipata ajali katika gari moja, mwili wa Diana ulifanyiwa uchunguzi lakini ule wa Dodi haukufanyiwa. Hii inatuleta kwenye swali lingine. Kwanini Dodi hakufanyiwa uchunguzi kama Diana ikiwa wote wawili walihusika katika ajali ile ile moja? Uchunguzi aliofanyiwa Diana lakini asifanyiwe Dodi ulikuwa wa nini?

Kuna wanaodai kuwa Diana alikuwa na mimba ya Dodi. Huenda hili si la kweli kwa sababu ni Diana peke yake, na pengine Dodi, angeweza kukiri au kukanusha. Lakini namna gani ikiwa watatokea “wenda-wazimu” wengine wakasema kuwa uchunguzi aliofanyiwa Diana ni kuhakikisha kuwa mimba aliyokuwa nayo inaondolewa ili kupoteza ushahidi wa kwamba alikuwa nayo? Hawa tutawaita “wehu”?

Ni vigumu kujua kama Diana alikuwa na mimba. Lakini Ijumaa ya Septemba 19, 1997, jarida TIME lililikariri shirika la habari la Ufaransa Agence France-Presse (AFP) likisema kwamba hadi siku ya ajali “huenda Diana alikuwa na mimba ya wiki sita.” Gazeti The Chicago Tribune (Julai 15, 1997) lilimripoti Diana akiwaambia waandishi hivi:

“Mtapata mshangao. Mtaona. Mtashangaa mtakapoona jambo nitakalofanya.” Alikuwa akizungumza kuhusu ujauzito wake? Alikuwa akigusia kuoana na Dodi? Jibu lolote kwa maswali hayo ni la kubuni.

Jarida TIME (Sept. 8, 1997) lilimkariri Frederic Maillez, tabibu wa dharura aliyekuwa wa kwanza kufika eneo la ajali, akisema kuwa wakati fulani (wakati hajakata roho) Diana alitamka kuwa alikuwa na mimba ya wiki tatu huku akishika tumbo lake. Inawezekana kuna mambo mengi alisema, lakini hatutaambiwa aliyosema.

Mmoja wa watu waliofanya upelelezi juu ya ajali hiyo ni polisi mstaafu aliyeitwa John Stalker. Aliposokia watu wakisema Serikali ya Ufaransa imekula njama ya kumuua Princess Diana, aliingiwa na swali moja la msingi:

“Kwanini Serikali ya Ufaransa imuue mwanamke wa Uingereza?” Stalker alianza kwa kuukataa uwezekano wa njama. Lakini kadiri muda ulivyopita aliingiwa na mashaka zaidi.

“Kwanini usalama wote wa Fayed aliopewa Diana ulipunguzwa hadi kufikia mlinzi mmoja asiyeaminika (Rees-Jones) na bila gari ya kusindikiza? Kwanini polisi haikuomba msaada kutoka kwa umma? Kwanini mwili wa Dodi Fayed haukufanyiwa uchunguzi?” Nilisoma maswali aliyokuwa akiuliza, lakini sijui kama aliwahi kupata majibu.

Baada ya ajali hiyo, wataalamu wa magari ya Mercedes Benz waliiomba serikali ya Ufaransa walifanyie uchunguzi gari hilo, lakini maofisa wa serikali walikataa. Kwanini? Lilikuwa na kasoro gani? Kitu gani kilikuwa kinafichwa hapo? Kama walitaka mambo yawe wazi kwanini walikataa ombi hilo?

Kama ilivyo katika mambo mengine yanayofanana na hili, kisingizio, au ‘kisababishi’, kilipatikana. Jambo la kwanza kufanyika ni kutuhumu watu.

Ikasemwa kuwa dereva Pauli Henri ni chanzo kwa sababu alikuwa amelewa kupita kiwango kinachoruhusiwa kisheria nchini Ufaransa. Lakini uchunguzi ukaonyesha hakuwa amevuka kiwango cha ulevi. Baadaye kidogo wimbo ukabadilika. Paparazzi ndio chanzo.

Kuna zaidi ya hayo. Inasemekana kuwa katika Jiji la Paris, moja ya miji sita mikubwa zaidi duniani, kuna kamera nyingi zilizoko maeneo yote ya barabara jijini humo—hasa eneo la Ponte de L’Alma ilipotokea ajali.

Ikiwa kamera hizo zingekuwa zinafanya kazi usiku huo ingekuwa ni rahisi kumaliza ubishi wote kwa sababu picha zake zingeonyesha kilichotokea na namna kilivyotokea.

Kamera moja inayotazama chini katika lango la kuingia katika barabara hiyo ya ardhini ingeweza kuona gari aina ya FIAT UNO inayodaiwa kusababisha ajali (kisingizio cha tatu), au watu waliokuwa katika pikipiki zinazodaiwa zilimfanya Henri Paul ashindwe kudhibiti gari lake.

“Lakini kamera hiyo, kama zilivyokuwa nyingine zote, ilikuwa imezimwa katika wakati huo muhimu sana,” kinasema kitabu Who Killed Diana kilichoandikwa na Simon Regan ambaye amekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi kwa miaka 35.

Kitabu The Biggest Secret © 1999 kinasema: “Hakuna wakati mwingine wowote katika historia ya Paris ambao mfumo huu wa kamera umekuwa na hitilafu kwa wakati mmoja na polisi wakakataa kueleza kilichotokea.”

Mfumo huo wa kamera hutumia umeme unaojitegemea na unaendeshwa na polisi na, “hasa hasa,” kinasema The Biggest Secret, “mawakala wa Shirika la Kijasusi la Ufaransa, kwa sababu kamera hizo zimewekwa maeneo hayo kwa ajili ya mambo mengi zaidi ya kutazama magari tu.”

Wakati huo huo ambao mfumo huo wa kamera ulipofeli, mawasiliano yote ya redio za polisi katika maeneo ya kati ya Paris yalizimika. Kwanini mambo hayo yatokee kwa wakati mmoja, hasa katika dakika chache kuelekea kifo cha mwanamke maarufu zaidi duniani?

Swali linaweza kuzuka. Kama Diana aliuawa, nani aliyeandaa mauaji hayo? Anayetoa amri ya kuua si lazima awe muuaji. Katika mtandao—au tuseme utando, buibui anaweza kuandaa mipango, lakini mipango hiyo ikatekelezwa na nzi, pengine bila nzi huyo kutambua.

Wanaoandaa kile kinachoitwa ‘nadharia ya kigwena’ wana mambo mengi zaidi ya kuzungumza, na ni mambo ambayo dunia inahitaji kujua.

Kwa mfano, kuna ushahidi kwamba Rais John Kennedy hakuuawa na Lee Harvey Oswald kama ilivyodaiwa awali, bali aliuawa na mtu kutoka Kikosi cha Jeshi la Siri (OAS) la Ujasusi la Ufaransa na, ushahidi mwingine unadai, wauaji hao walipata mafunzo kutoka kwa “muuaji mkuu” wa Mossad (Israel) katika Bara la Ulaya aliyeitwa Yitzhak Shamir.

Kwa mujibu wa Encyclopedia of Terrorism © 2002, miaka 20 baada ya mauaji ya Kennedy Novemba 1963, Shamir akawa Waziri Mkuu wa Israel (1983-1984 na 1986-1992) hadi aliposhindwa na Yitzhak Rabin katika uchaguzi wa 1992. Alikuwa mpinzani wa Rabin, je, alishiriki katika kumuua? Ni vigumu kujua!

Sven Olof Joachim Palme, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Sweden, inadaiwa—hii haijathibitishwa—wauaji wake walipokea amri ya mauaji kutoka kwa Baba George Bush. Mauaji hayo yalitekelezwa na majasusi wa Afrika Kusini wanaojulikana kama BOSS (South African Bureau Of State Security).

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ina kikosi chake cha siri (cha mauaji) kinachojulikana kama Group 13. Ujasusi wa Uingereza una vikosi kama MI5 (Military Intelligence 5) ambacho kinashughulikia ‘usalama’ wa ndani na MI6 (Military Intelligence 6) kinachoshughulikia mambo ya nje.

Mwaka 1998 MI5 kilidai kuwa hakiui watu. Lakini haiwezekani inatuma wengine waue badala yake? Kauli hiyo ilikuja baada ya ofisa wa MI5, David Shayler, kufichua siri kwamba MI6 ilikula njama za kumuua Kanali Gaddafi wa Libya.

Jaribio hilo lilishindwa kwa sababu bomu lililokusudiwa lilitegwa kwenye gari tofauti na alilopanda Gaddafi. Hii ilikuwa Februari 1996. Gaddafi alinusurika, lakini watu kadhaa waliuawa.
Miaka kumi kabla ya hapo, Jumanne ya Aprili 15, 1986, Gaddafi alinusurika wakati ndege za Marekani, zikitokea Uingereza, zilipokusudia kumuua yeye na familia yake. Ingawa hakuuawa, raia 55 wasio na hatia mjini Tripoli, pamoja na binti mmoja wa Gaddafi, waliuawa katika shambulio hilo.

Shayler aliiambia BBC kwamba MI6 ilipenyeza dola 160,000 za Marekani kwa Waislamu wenye msimamo mkali wamuue Gaddafi. Shayler alipotaka kuzungumza katika TV kuhusu ukweli wa ‘ajali’ ya Princess Diana, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Robin Cook, alimzuia. Baadaye Shayler alikamatwa mjini Paris na kupelekwa London, Uingereza.

Chanzo kingine kinadai kuwa MI6 ilipanga kumuua aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia, Slobodan Milosevic, mwaka 1992 kwa ajali ya gari. Waliposhindwa, walitumia mabomu ya NATO mwaka 1999. Kama ni kweli walipanga mauaji ya wakuu wa nchi, sembuse Diana?

Chanzo muhimu cha Serikali ya Ufaransa kililiambia jarida The People (Nov. 9 1997) kwamba kulikuwa na “…angalau maofisa (majasusi) sita wa MI6 katika Ubalozi wa Uingereza mjini Paris mwisho wa juma lile la kifo cha Diana …angalau ofisa mmoja kati ya hao alionekana akiwafuatilia Diana na Dodi baada ya kuwasili kutoka katika mapumziko huko Sardinia.”

Gazeti Daily Mail (Des. 4, 2004) la Uingereza lilifichua kuwa dereva Henri Paul, ambaye naye alifariki katika ajali, alikuwa akilipwa na MI6. Upo hapo? Hii ilijulikana wakati wa upelelezi wa kamishina wa Scotland Yard, Sir John Stevens. Lakini Stevens alikumbana na vikwazo kwa sababu kuhoji maofisa wa MI6 kulihitaji kwanza ridhaa ya mkuu wa MI6, John Scarlett.

