WANAOTAKA KUONA YALIYOFICHIKA WATAYAONA
William ShaoNILIPOANDIKA makala niliyoiita “
Ukweli Kuhusu Septemba 11” na kutaja ‘muujiza’ wa Septemba 11, au namba 11, au 911 (nine-eleven), kuna walionipigia simu wakisema niliyoandika hayakuwa na umuhimu wowote kwa sababu mambo mengi yanayotokea duniani hutokana na historia kujirudia.
Kuna usemi usemao “historia hujirudia yenyewe”. Ni kweli kwamba historia huwa ikijirudia yenyewe? Ukweli ni kwamba kuna matukio yanayofanana na yale yaliyowahi kutukia siku za nyuma.
Hata hivyo, matukio mengi hayatokei kwa njia ile ile. Kutukia tena kwa jambo fulani hakumaanishi kwamba historia imejirudia, bali ni jambo lingine linalofanana na