Mwaka 2003, Paul Burrell, aliyekuwa mtumishi wa Princess Diana na rafiki yake mkubwa, alisema miezi kumi kabla ya ‘ajali’ hiyo alipata barua kutoka kwa Diana ikisema kuwa kulikuwa na njama za kumuua kwa ajali ya gari.

“Kipindi hiki cha maisha yangu ni cha hatari sana kwangu,” barua hiyo ilisema na kudai kuwa hatari kubwa ni kwamba “Prince Charles anaandaa ‘ajali’ katika gari langu, …”

Kama MI6 walimuua Diana, basi walitumwa, na kama ndivyo, waliwashirikisha wenzao wa Ufaransa. Lakini ikiwa walikula njama ya kumuua Diana, wangepata faida gani kutokana na kifo chake? Yako mengi, lakini tazama haya mawili tu.

Kwanza, Princess Diana alikuwa tayari ameanza kuwa mtu hatari kwa familia ya Ufalme wa Uingereza kwa sababu alijua siri nyingi sana za familia hiyo na alikuwa ameshaanza kuzianika.

Pili, “Serikali ya Uingereza haikuweza kuvumilia wazo la kwamba Diana—akiwa katika mapenzi na Mwislamu wa Misri—angeweza kubadili dini na kuwa Mwislamu, kwa hiyo ilibidi aondoke…” (Independent on Sunday, Okt. 12, 1997).

Pengine haya si mambo muhimu ya kuandika, lakini tunajua kuwa yanatuathiri sote. Pengine tungezingatia hoja na mambo mengi kuhusu kifo cha Diana, hitimisho letu lisingekuwa hivi: “Kwa vyovyote kifo cha Princess Diana ni ajali iliyotokana na Mungu.”

Mwanadamu Aliyepuuzwa


MWANADAMU ALIYEPUUZWA NA MAPINDUZI YA ZANZIBAR







Na William Shao

USIKU wa Jumamosi kuamkia Jumapili, Januari 11-12, 1964, kulitokea mapinduzi yaliuouondoa madarakani utawala wa Kisultani katika visiwa vya Zanzibar.

Ingawa huo ni ukweli wa kihistoria, ile sehemu ya historia inayozungumzia Mapinduzi ya Zanzibar imembagua mwanadamu mmoja tu muhimu sana ambaye ndiye hasa aliyefanya mapinduzi hayo—‘Field Marshal’ John Okello.

Marejeo mengi yanaonyesha kuwa aliyefanya Mapinduzi ya Zanzibar ni raia wa Uganda aliyeitwa John Okello aliyekuwa Unguja, na wala si Abeid Karume, ingawa Karume hatimaye alitokea kuwa Rais wa Zanzibar mara baada ya mapinduzi.

Inaelekea kuna mambo yaliyofichwa katika historia hiyo. Swali ni kwanini hata yafichwe? Hata kama Okello hakufanya mapinduzi hayo, kwanini hatajwi na wanahistoria wengi wa Tanzania kuwa alihusika, au angalau tu kushiriki, katika mapinduzi hayo? Historia ya Zanzibar inasababisha maswali mengi kuliko majibu.

Wanasiasa wengi—hasa wale Zanzibar—wanasema John Okello siye aliyefanya Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini baadhi yao wanashindwa kukanusha kuwa Okello alikuwa Zanzibar wakati wa Mapinduzi hayo yakifanyika.

Miongoni mwa waliokana ukweli huo ni Hayati Khamis Daruwesh. Hata hivyo na yeye alikiri kuwa John Okello alikuwa na “…mvuto" huko Zanzibar (rejea RAI, Aprili 14—20, 2005).

Hata hivyo, katika picha ya pamoja ambayo ‘wanamapinduzi’ walipiga Jumatatu ya Januari 12, 1964, Okello anaonekana amekaa mkao wa kiongozi mbele ya wengine, tena akiwa amezungukwa na wanachama wa Baraza la Mapinduzi walioshiriki katika mapinduzi hayo.

Miongoni mwa wote hao ni yeye peke yake anaonekana tofauti kabisa na wengine wote akiwa amevalia nguo ama za kijeshi au za polisi. Wengine wote wamevalia nguo za kawaida tu.

Wengine katika picha hiyo ni pamoja na Yusuf Himid, Said Abdallah Natepe, Ramadhan Haji, Said Buvai, Said wa Shoto, Muhammed Abdallah, Pili Hamis, Hamis Darwesh, Khamis Hemed, Hafiz Suleiman na Hamid Ameir.

Ni watu watatu tu walikuwa wamepewa viti na kukaa mbele ya wengine. Wengine wote, akiwemo Daruwesh mwenyewe, walisimama nyuma ya Okello, na katikati ya wote hao ndipo alipokaa “Jemadari Mkuu” John Okello.

Ingawa wanajitahidi kuficha kuhusika kwa Okello katika mapinduzi ya Zanzibar, historia inasimama kama shahidi. Gazeti Tanganyika Standard (Jan. 13, 1964), katika ukurasa wake wa mbele liliandika hivi: “Wapigania uhuru waliokuwa na silaha wamekitwaa kisiwa cha Zanzibar.

“Wamekamata majengo yote muhimu ya serikali kwa muda usiozidi saa 24 …usiku kiongozi wa mapinduzi alitangaza muundo wa serikali mpya ya ‘Jamhuri ya Zanzibar na Pemba’ Sheikh Karume akiwa kama Rais na Bw. Kassim Hanga kama Waziri Mkuu…”

Watu hawa waliopewa uongozi wa nchi—Karume, Hanga na baadhi ya wengine—hawakuwa Unguja wakati Okello akitaja vyeo vyao. Walikuwa wamekimbilia Dar es Salaam kujificha, wakihofia kuwa ikiwa mapinduzi yangeshindwa wangekamatwa na kutiwa kizuizini.

Gazeti hilo liliandika kuwa mtangazaji huyo ni “kiongozi wa mapinduzi” na kwamba ndiye “alitangaza muundo wa serikali mpya ya ‘Jamhuri ya Zanzibar na Pemba’.”

Kwa namna Okello alivyopanga mapinduzi hayo na kuyafanikisha, walioyashuhudia na walioyasikia yalivyofanyika hawakuamini kama kweli mtu huyo alikuwa wa kawaida. Maswali mengi kumhusu Okello yalianza kuulizwa. Wengine walidhani kuwa aliwahi kupata mafunzo ya kijeshi katika Uchina au Cuba.

Maswali na uvumi wa aina hiyo ulisambaa sana kila kona kiasi cha kulisukuma gazeti Tanganyika Standard kwenda kumuuliza maswali hayo. Baadaye gazeti hilo liliripoti hivi: “Field Marshal John Okello leo amesema yeye ni mtu thabiti wa mapinduzi ya Zanzibar na ni yeye aliyemteua Sheikh Abeid Karume kuwa Rais. Kiongozi huyo wa maasi mwenye umri wa miaka 27, …amesema anachoitakia Zanzibar ni ‘demokrasia na uhuru’.

“Field Marshal amefanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari katika ofisi za kurushia matangazo ya redio ambazo zilikuwa zimechukuliwa kama makao makuu mapya ya Serikali. Lundo la bastola aina ya .22 lilikuwa mbele ya meza yake. Walinzi waliokuwa na bastola na bunduki mbalimbali walisimama kumzunguka.

“Kiongozi huyu wa waasi aliye mfupi amesema hakuwahi kuwa na mafunzo yoyote yanayohusiana na uasi nje ya nchi na kukanusha taarifa kuwa aliwahi kwenda Cuba au Peking (China). Alisema alipanga kuiangusha Serikali ya Zanzibar akisaidiana na Kamati Kuu yake ya watu waliopewa siku 14 tu ya mafunzo msituni…”

Hiyo ni sehemu tu ya taarifa iliyotolewa na chombo cha Serikali ya Tanganyika—Tanganyika Standard. Taarifa hiyo haimtaji Karume kama mwanamapinduzi, bali John Okello.

Tanganyika Standard haikutoa kielelezo chochote kinachodokeza kwamba Abeid Karume au mtu mwingie yeyote, isipokuwa Okello, ndiye aliyefanya mapinduzi ya Zanzibar. Kwamba Karume ndiye kiongozi wa Mapinduzi ni historia iliyogeuzwa baada ya John Okello kufanyiwa njama za kumwondosha Zanzibar.

Ingawa historia inaonesha kuwa John Okello alihusika sana na Mapinduzi ya Zanzibar kuliko Mzanzibari au Mtanzania yeyote—awe Sheikh Karume, Thabit Kombo, Kassim Hanga, Abdulrahman Babu au Mwalimu Julius Nyerere—hapewi sifa hiyo, angalau hata kutajwa tu kwamba alikuwepo Zanzibar wakati mapinduzi hayo yanafanyika, hata kama hakushiriki katika kufanya mapinduzi.

Wala hatamkwi kwamba yeye ndiye aliyetangaza ushindi. Hakuna kumbukumbu za kihistoria zilizoachwa kwa ajili ya vizazi vya baada ya mwaka 1964 zinazotosha kuvihamasisha kuvutiwa na mambo ya Okello. Habari zake zinaepukwa hata wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi Zanzibar inayojulikana kama ‘Januari 12’.

Madai kwamba “Mapinduzi ya Zanzibar ni mapinduzi ya Okello” yalichapishwa pia na gazeti la chama cha TANU, The Nationalist & Freedom (Jan. 12, 1965), mwaka mmoja barabara baada ya kufanyika kwa mapinduzi hayo.

Magazeti mengi ya ndani na nje ya Tanganyika, hususan The Standard la Tanganyika, yaliyochapishwa katika siku zile ambazo mapinduzi yalifanyika, yaliandika sana kuhusu habari za Okello na jinsi alivyofanya mapinduzi hayo.

Pamoja na hayo, nadharia nyingine—ambazo hazina uhakika wa kihistoria—zinadai kwamba kiongozi na mwanamapinduzi wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar aliuawa mwanzoni kabisa mwa mapinduzi hayo na hivyo Okello akatwaa usukani wa kuendesha Mapinduzi.

Ingawa nadharia hiyo inakataa kwamba Okello hakuwa kiongozi wa mapinduzi hayo tangu pale mwanzoni, angalau inakubali kuwa alishiriki mapinduzi hayo na hata akawa kiongozi wake baada ya “kiongozi na mwanamapinduzi wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar” kuuawa mwanzoni kabisa mwa mapinduzi hayo.

Nadharia hiyo inajaribu kukataa kwamba Okello hakuwa kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar, lakini inashindwa kumkana. Ikiwa kiongozi na mwanamapinduzi wa kweli aliuawa mwanzoni kabisa mwa mapambano, basi hakuwa mpambanaji mzuri.

Lakini yule aliyechukua usukani na kuendeleza mapambano hadi kufanikisha lengo lake, huyo ndiye anayepaswa kuwa mpambanaji na mwanamapinduzi wa kweli.

Ni nani mshindi wa kweli wa mapinduzi kati ya kiongozi aliyeanzisha mapambano na kisha akauawa mwanzoni mwa mapambano hayo na yule aliyepokea usukani akapambana hadi mwisho na kupata ushindi?

Hata kama itakubalika kwamba Okello hakuwa kiongozi wa mapinduzi pale mwanzoni, inaeleweka kuwa anayepata ushindi ndiye mshindi. Haijulikani ni nani aliyetengeneza nadharia hiyo ya udanganyifu na, la maana zaidi, haijulikani kwanini nadharia hiyo ikatengenezwa na ni kwa maslahi ya nani.

Magazeti ya The Standard na The Nationalist & Freedom lililozinduliwa na Mwalimu Julius Nyerere Alhamisi ya Aprili 16, 1964, yaliripoti sana habari za Okello na jinsi alivyoshiriki kikamilifu katika Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika habari zote kuhusu jambo hilo katika kipindi cha mwanzo cha 1964, magazeti hayo hayakueleza kama kulikuwa na kiongozi wa mapinduzi aliyeuawa na, kama matokeo ya kuuawa huko, Okello akachukua usukani.

Lakini iliwashangaza wasomaji wengi madai hayo yalipotolewa mwaka mmoja baadaye kwamba Okello hakuwa kiongozi, bali alichukua uongozi baada ya kiongozi wa kweli wa mapinduzi hayo kuuawa katika mapigano.

Mwandishi Keith Kyle wa Uingereza aliyeandika makala mbili tofauti kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar katika matoleo mawili tofauti ya gazeti The Spectator, alikuwa sahihi kwa sababu alichoandika kinafanana na maelezo mengi yaliyoonekana katika machapisho mengine ya ndani na nje katika kipindi cha Januari na Februari 1964.

Zaidi ya hilo, mwandishi Kyle alikuwepo Zanzibar wakati wa matukio ya Januari 11-12, 1964, akithibitisha kushiriki kwa Okello katika Mapinduzi ya Zanzibar. Imani ya Kyle inadokeza kuwa matangazo ya redio yaliyotolewa na Okello mara tu baada ya Mapinduzi na habari nyingine kumhusu mwanamapinduzi huyo zinathibitisha kuwa alishiriki moja kwa moja katika Mapinduzi hayo.

Baada ya kukidhibiti kisiwa cha Unguja, John Okello alimwalika Abeid Karume kurudi Zanzibar kuchukua nafasi ya Urais,” kinasema Wikipedia Encyclopedia. Kinaongeza kusema hivi: “(Abeid) Karume hakuwa Zanzibar usiku ule Mapinduzi yalipofanyika.”

Michael F. Lofchie, katika kitabu chake, Was Okello's Revolution a Conspiracy? © 1967 (uk. 36-42), aliandika hivi: “…Okello alifanya Mapinduzi ya Zanzibar…” Lakini anaongeza kuandika: “Njama za kumwondoa Zanzibar ni za kuficha ukweli unaochukiza...”

Okello ameelezwa sana katika kitabu Revolution in Zanzibar (1967) kilichochapishwa mjini Nairobi. Alitajwa sana katika gazeti The Standard la Tanganyika/Tanzania kwamba yeye ndiye aliyefanya mapinduzi katika Zanzibar.

Hata waliokuwa viongozi wa serikali ya Sultani wanakiri ukweli kwamba Okello ndiye aliyefanya mapinduzi na wala si Karume. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Sultani, Ali Muhsin Ali Barwan, ambaye alikuwa Zanzibar wakati serikali yake ikipinduliwa, Jumanne ya Oktoba 21, 1997, akiwa Dubai katika Falme za Kiarabu, aliukiri ukweli huo.

Alisema: “…John Okello, askari mamluki, aliongoza mauaji ya kinyama, …watu 12,000 walichinjwa. Lakini msingi wenyewe uliwekwa mwaka 1957 wakati vyama vya Shirazi Association na African Association vilipoungana na kuunda Muungano wa Afro-Shirazi chini ya ushawishi na uongozi wa Julius Nyerere.” (kitabu Conflicts and Harmony in Zanzibar © 1997)

Kwa wale wasiotaka kupotosha mambo wanakiri kwamba Abeid Karume hakufanya mapinduzi kama inavyodaiwa, bali ni Okello akisaidiwa na baadhi ya wale aliowaita ‘wapigania uhuru.’

Kitabu Mwalimu: The Influence of Nyerere © 1995 (uk. 172), kinasema: “Uhuru wa Zanzibar ulipatikana (Alhamisi ya) Desemba 10, 1963, sultan akiwa Mkuu wa Nchi (Zanzibar) na kupewa mamlaka ya kumteua mrithi wake …Ndani ya majuma matano tu Serikali hiyo na mtawala wake walipinduliwa na ‘masiha mjinga’ ambaye ni kiongozi wa wanaharakati, John Okello. Baada ya kipindi kifupi cha vurumai na mauaji, Okello alisimika Baraza la Mapinduzi chini ya uongozi wa (Sheikh Abeid) Karume.”

Hayo yaliandikwa na Profesa Haroub Othman ambaye ni mtaalam wa mambo ya siasa za ulimwengu na Mzanzibari anayejua mambo mengi kuhusu historia ya visiwa hivyo. Lakini kinachotatiza ni kwanini Okello hatajwi kabisa wakati suala la Mapinduzi ya Zanzibar linapozungumzwa?

Hata hivyo, jarida la African Studies Review, katika pitio lake la vitabu la Septemba 2003 ambalo Jennifer Betowt alikifanyia kitabu Revolution in Zanzibar: An American's Cold War Tale, alidai kuwa habari nyingi kuhusu Okello hazina uhakika.

Gazeti lichapishwalo mjini London, Uingereza, The Spectator (Feb. 7, 1964) chini ya makala Gideon’s Voice, pamoja na lile la (Feb. 14, 1964), chini ya makala How it Happened, linaelezea kuhusika moja kwa moja kwa Okello katika Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika magazeti hayo Okello anafafanuliwa kuwa mhusika mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar, na kwamba yeye ndiye aliyewavuta wengine wote waliokuja kushirikiana naye katika kufanya mapinduzi hayo.

Majira ya saa moja asubuhi ya Jumapili ya Januari 12, Okello alianza kutoa moja ya matangazo yanayojulikana Zanzibar kuwa ni mabaya zaidi. Hapa ndipo Okello alipotamka kwa mara ya kwanza kabisa kuwa yeye ni "Field Marshal wa Wapigania Uhuru." Awali hakutaja jina lake, lakini saa chache baadaye alitamka jina lake likitanguliwa na cheo alichojipachika — Field Marshal John Okello. (Gazeti Tanganyika Standard, Jan. 13, 1964)

Akitumia jina lake kupitia matangazo ya redio, mchana wa siku hiyo Okello, akitumia redio, alisema: “Amkeni ninyi mnaojiita wafalme, hakuna tena serikali ya kifalme katika kisiwa hiki. Sasa hii ni serikali ya wapigania uhuru. Amkeni nyie watu weusi, na kila mmoja wenu abebe bunduki na zana za vita na kuanza kupigana.”

Baada ya kuridhika na mipango yake, mchana wa Januari 12, 1964, Okello alitangaza jamhuri—Jamhuri ya Zanzibar—yeye mwenyewe akajitangaza kama “Waziri wa Ulinzi na Utangazaji na Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi.”

Sheikh Abeid Karume alitangazwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Kassim Hanga akatangazwa kuwa Makamu wa Rais, na Abdulrahman Babu pamoja na viongozi wengine wa ASP wakawa mawaziri katika serikali mpya.

Aboud Jumbe alitengewa nafasi ya uongozi. Alipewa Uwaziri wa Afya na Huduma za Jamii. Othman Sharif aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu; Hasnu Makame, Waziri wa Kilimo; Idris Abdul Wakil, Waziri wa Biashara na Abdulrahman Babu, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Katika matangazo mengine ya redio, Okello alimteua tena Hasnu Makame kuwa Waziri wa Fedha na Saleh Sadalla kuwa Waziri wa Kilimo.

Siku iliyofuatia, Jumatatu ya Januari 13, Okello, akiwa ameshika hatamu za serikali ya Zanzibar na kuwateua mawaziri wake, (rejea magazeti ya Tanganyika Standard, Jan. 14, 1964) alikuwa na kukurukakara nyingi.

Alionekana akipita hapa na pale kama mtu aliyekuwa akitafuta jambo fulani asilipate. Mipango yake ilikuwa haijamalizika, badala yake ilizidi kuwa mingi. Aliwateua maofisa wengine zaidi wa serikali yake, wengi wao wakiwa ni wahamiaji wa kutoka bara waliohamia Unguja siku za karibuni.

Baada ya kupanga safu ya serikali yake huku watu wengi kisiwani Unguja na duniani kwa ujumla wakiwa hawajawa na uhakika wa kitakachotokea baadaye, sauti ya Okello ilisikika redioni ikisema: “...Serikali sasa inaendeshwa nasi—Jeshi. Ni juu ya kila raia, mweusi, maji ya kunde au mweupe, kutii amri. Ukiwa mkaidi au kudharau amri, nitachukua hatua kali mara 88 zaidi ya hatua nilizochukua sasa hivi (kuangusha serikali ya Sultan).

Vitisho na uwezo wake wa kuvitekeleza viliwashtua sana raia wengi. Kesho yake, Jumanne, Januari 14, 1964, alitoa tangazo lingine lililokuwa na maneno makali hata zaidi. Alisema:

"Huyu ni Field Marshall (Jemadari Mkuu) wa Zanzibar na Pemba …Ninafikiria kwenda (kijiji cha) Mtendeni kukiangamiza ikiwa watu wa huko hawataki kutii amri. Baada ya dakika 40 nitakuja kuwamaliza nyiye wote, hasa Wacomoro.”

Huyu ni mwanadamu ambaye waliosikia habari zake na yale aliyoyafanya huko Zanzibar wanashangaa ni kwanini hatamkwi kabisa katika historia ya Zanzibar. Lakini kwa waliosoma kazi za Michael Lofchie, hasa kitabu chake, Was Okello's Revolution a Conspiracy? hawatashangaa kusoma kwamba “Njama za kumwondoa Zanzibar ni za kuficha ukweli unaochukiza...”

********************************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754 989 837. E-mail: shao2020@yahoo.co.uk., Blog: willyshao.blogspot.com.
********************************************************

Unajimu na Sayansi



KUNA UHUSIANO WOWOTE KATI YA SAYANSI NA UNAJIMU?




Na William Shao

MAMILIONI ya watu hutafuta ushauri kutokana na mambo ya nyota kila siku duniani. Je, unajimu ni sayansi—au angalau una uhusiano wowote na sayansi? Kuna uhusiano wowote wa kweli kati ya nyota na maisha ya binadamu ya kila siku? Ikiwa kuna uhusiano wowote wa kweli, binadamu huathirika jinsi gani kutokana na unajimu huo? Nyota hutimiza makusudi gani? Inawezekana kwa vyovyote kwa nyota kuongoza maisha ya watu?

Kwa kutazama matukio ya kidini na kijamii, unajimu unao historia ndefu tangu mwanzo mdogo kabisa wa historia ya mwanadamu.

Haishangazi kwamba watu wengi hupendezwa sana na wakati wao ujao na wakati ujao wa wenzao, hasa wanapofikiria kutukia kwa matukio yanayovuta sana fikra zao kama vile kuzuka na kumalizika kwa Vita Kuu I na II ya Dunia, kuzama meli ya Titanic Aprili 1912 na MV. Bukoba Mei 1996 na matetemeko ya ardhi pamoja na matatizo mengine ya kawaida lakini yanayosumbua maisha ya watu ya kila siku pamoja na mambo yanayohusiana na maisha hayo.

Kulingana na ripoti moja kutoka Chuo Kikuu cha Hamburg ambayo ilichapishwa katika gazeti ‘International Herald Tribune’, “…1992 ulikuwa ni mwaka wa ugomvi zaidi kuliko mwaka mwingine wowote katika karne ya 20 …ulikuwa na vita vingi mahali pengi duniani kuliko wakati mwingine wowote katika historia.”

Ingawa vita hivyo vinavyotajwa na gazeti hilo havikuwa na uzito ule ule uliokuwa wa Vita Kuu I na II ya dunia, kwa takwimu za kawaida tu, viligharimu idadi kubwa zaidi ya maisha ya watu na mali kwa kipindi cha mwaka mmoja tu ikilinganishwa na Vita Kuu II. Hakuna aliyetazamia hivyo.

Kwa hakika, ulikuwa ni mwaka wa peke yake ambao wanajimu hawakuweza kuuona kabla ya hapo. Kitabu ‘Britanicca Book of the Year’ (1993), katika utangulizi wake, kinasema: “Ni mwaka uliokuwa na zaidi ya vita 52 vya silaha kali katika nchi tofauti-tofauti…” na mamilioni ya watu walikufa kutokana na athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na vita hivyo.

Basi, kutokana na hali hiyo, wale wapenda amani wamekuwa wakijiuliza “ni wapi tunapoweza kupata uthabiti, amani na utulivu?” Hata wale wasio wapenda amani, lakini wanaojali sana wakati ujao wa maisha yao na wa maisha ya wenzao pia, wamevutwa sana na unajimu na kuutegemea kwa utabiri wake.

Wao wanaona kuwa kupata amani, uthabiti na utulivu wa maisha yao ni kujua wazi mambo yajayo. Hata kama si kujua mambo ya wakati ujao ulioko mbali sana, basi angalau ule wakati ujao ulio karibu zaidi, hata kama chache tu zijazo.

Kukosa uhakika juu ya matukio ya wakati ujao ndiko kulikosababisha kuvuma sana kwa aina mbalimbali za utabiri ambazo nyingine hudaiwa kuwa ni sayansi. Na kwa kuwa watu wengi wanapenda kujua mambo yao ya wakati ujao, basi watabiri (wa kweli au wa uongo) hupewa aina fulani ya heshima ya pekee. Katika mambo ya utabiri, labda unajimu ndiyo aina inayojulikana zaidi ya utabiri siku hizi.

Kitabu ‘The International Encyclopedia of Astronomy’, kinasema: “Katika China ya kale …ishara za angani na vilevile misiba ya asili zilifikiriwa kuwa zilionyesha matendo mazuri na hodari na matendo mabaya ya Maliki na serikali yake."

Kulingana na kitabu hicho, unajimu, ambao ni tofauti na elimu ya sayansi ya nyota (astronomy), ni “…kufanya uaguzi juu ya athari ambazo nyota na sayari nyingine hudhaniwa kuwa nazo juu ya maisha ya binadamu ambayo ni matukio yaliyo nje ya uwezo wake kwa kutegemea mahali nyota hizo zilipo na jinsi zilivyokaa kuhusiana na jua.” Leo, mamilioni ya watu wanashindwa kujizuia kusoma falaki (maarifa ya kubahatisha matukio kulingana na elim ya nyota) ili kupata madokezo ya wakati wao ujao.

Maeneo mengine ambamo wanajimu hudai kwamba huwa wanatabiri wakati ujao ni pamoja na matokeo magumu ya ndoa, matatizo ya afya, kuinuka na kuanguka kwa viongozi wa kisiasa, tarehe nzuri kabisa ya kufungua biashara mpya au kufunga biashara ya zamani pamoja na tarakimu za kutumia ili kushinda mchezo wa bahati nasibu au mchezo mwingine wowote.

Hata hivyo, kitabu ‘New Catholic Encyclopedia’ kinasema kwamba “unajimu ulitumiwa zamani na Papa Julius II [1503-13] ili kupanga siku ya kutawazwa kwake na ukatumia na Papa Paul III [1534-49] kuamua wakati halisi wa kuitisha Mkutano wa Kuzungumzia Masuala Mazito.”

Kitabu ‘The Thunder of Stars’ kimeandika kuhusu Bw. Alfred Hug ambaye ni mkurugenzi wa shirika moja la Uswisi ambalo mara nyingi hutumia unajimu kuwashauri watu wanaoweka akiba katika soko la hisa. Mnajimu huyo huwathibitishia watu mafanikio. Yeye Hug, alipoulizwa kuhusu utabiri anaofanya, alisema, “hayo yameandikwa katika nyota.”

Jambo la wazi ni kwamba wengi huhisi kwamba nyota huathiri maisha yao. Tofauti na inavyofikiriwa, mazoea ya kutazama nyota si mapya. Kitabu ‘The World Book Encyclopedia’ kinadokeza hivi: “Maelfu ya miaka iliyopita wakulima walizitazama nyota kujua wakati wa kupanda mimea yao. Wasafiri (nao) walijifunza namna ya kutumia nyota ili kuelewa upande wa kuelekea.”

Kulingana na mfululizo wa vitabu vya kujifunza Kiarabu, ‘Arabic by Radio’, baharia maarufu wa Oman, Ibn Majid, aliongoza chombo baharini kwa kuangalia nyota. Inasemekana kuwa huyu Majid aliwaongoza Wareno, akiwemo Vasco da Gama, kwa kutumia nyota (unajimu) kuja Afrika Mashariki kufanya ziara zao za upelelezi.

Hata hivyo, kwa kuzitazama zikiwa angani, idadi na ukubwa wa nyota ni mambo yanayoweza kushangaza sana. Inakadiriwa kuwa kuna makundi makubwa sana ya nyota (galaxy) kiasi cha bilioni 10 angani, kinasema kitabu ‘Encyclopedia Britanicca’.

Kitabu cha ‘International Encyclopedia of Astronomy’ kinasema: “…Hiyo ndiyo hesabu ya punje ndogo sana ambazo zingeweza kuingizwa katika jumba kubwa sana la wastani …Galaxy mojawapo ambayo mfumo wetu wa jua ni sehemu yake, inakadiriwa kuwa na angalau nyota nyingi kadiri hiyo.”

“…Nyota iliyo karibu zaidi na Dunia (ukiondoa jua), ambayo ni ya kikundi cha ‘Alpha Centauri’, iko umbali ambao mwanga unaoingia ndani ya jicho la binadamu unakuwa umetoka katika nyota hiyo kwa miaka 4.3 ukiwa bado unasafiri kwa mwendo wa kilomita 299,792 kwa sekunde moja (sawa na kilomita milioni 1,079.25 kwa saa moja).” Hata hivyo, kulingana na kitabu hicho, hiyo ni ile nyota iliyo karibu zaidi tu.

Nyota nyingine ziko mbali zaidi. Umbo kama nyota ambalo liko karibu zaidi na dunia ni mwezi, ambao, nao umetajwa mara kadhaa kuwa unahusiana na mawimbi ya bahari kwa namna fulani.

Mwezi huo huwa na athari ya wazi juu ya dunia yetu, “…hata uvutano wake husababisha tofauti ya zaidi ya mita 15 kati ya kujaa na kupwa kwa bahari mahali fulani-fulani,” chasema kitabu ‘International Encyclopedia of Astronomy’.

Kulingana na wanasayansi watatu wa Ufaransa, ingawa walionesha wasiwasi fulani ambao haukuwa dhahiri, wakati fulani waliliambia gazeti la ‘Nature’ (Feb. 18, 1993) hivi: “Uvutano wa mwezi sasa (kwa dunia) ndio unaoweka ‘mwinamo’ wa dunia katika ‘mlalo’ wa nyuzi (degree) 23,” na hivyo kuhakikisha kuna badiliko la kawaida la majira (ya mwaka).

Ripoti moja kutoka katika Kituo cha Utafiti wa Kisayansi cha Taifa cha Ufaransa (CNRS) sasa kinathibitisha kwamba mwezi una matokeo kama hayo juu ya uso wa ardhi ya dunia.

Kwa njia ya chombo cha uchunguzi kilichowekwa kwenye dimbwi la maji ya chumvi katika pango lililozibwa lililoko meta 1,000 (kilometa moja) chini ya ardhi, watafiti waliweza kugundua hali ya kuinuka na kuanguka kwa vitu vilivyokuwamo ndani ya pango hilo saa 12.

Mwendo huo, ulisababishwa na kupanuka na kusongamana kwa kuta za pango hilo. Kulingana na mwendo wa mwezi kuzunguka dunia nao huthibitissha kwamba kwelikweli mwezi ndio chanzo cha kile ambacho wataalamu katika kituo hicho cha CNRS hukiita "kupumua kwenye kushangaza chini ya ardhi."

Sasa, kufikia hapo, wale ambao walipata kuyajua hayo, walianza kujiuliza hivi: “Kwa kuwa mwezi una athari nyingi kiasi hicho juu ya sayari (dunia) yetu, ni namna gani basi yale mabilioni ya nyota?

Na kama kila nyota ina athari zake kwa dunia, kutakuwapo na mabilioni mangapi ya athari? Ndipo wengine wakaamua kwamba kwa kuwa hivyo ndivyo mambo yalivyo, kama mwezi huiathiri dunia, basi si tu kwamba nyota nazo huathiri dunia tu, lakini pia hata kile kinachohusiana na dunia hiyo.

Hata hivyo, mwandishi mmoja, Edwin Way Teale, katika kitabu chake ‘When Were You Born’, aliandika: “Nyota zisizo na uhai zinaweza kutuambia jambo fulani ikiwa tuko tayari kuzisikiliza, lakini si wakati tusipotaka kuzisikiliza …Nyota zinasema juu ya udhaifu wa binadamu katika muda fulani wa wakati.”

Mwanastronomia wa Ujerumani aliyeishi kati ya mwaka 1571-1630 alisema “unajimu ni kitu cha ziada tu (kisicho na ulazima wowote) na kishiriki cha astronomia.”

Mwanachuo mmoja wa Kiyahudi aliyeishi Enzi za Kati kati ya mwaka 1135-1204, Moses Maimonides, kwa mujibu wa kitabu ‘Guide for the Perplexed’, aliliona hilo kwa njai nyingine. Alisema: “Unajimu ni ugonjwa, si sayansi …Ni namna ya mti ambao chini ya kivuli chake namna zote za ushirikina na washirikina hushamiri.”

C. A. Ronan, ambaye ni mratibu wa mradi wa Historia ya Sayansi ya Asia Mashariki, Cambridge, Uingereza na mchangiaji wa habari katika kitabu ‘The International Encyclopedia of Astronomy’, alisema hivi:

“Sayansi ya kizamani ambayo hudai kwamba inaweza kukadiria utu na mwenendo wa mtu na kutabiri mwelekeo na matukio ya wakati ujao kutokana na jinsi maumbo ya sayari zilivyokaa mbinguni …labda katika karne ya sita—Wakaldayo walioishi kusini mwa Iraq hufikiriwa kuwa ndio walioanzisha falaki (maarifa ya kubahatisha matukio kulingana na elimu ya nyota). Hiyo ilihusiana na athari zilizosababishwa wakati wa kuzaliwa na nyota zilizokaa mahali pamoja, na pia Jua, Mwezi na Sayari tano.

“…Taratibu za unajimu na ule utaratibu wa kufasiri wa falaki hutegemea mawazo ambayo wanaastronomia na wengi wa wanasayansi wengine huyaona kuwa ni ya watu binafsi na yasiyokubalika.”

Katika kitabu hicho, Ronan aliyetajwa hapo juu anaeleza kwamba ingawa akili za watu wa nchi za Magharibi huchukulia kwamba ile sayari nyekundu inahusiana na vita na hali ya kutaka ugomvi, kwa Wachina, wekundu ni rangi ya bahati, na hutiliwa maanani kuwa ni ishara ya wema.”

Tofauti na hivyo, hadithi za Magharibi huihusisha Zuhura weupe pamoja na uzuri au bahati. Kwa Wachina, kulingana na kitabu ‘The International Encyclopedia of Astronomy’, rangi nyeupe huchukuliwa kuwa ni rangi ya kifo, misiba na maangamizi” na hivyo wao huitaja Zuhura kuwa ni “ile sayari ya ugizagiza na vita.”

Ronan anaendelea kusema kwamba “ingawa unajimu una asili ya sayansi ya kizamani, katika nyakati za mapema ulishiriki sehemu iliyokuwa na mafanikio sana katika kuendeleza astronomia na kuandaa fedha za kuutekeleza.”

Kitabu ‘The World Book Encyclopedia’ kinasema washindi 19 wa Tuzo la Nobel, pamoja na wanasayansi wengine, katika mwaka 1975 walitoa tangazo rasmi lililokuwa na kichwa cha habari ‘Kukanusha Unajimu—Taarifa ya Wanasayansi Mashuhuri 192’. Taaarifa hiyo lilitangaza hivi: “Katika nyakati za kale watu hawakuwa na wazo lolote juu ya umbali mkubwa sana uliopo kutoka duniani hadi kwenye zile sayari na nyota.

“…Kwa kuwa sasa umbali huo unaweza kuhesabiwa na tayari umeshahesabiwa na unaendelea kuwa rahisi zaidi kuhesabiwa, tunaweza kuona jinsi zilivyo ndogo sana zile nguvu za uvutano na matokeo mengine yanayosababishwa na hizo sayari za mbali na nyota zilizo mbali hata zaidi.

“…Ni kosa kuwazia kwamba athari za nyota na sayari wakati wa kuzaliwa zinaweza kwa njia yoyote na kwa vyovyote kuamua mapema, kubashiri na hata kujua nyakati zetu zijazo zitakavyokuwa.”

Mwanzoni mwa mwaka 1993, Shirika la Utafiti wa Kisayansi wa Mambo Yasiyojulikana na Sayansi nchini Ujerumani lilikusanya utabiri 70 uliofanywa na wanajimu kisha likakadiria matokeo mwishoni mwa mwaka.

“Walisema uongo mtupu,” likaripoti jarida ‘New Scientist’, likimkariri msemaji mmoja wa shirika hilo. “Wanajimu wengi hawaamini hata utabiri wao wenyewe.”

Wanasayansi wanaonyesha kwamba kama kweli nyota zilizo katika mbingu zinakuwa na matokeo yoyote juu ya watu mmoja mmoja, matokeo hayo ni kidogo sana. Kwa hakika, wazo lenyewe ambalo lilitegemewa ili kuanzisha unajimu, la kwamba dunia ndiyo mahali pa katikati pa ulimwengu mzima, na kwamba jua na sayari zinazunguka-zunguka dunia, “limethibitishwa na sayansi kuwa ni la uongo,” kikasema kitabu cha ‘The Encarta Encyclopedia Delux Edition’.

Ingawa kuna mashaka juu ya kama kutabiri mambo ya kutazama nyota kunasaidia, mtu anaposoma safu zinazohusu kutazama nyota, ana hatari ya kupoteza uwezo wa kufanya maamuzi ya maana, au kama vile mtaalam wa kuchunguza nyota, Roger Culver alivyoeleza: “Hatari ni kwamba unaweza kujiondolea lawama na kusema nyota ndizo zilizokufanya utende vile.”

Ni kweli kwamba huenda mtu akasoma safu kama hizo kwa makusudi ya kujifurahisha tu, lakini, kwa mfano, tukio fulani maishani mwake linalingana bila kutazamiwa na jambo alilosoma katika maelezo ya nyota hizo, anaweza kushawishika bila kutambua na kumfanya aamini kwamba kuna ukweli fulani katika utabiri wa nyota hizo, na hatimaye atashawishiwa zaidi kujiingiza katika unajimu.

Ikiwa ndivyo, jambo fulani lililo zito zaidi linaweza kutukia. Jambo lililoanza kama hamu tu ya kutaka kujua jinsi mambo yalivyo lingeweza kugeuka liwe mazoea yanayokuwa na nguvu zaidi ya mambo mengine ya maana zaidi.

Katika jarida ‘Nature/Science Annual’, Dk. Alan Rosenburg, daktari wa magonjwa ya akili, aliandika: “Watu wamevurugika mawazo. Wanataka msaada wa kufanya maamuzi yanayohusu pesa, uhusiano wao na watu wengine na kazi ya kuajiriwa.

“Dini haitimizi haja zao hizo kama ilivyokuwa zamani, na udaktari wa magonjwa ya akili unapungukiwa katika mambo fulani. Kwa hiyo …wakiwa katika jaribio la kutaka kushikamana na jambo linaloonekana kuwa na uwezekano wa kisayansi, wao wanazidi kugeukiwa wanajimu kwa wingi kutatua matatizo yao…”

Katika hatua moja, Halmashauri ya Uchunguzi wa Kisayansi ya Madai ya Maajabu ya Visivyoonekana nchini Marekani, Novemba 16, 1984 ilidokeza kwamba “matabiri yanayofuata ya unajimu yapaswa kusomwa kwa faida za kujifurahisha tu. Matabiri hayo hayana msingi wa kutegemeka wenye ukweli wa kisayansi.”

Vita fupi zaidi



VITA FUPI ZAIDI YA MAPINDUZI DUNIANI, JANUARU 12, 1964

Na William Shao


KISICHOJULIKANA sana katika historia hadi karne ya 20 ni kwamba vita vifupi zaidi vya mapinduzi ni vile vya Zanzibar vilivyodumu kwa saa chache tu na hatimaye kufanikisha lengo lake. Hayo yalitokea usiku wa kuamkia Januari 12 1964.

Hali ya kisiasa Zanzibar ilikuwa ikizorota tangu kifo cha Sultani Khalifa kilichotokea Oktoba 9, 1960. Khalifa alikuwa ameitawala Zanzibar kama Sultan tangu Desemba 9, 1911.

Chaguzi za mseto zilipofanyika mwaka 1961, vyama vikuu vya Zanzibar, kila kimoja, vilishindwa kujipatia wingi wa kura. Hatimaye, mwaka 1963, Waingereza waliondoa majeshi yao. Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar Desemba 10, 1963, aliashiria kuondoka kwa Gavana wa mwisho wa Kiingereza huko Zanzibar, na huo ukawa mwisho wa ukoloni wa Uingereza.

Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa 1963 ulikipa ushindi finyu muungano wa vyama viwili ZNP na ZPPP. Lakini taifa hilo lililokuwa mwanchana kamili wa Jumuia ya madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.

Mashambulizi ya kuipindua Serikali ya Sultan yalianza Januari 11 kuamkia Januari 12, 1964. Yalianza Jengo la polisi la Ziwani kwa ukataji wa nyaya za seng’enge. Ingawa baadhi yao waasi walianza kuogopa walipoanza kukata nyaya hizo, walipeana moyo kwamba ikiwa hili lingeshindwa, wangekamatwa na kuuawa.

Ilikuwa ni bora zaidi kwao kufa katika mapambano kuliko kushindwa kisha wakauawa na serikali. Kwa hiyo, walielezana kuwa ni afadhali kuhakikisha kuwa hili linafanikwa ama kwa kufa au kwa kupona kuliko kuacha lishindwe halafu tuuawe.

Askari wa zamu waliokuwa wakilinda kituo hicho walishtuka. Wakaanza kujibu mashambulizi mazito yaliyoelekezwa kwao. Mlango wa mbele ulifunguliwa, lakini wakati huo askari wa serikali ambao walikuwa wamelala ghorofani katika jengo hilo waliamka ghafla na kuteremka haraka haraka.

Kiasi cha askari 40 wa serikali walishambuliana na askari wa wanamapinduzi, ambao wengi wao walikuwa wakitumia pinde na mishale pamoja na mawe ili kuwazuia polisi hao wasiteremke kutoka ghorofani wakati wengine wakivunja ghala la silaha.

Bunduki aliyoichukua kiongozi wa mapinduzi hayo, John Okello, kutoka kwa askari mmoja aliyekuwa zamu kituoni hapo ilikuwa imebakiwa na risasi tatu tu, na hiyo ndiyo iliyokuwa silaha ya kwanza ya kisasa waliyokuwa nayo katika Mapinduzi yao, na ilikuwa muhimu mno kwa sababu iliwapa faida katika zile dakika chache za kwanza.

Katika hali ya kuchanganyikiwa, polisi walianza kubonyeza ving’ora na kupiga tarumbeta na kuwarushia waasi mabomu ya kutoa machozi. Lakini kwa kuwa kundi la Okello lilikuwa na askari ambao waliwahi kufanya kazi katika baadhi ya vituo hivyo, waliweza kukata nyaya za ving’ora hivyo na kuvinyamazisha. Waliweza pia kukabiliana na mabomu ya machozi kwa kuyasokotea katika mashati yao na kuwarushia polisi hao.

Kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo, Okello aliipiga risasi tarumbeta iliyokuwa ikipulizwa na mmoja wa polisi hao, ikaanguka sakafuni. Wakitumia mashoka, nyundo, mapanga na vifaa vingine vya kuvunjia nyumba, hatimaye askari wa Okello walifanikiwa kuvunja ghala la silaha.

Mpaka walipovunja ghala hilo, nusu ya wale polisi 40 walikuwa ama wameuawa au wamejeruhiwa na waliobakia walilazimika kujisalimisha hata kabla silaha na zana nyingine za kivita hazijaanza kugawanywa askari wa Okello kutoka ghalani.

Kikosi cha wapiganaji 200 cha serikali kiliwasili katika eneo hilo saa 10:30 usiku, lakini baada ya mapigano ya saa nzima hakikufua dafu. Ilipofika saa 11:30 asubuhi wengi wa wapiganaji wa serikali walikuwa tayari wameuawa, wangine wakiwa wamejeruhiwa na wengi walikimbia.

Okello alidai kuwa Ziwani lilikuwa ni eneo la kwanza kutekwa, lakini kuna waandishi walioandika kuwa Mtoni ndilo eneo la kwanza kutekwa. Baada ya kituo cha Polisi cha Mtoni kutekwa, ambacho hakikuwa na ulinzi mkali kama kile cha Ziwani, askari wa Okello walikamata bunduki 200 za kawaida, Sub Machine-Gun 20, mabomu ya kutupwa kwa mkono pamoja na mabomu ya kutoa machozi.

Ingawa Haji alijeruhiwa wakati wa utekaji wa kituo hicho, alituma ujumbe wa mafanikio na hongera kwa Okello ambaye alitembelea kituo hicho cha polisi kabla hajaenda katika kituo cha redio ambako alimkuta fundi mitambo wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akijiandaa kutoa matangazo yake na kumlazimisha kwa mtutu wa bunduki kutangaza aliyotaka yeye (Okello) yatangazwe.

Kukamatwa kwa kituo cha redio kulikofanywa Mzee Mohamed na kundi lake la askari 100 waliounda kundi la pili, ‘2nd Battalion’, kulikuwa ni kwa mafanikio makubwa. Wanamapinduzi sasa wangeweza kutangaza mapinduzi yao. Sasa wangeweza kuiambia dunia kuwa wamekwishateka nchi. Njia pekee ya matangazo ambayo serikali ilikuwa imebakiwa nayo ni simu.

Katika kituo cha Polisi cha Ziwani ndipo palikuwa na ghala za silaha za polisi. Kwa mujibu wa kitabu Conflict and Harmony in Zanzibar, polisi wa zamu walikuwa na bunduki na kila moja ilikuwa na risasi tano.

Wakati fulani usiku wa manane Mrakibu wa Polisi, Durham, ambaye alikuwa Mwingereza, aliwapitia walinzi hao, akachukua risasi za walinzi hao na kuziweka kwenye kikapu alichoondoka nacho.

Ali Muhsin, katika kitabu hicho, anadai kuwa muda mfupi baadaye kituo cha Polisi Ziwani kilianza kushambuliwa kwa mishale na bunduki, na ghala lake la silaha likavunjwa.

Baadhi ya askari waliokuwa na bunduki, lakini hawakuwa na risasi, waliuawa, na wengine wakakimbilia vichakani. Muhsin anadai kwamba mmoja wa askari hao, ambaye alikuwa akifanya kazi ya kumpelekea habari, walitiwa pamoja kizuizini huko Dodoma.

Anadai kwamba hata polisi wengine waliokuwa kituo cha Ziwani walimwambia habari hizo hizo na kwamba maofisa wote wa polisi wa Kiingereza waliondoka na familia zao kutoka katika kituo cha Ziwani bila kuguswa, wakati polisi wa Unguja wakichinjwa.

“Kweli kweli katika muda wote wa ‘mapinduzi’ ambao maelfu ya watu weusi na watu wa rangi ya kahawia wakiuawa, kulemazwa na kubakwa, watu wa rangi nyeupe hawakuguswa,” alidai Muhsin.

Majira ya saa moja asubuhi ya Jumapili, Januari 12, Okello alianza kutoa moja ya matangazo yake. Aliwatisha Waarabu. Alisema: “Amkeni ninyi mnaojiita wafalme, hakuna tena serikali ya kifalme katika kisiwa hiki. Sasa hii ni serikali ya wapigania uhuru. Amkeni nyie watu weusi, na kila mmoja wenu abebe bunduki na zana za vita na kuanza kupigana.”

Baada ya kutangaza hivyo John Okello aliondoka katika studio za redio kisha akaenda katika gereza la Mazizini akiwa na kundi lenye silaha walizokamata kutoka katika maghala ya polisi na kuamuru mashambulizi yafanyike majira ya saa nne asubuhi.

Matokeo ya mashambulizi hayo ni kwamba katika muda usiozidi dakika 30 wapiganaji wa Okello waliyakamata majengo yote ya gereza hilo, baadhi ya majengo mengine yalichomwa moto.

Hakukuwa na upinzani mkubwa. Walinzi wa gereza hilo walikuwa na silaha lakini hazikuwasaidia sana. Wakati hili likitokea Mazizini, Okello alipata habari kwamba Waarabu wa Kimanga wameanza kuwaua Waafrika katika maeneo ya vijijini, kwa hiyo aliwagawanya wapiganaji wake kwenda kuwashambulia Wamanga hao na wengine wote waliobakia katika kituo cha polisi cha Malindi.

Baadhi ya wafuasi wa Okello walianza kuteka nyara maduka ya Wahindi na Waarabu katika eneo la Darajani na kwingineko. Katika maeneo kadhaa watu walikuwa wakiuawa ovyo. Waingereza hawakuwa wakiuawa kama Waarabu, lakini walikuwa wakipigwa kwa mawe.

Saa moja asubuhi Sultan alipanga safari ya haraka ya kuondoka Zanzibar. Alitumia meli ya serikali iliyojulikana kwa jina la Salama iliyokuwa imetia nanga bandarini. Muda mfupi baadaye aliwasili bandarini tayari kuondoka, huku akiwa chini ya ulinzi mkali ukiwa katika msafara wa magari matatu.

Maofisa wa Uingereza waliwashauri mawaziri wa serikali ya Zanzibar pia waondoke Unguja kwa kutumia meli hiyo kwa usalama wa maisha yao na kwamba wangeweza kurejea Unguja wakitokea Pemba ambako wangeweza kupokelewa vizuri na kupanga mikakati kamambe ya kurejea madarakani.

Mawaziri hao walikataa, na ilionekana kana kwamba mawaziri wengine walitaka kujaribu kufanya mashauriano na mapatano na waasi walioiangusha serikali yao kutoka walikokuwa. Wengine hawakutaka kuondoka kwa sababu waliogopa kuondoka katika maeneo walimokuwa wamejificha.

Baadhi waliomba hifadhi katika Ubalozi wa Uingereza; wengine, kama Ali Muhsin (Waziri wa Mambo ya Nje) na Juma Aley (Waziri wa Maendeleo ya Fedha) walijaribu kwenda katika vituo vya polisi ambavyo vilikuwa havijatekwa bado, lakini wasiwasi uliwafanya washindwe kutekeleza uamuzi huo.

Wakati hali ya kisiasa Unguja imechafuka, mapema asubuhi Sheikh Abeid Amani Karume aliamshwa nyumbani kwake Miembelado na kundi la askari wa Okello. Alileta ubishi kidogo, lakini alizidiwa nguvu na shuruti ya askari hao.

Walimtaka aondoke Unguja haraka iwezekanavyo. Kisha wakampakia katika jahazi lililompeleka Dar es Salaam. Sababu za kuondolewa kwa Karume Unguja kwa lazima na kutakiwa kwenda Dar es Salaam zilielezwa na wafuasi wa Okello kuwa “...ni usalama wake ikiwa mapinduzi yangeshindwa” au ikiwa Waarabu wangewazidi maarifa.

Karume alijikuta amefikishwa Dar es Salaam huku akiwa amechanganyikiwa kutokana na hali iliyotokea Zanzibar. Mwingine aliyekuwa amechanganyikiwa sawasawa na Karume ni Kassim Hanga na Abdulrahman Babu ambao tayari walikuwa wamewasili Dar es Salaam.

Othman Sharif naye alifanyiwa kama Karume alivyofanywa—kuamshwa mapema asubuhi. Aliamshwa asubuhi na wanaume wawili, mmoja akiwa na bunduki na mwingine akiwa na mishale na upinde.

Lakini, tofauti na Karume, badala ya kusafirishwa kwenda nje ya Unguja, aliambiwa asiongee lolote kwa muda wa saa kadhaa, lakini aliamriwa kuwaonesha wanaume hao mahali wanapoishi mafundi mitambo wa redio. Viongozi wengine wa ASP walifichwa mahali ambako walilindwa na wanamapinduzi mpaka mwisho wa maasi.

Wakati huo huo, aliposikia milio ya kwanza ya bunduki, Smithyan, Katibu wa Kudumu Katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alijaribu kutambua ni kitu gani kilichokuwa kikitokea.

Alijaribu kumweka katika hali ya tahadhari ofisa wa Kiingereza katika serikali ya Zanzibar, H. Hawker, ambaye naye alimtahadharisha Balozi wa Uingereza aliyekuwa Unguja, Tim Crosthwait.

Ingawa kituo cha redio kilikuwa tayari kimetekwa, mawasiliano ya simu yalikuwa bado yanafanya kazi muda wote wakati mapinduzi yakifanyika. Mpaka jioni ya siku hiyo, Januari 12, mfumo wa mawasiliano usiotumia waya wa uwanja wa ndege ulikuwa ukifanya kazi pia.

Kwa kupitia uwanja wa ndege, nchi za nje zilikuwa zikijulishwa mambo yaliyokuwa yakitendeka Zanzibar kwa wakati huo, na misaada kadhaa iliombwa kukabiliana na waasi. Meli moja ya jeshi la maji iliyojulikana The Owen, ilitumwa kutoka Uingereza kwenda Zanzibar kufanya kazi ya uokozi, lakini ilikuja kuwaokoa raia wa Uingereza na wala si kukabiliana na waasi.

Baada ya kuona hakuna msaada wa ziada unaokuja, Smithyan aliona kuwa makao yake hayakaliki, hivyo saa mbili asubuhi aliondoka katika himaya yake. Baada ya kukabidhi madaraka kwa Hawker ambaye alikuwa akiwasiliana na mawaziri wa Sultan, Smithyan, kwa usalama wake aliogelea baharini kutoka ufukweni hadi alipofanikiwa kuingia katika meli iliyoitwa Salama.

Hawker alifanya mpango wa kurejeshwa kwa meli kubwa ya serikali iliyoitwa ‘Seyyid Khalifa’ ambayo kwa wakati huo ilikuwa Tanga. Lakini meli hiyo iliwasili Zanzibar jioni ya Januari 12.

Wakati Shamte Hamadi, Juma Aley na Muhsin wakiwa katika Kituo cha Polisi cha Malindi kabla hakujapambazuka, kwa kushauriwa na Kamishna wa Polisi, J. M. Sullivan, walijaribu kuomba msaada kutoka kwa jeshi la Uingereza lililokuwa Kenya. Lakini ombi lao halikufanikiwa.

Ilipofika jioni, huku hali ikiwa ya kutatanisha, Waarabu wa Kimanga walikuwa wakitafuta hifadhi katika vituo vya polisi ambavyo vilikuwa havijatekwa bado. Wanamapinduzi walimtumia ujumbe ofisa mmoja wa Kitengo Maalum cha Polisi aliyekuwa akishirikiana nao amshawishi Sullivan aondoke ili waweze kuteka maeneo yote ya Ziwani.

Mashambulizi katika kituo cha Polisi cha Malindi yalifanywa mchana wa kati ya saa saba na saa nane huku yakishuhudiwa na makundi makubwa ya watu. Baada ya matukio mengi ya kisiasa na kijeshi, na baada ya kujaribu kufa na kupona kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na wanaharakati ambao sasa walikuwa wameweka kituo chao eneo la Raha Leo, Sullivan aliwakusanya watu wake waliomtii—weupe kwa weusi—katika kundi moja na kuwapeleka bandarini.

Kutoka hapo walivushwa kwenye maji hadi ilipokuwa meli ya Salama na wengine, baadaye, wakapakiwa katika meli ya Seyyid Khalifa na kisha wakapelekwa Dar es Salaam. Baadhi ya hawa walirejea Zanzibar baadaye, ambapo wengine walikamatwa na kutiwa ndani.

Huku mfumo wa serikali ya Zanzibar ukiporomoka zaidi, na taarifa kuhusu waliouawa na majeruhi zikitolewa, na kutokuwa na idadi isiyoaminika ya askari, Sullivan alikuwa katika hali ngumu ya kuamua mambo.

Kisio la polisi waliouawa au kujeruhiwa katika mashambulizi siku hiyo walidaiwa kufikia 300, lakini inawezekana idadi ilikuwa ndogo zaidi ya hiyo kutokana na polisi wengine kukimbia wakati mashambulizi yalipokuwa makali na hivyo kuhesabiwa kama ama walijeruhiwa au kuuawa.

Upinzani ulikuwa mkubwa zaidi katika eneo la kituo cha polisi cha Mjini kilichokuwa chini ya ofisa wa Kiarabu aliyejulikana sana kwa jina moja la Sketi, ambaye mapema alikuwa ameteuliwa na Shamte kuwa Msaidizi wa Kamishna wa Polisi. Sketi aliuawa kwa kukatakatwa kwa mapanga na mashoka na kundi lililounga mkono wanaharakati wa mapinduzi.

Ilipofika jioni ya Januari 12, 1964 hakukuwa na upinzani wowote dhidi ya wanamapinduzi mjini Unguja, ingawa kulikuwa na milio ya risasi na mauaji kadhaa yaliyoripotiwa kuendelea kufanyika katika maeneo ya vijijini kwa muda fulani hadi jua lilipozama, hususan maeneo ya Bumbwini kaskazini ambako Waarabu waliokuwa na silaha waliendelea kuwafyatulia watu risasi kwa saa kadhaa. Vikundi vingine vya Waarabu viliendelea kupigana katika maeneo ya Nungwe na Bububu hadi waliposhindwa na wanaharakati na kuuawa kwa kuchinjwa mithili ya wanyama machinjoni.

Huo ukawa mwisho wa Serikali ya Sultan iliyodumu Zanzibar kwa zaidi ya karne moja. Sultan wa kwanza wa Zanzibar alikuwa Majid bin Said (1856–1870). Kisha wengine waliofuata ni pamoja na Barghash bin Said (1870–1888), Khalifah bin Said (1888–1890), Ali bin Said (1890–1893), Hamad bin Thuwaini (1893–1896), Khalid bin Barghash (1896).

Wengine ni Hamud bin Muhammed (1896–1902), Ali bin Hamud (1902–1911), (alijiuzulu), Khalifa bin Harub (1911–1960), Abdullah bin Khalifa (1960–1963) na hatimaye akaja Jamshid bin Abdullah (1963–1964) ambaye alipinduliwa Januari 12, 1964.


Penye ukweli, uongo hujitenga



PENYE UKWELI, UONGO HUJITENGA



Na William Shao



“Nawaandikia makala hii wale wanaoheshimu Maandiko Matakatifu ya Biblia.” Ndivyo alivyoanza kuandika msomaji aitwate Innocent R. Mutahyabarwa katika gazeti la RAI (Novemba 23-29, uk. 20).



Nimependa changamoto yake, lakini hakukumbuka kuwa tafsiri anazotumia kimsingi zinamtatiza yeye mwenyewe na kutatiza wengine. Kuna mambo mengi ambayo ama anaficha kwa makusudi au hayajui kwa ‘maasumu’ kama jina lake linavyofasiriwa kwa Kiswahili.



Kwa kuwa kujibu yote aliyoandika katika makala hiyo ni sawa na kuandika kitabu kizima, kupoteza wakati na kujaza nafasi gazetini, nitataja machache sana kwa uchache sana, kisha wasomaji wa RAI ninaoamini wamefunguka bongo zao wataamua kama majibu hayo ni halali au la.



Ingawa Innocent hakukosea katika kila sentensi, amekosea katika kila aya aliyoandika. Kwanza hakuna kitu duniani kinachoitwa ‘Maandiko Matakatifu ya Biblia’. Biblia yenyewe ndiyo inayoitwa Maandiko Matakatifu.



Hilo ni kosa lililoonekana katika sentensi yake ya kwanza katika aya ya kwanza ya makala yake. Labda alitaka kusema Biblia Takatifu, ambayo hutafsiriwa kama Maandiko Matakatifu.



Biblia yenyewe, hasa Union Version na King James Version, inajitafsiri hivi: hii ni “Maandiko Matakatifu ya Mungu yaitwayo Biblia, yaani Agani Jipya na Agano la Kale.” Kutamka “Maandiko Matakatifu ya Biblia” ni sawa na kusema “Biblia ya Biblia, au Maandiko Matakatifu ya Maandiko Matakatifu”.



Kitabu kinachofuatwa na Wakritso ni Maandiko Matakatifu ‘yaitwayo’ Biblia na wala si Maandiko Matakatifu ‘ya’ Biblia. Innocent amekosea katika sentensi ya kwanza ya makala yake kama alivyokosea karibu kila sentensi ya katika kila aya.



Innocent aliandika kuwa “Biblia huweza kunukuliwa na yeyote, hata shetani.” Kwa hili nakubaliana naye, kwamba hata shetani anaweza kuinukuu Biblia, ili mradi hakuniita shetani. Lakini amesema “Mwandishi Shao anaichukulia juu juu Biblia.”



Katika aya nyingine aliandika, “Kuna vitabu vingine ambavyo wamejiandikia wapotoshaji wa Ukristo anavyotaka mwandishi (Shao) tuvisome. Vitabu hivyo siyo vitabu vya historia halisi ya Kanisa Katoliki.”



Alitaka kumaanisha nini? Kwamba ni vitabu vya historia ya Kanisa Katoliki ni kwa vile tu siyo vitabu “halisi”? Ni kweli kwamba vitabu nilivyonukuu katika kitabu changu, MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA, siyo vitabu ‘halisi’ vya historia ya Kanisa Katoliki.



Innocent anataka kuwaambia wasomaji wake kuwa kitabu kikishakuwa cha historia ya Kanisa Katoliki ni kitakatifu na kwamba hakipotoshi, hakiwezi kukosewa na mwandishi wake na ni kitakatifu—au pengine ni zaidi ya wanadamu?



Hata hivyo, ukweli ni kwamba Biblia siyo kitabu cha historia ya Kanisa Katoliki—iwe ni historia halisi au isiyo halisi. Hakuna mahali popote katika Biblia palipo na neno ‘Katoliki’ au ‘Ukatoliki’. Hicho ni kitabu kinachotumiwa na Wakatoliki, lakini si cha Kikatoliki. Ni kitabu cha Kikristo.



Kuna Biblia za Kikatoliki, ambazo zimetafsiriwa na Wakatoliki kutoka katika Biblia halisi. Mojawapo ni Biblia ya Douay, au Douay-Rheims, ambayo tafsiri yake ilikamilika kati ya mwaka 1582 na 1609.



Ingawa kuna hoja nyingi za kumjibu, nianzie pale ninapoichukulia Biblia kijuu juu na yeye anapoichukulia kwa uzito. Tuache kutumia nukuu yoyote katika kitabu chochote kisichohusiana na “historia halisi ya Kanisa Katoliki”. Tuchukulie kwamba Biblia inahusiana na Kanisa Katoliki, madhali wanaikubali.



Innocent alisahau kwamba katika sentensi ya mwisho ya aya ya sita ya makala yake hiyo alidai hivi: “Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja.” Hapo alitamka ukweli usioweza kupingwa.



Ni kweli Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja. Je, makasisi wa Kikatoliki siyo Wakristo? Kama Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, mbona mapadri, ambao ni Wakristo, hawafungi ndoa? Au angalau ndoa ya mke mmoja?



Haya ni maswali yanayotokana na hoja ya Innocent. Pengine alijisahau tena alipoandika: “Kama mnavyoelewa Wakatoliki wote ni mapadri.” Nani anayeelewa? Ni rahisi kumwelewa? Tazama sentensi zake: “Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, … Wakatoliki wote ni mapadri.”



Ukizitumbukiza sentensi hizo katika mantiki zitakataa. Kama Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, na kama Wakatoliki wote ni mapadri, kwanini mapadri hawafungi ndoa? Kama mapadri hawafungi ndoa kamwe, na kama Mkristo anafunga ndoa ya mke mmoja, ni rahisi kuhitimisha kimantiki kuwa mapadri siyo Wakristo(?)



Innocent anaonyesha kudai kwamba Biblia inaunga mkono makasisi kutooa. Sikuona mahali popote katika Biblia panaposema hivyo. Yeye anasema: “Na hata tukimsoma 1 Wakorintho 7:7…,” kana kwamba mstari huo unaunga mkono padri kutooa.



Tuanzie hapa. Ni kweli kwamba Biblia inasema: “...Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendeje Bwana; bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.” (1Wakorintho 7:32,33).



Sentensi hiyo ndiyo inayotumika kama kigezo? Kama hivyo ndivyo, hiyo haijaelezwa kuwa ni lazima, bali ni hiari tu.



Kwa kuonyesha tu kwamba hilo ni pendekezo, Biblia inasema hivi: “Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia ... Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi, ... Lakini mtu awaye yote akiona ya kuwa hamtendei mwanamwali wake vipendezavyo, na ikiwa huyo amepita uzuri wa ujana wake, na ikiwapo haja, basi, afanye apendavyo, hatendi dhambi; na awaruhusu waoane.” (1 Wakorintho 7:28, 35, 36). Huko ni kusoma Biblia kijuu juu?



Yesu mwenyewe, wakati akijibu maswali ya Mafarisayo, alisema: “…Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si mwili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” Mathayo 19:4-6.



Lakini katika Biblia, ndoa huchukuliwa na kuheshimiwa kama zawadi safi na takatifu kutoka kwa Mungu. Na Mungu huzibariki ndoa kuwa ni kitu chema, kama ilivyoelezwa hapo juu kutoka katika kitabu cha Mithali 18:22, kwamba: “Apataye Mke apata kitu chema; naye ajipatia kibali kwa Bwana.” Kwa kutumia mantiki hii, mapadri hawana kitu chema, wala kibali kutoka kwa Bwana?



Zaidi ya hilo, inaelezwa kuwa ni “afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwezake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kimwinua” (Mhubiri 4:9, 10) Ndiyo maana kuna mapadri wengi huanguka katika zinaa na wala hawana wa kuwainua wala wa kuwazuia wasiangukie tena huko.



Mungu alipomuumba mwanadamu wa kwanza ambaye alikuwa mwanaume, hakukusudia aendelee kuishi peke yake. Ingawa alikuwa akimtafutia mwenza wake, hakumletea mwanaume mwenzake, bali alimtengenezea mwanamke----mke wake.



Baada ya kumuumba mwanadamu katika Bustani ya Edeni, “Bwana Mungu akasema, Si vyema mtu huyo awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye … na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.



“Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu ... kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” (Mwanzo 2:18, 22-24).



Mtume Petro na baadhi ya watumishi wengine wa Mungu waliokubaliwa na waliokuwa na nyadhifa na mamlaka katika kazi za Kikristo siku za mwanzo za Ukristo walikuwa ni wanaume waliofunga ndoa.



Walikuwa na wake na familia zao. Hawa walikuwa ni Wakristo halisi kuliko Wakristo wengine, au wote, wa siku hizi. Mungu aliwakataa watu hao kwa sababu ya kuoa kwao?



Biblia inasema: “Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.” (Mathayo 8:14) Haiwezekani Petro akawa na mkwe na wakati huo huo asiwe ameoa mke. Hata mitume nao walikuwa wameoa. Hawakulazimishwa kuwa waseja ili waweze kushiriki katika kazi zao za utume.


Kitabu cha Matendo 21:8-9 kinasimulia hivi: “Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake. Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.” Je, mtumishi huyo alikuwa na mabinti aliowapata kutoka wapi kama hakuwa na mke aliyemzalia watoto hao kupitia njia ya ngono?


Ingawa Kanisa Katoliki ndilo linalosisitiza makasisi wake wasioe, ukweli wa kihistoria ni kwamba kuna mapapa waliokuwa wameoa—nasema mapapa, si makasisi wa kawaida au viongozi wa kanisa Katoliki wa vyeo vya chini. Na hawa walikubaliwa na kanisa.


Hata wale ambao hawajaoa wana mahawara, vimada na watoto waliozaa kwa siri. (tazama kitabu changu, MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA). Kitabu hicho kinawataja mapapa waliooa, idadi ya watoto waliozaa na hata watoto wa mapapa ambao nao walitawazwa kuwa mapapa kama baba zao.


Innocent, unaweza kusema ni kwanini kuna papa waliokuwa wameoa? Kwanini hatimaye wakaamua mapadri wasioe tena baada ya karne nyingi baada ya Kristo? Mapapa hawa hawakulijua neno la Mungu?


Mwaka 1967, Papa Paul VI (1897-1978)—au kama ndugu na rafiki zake wa eneo la Concesio, Italia walivyomjua, Giovanni Battista Montini, kwa mujibu wa jarida la Kikatoliki, ‘Priestly Celibacy’ (la Ijumaa ya Juni 23, 1967), alikiri hivi:


“Agano Jipya ambalo ndilo hutoa mafundisho ya Kristo na Mitume wake …halidai useja wa kushurutishwa kwa wahudumu wa kanisa …Yesu mwenyewe hakuweka jambo hilo kama sharti la kuwachagua Mitume wake Kumi na Wawili, wala Mitume walioongoza Ukristo katika zile siku za mwanzo hawakuwalazimisha watu wasioe ili wawe watumishi …Agano Jipya …halilazimishi useja kwa wahudumu wa makanisa.”


Hata hivyo, maelekezo ya mtume Paulo kwa Timotheo juu ya kuwekwa rasmi kuwa waangalizi wa Wakristo, au mapadri, au maaskofu, hudhihirisha jambo hili: “Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha ... mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu ... Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.” (1 Timotheo 3:2, 4, 11).


Hayo ni masharti yaliyotajwa na Mtume Paulo, lakini katika masharti hayo yote yaliyotolewa katika kitabu cha Timotheo, ingawa hakuna hata moja linalomlazimisha askofu kuoa, hakuna hata moja linalomkataza asioe kwa ajili ya utumishi wake akiwa katika cheo cho chote cha utumishi wa kanisa katika Ukristo.


Mtume Paulo alionyesha tu kwamba ‘askofu’ hapaswi kuoa wake wengi, lakini haikudokezwa popote katika Biblia kwamba hapaswi kuoa kamwe.


Anawajibika awe mume wa mke mmoja, na wake zao wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. Ikiwa amefunga ndoa, anapaswa kuwa na mke mmoja tu----wala si kutooa kamwe.


Sehemu ya Waraka wa Kwanza wa Paulo Mtume kwa Wakorintho unasomeka hivi: “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karamu yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane. Ni heri wakae kama mimi nilivyo.” (1 Wakorintho 7:7, 8).


Je, hilo ndilo neno linalochukuliwa kama chanzo cha useja katika nyadhifa za Kanisa? Huenda. Lakini Kanisa halijaitamka waziwazi. Na kama linachukuliwa hivyo, ni kwanini jambo la kutooa linasisitiziwa makasisi peke yao lakini lisisisitizwe kwa “wale wasiooa bado, na wajane” kama Biblia inavyosema?


Apendalo Mtume Paulo halijaelekezwa kwa makasisi, bali ni kwa wasiooa bado na wajane. “Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo.” (1 Wakorintho 7:8). Walioambiwa wakae kama Mtume Paulo alivyo ni wale wasiooa bado, na wajane, lakini si makasisi.


Hata kama walioambiwa maneno hayo ni makasisi, pale mwanzoni mtume Paulo aliwaambia Wakorintho hivi: “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. (1Wakorintho 7:1-2).


Mstari wa tisa anasema, “Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” Ni kweli kwamba mapadri hawagusi wanawake? Hawawaki tamaa? Hawazini? Vyovyote iwavyo, hata kama hawawaki tamaa au hawazini, katika Maandiko Matakatifu haijasemwa kwamba hiyo ilikuwa amri. Ni pendekezo tu.


“Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.” (1 Wakorintho 7:6). Hakuna amri iliyotolewa. Ilikuwa ni idhini tu—au pendekezo tu. Ikiwa Biblia inatoa idhini tu, “...si kwa amri.” Hiari hiyo haikutolewa kwa makasisi, bali ni wale wasiooa bado na wajane.


Kwanini leo Makanisa yanatoa amri, si kwa idhini? Kwanini yanatoa amri ambayo Biblia haijatoa? Wao walizipata wapi amri hizo? Amri zenyewe zinatimiza kusudi gani? Je, wao ni matowashi?


Biblia imezungumzia hali hiyo. Inasema kuwa wanaume na wanawake fulani huchagua useja kwa hiari zao wenyewe, na ingefaa useja uchaguliwe kwa “idhini..., si kwa amri.” (1Wakorintho 7:6).


“Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; (kama ilivyoelezwa hapo juu kuhusu nchi ya India) tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” (Mathayo 19:12).


Labda Innocent atuambie kuwa mapadri ni matowashi kwa maana ya neno ‘towashi’. Hata hivyo, katika Biblia, neno ‘towashi’ halijapewa uzito wa upadri. Neno hilo, ambalo kwa Kiingereza ni ‘eunuch’, limeonekana mara 19 tu katika Biblia.


Limeonekana mara kadhaa katika vitabu kadhaa vya Biblia. Katika kitabu cha Esta (5), Isaya (2), Daniel (1), Mathayo (5), Yeremia (1) na Matendo (5). Kufikia hapo nafunga mjadala. Kwa wasomaji wa RAI, ambao ni wasomaji makini, wachambue hoja hizo waamue kama ni halali au si halali.


William Shao ni mwandishi wa kitabu kiitwacho MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA na mwandishi wa habari wa HABARI CORPORATION LTD. Anapatikana kupitia 0754-989837, shao2020@yahoo.co.uk.

Rudi Nyuma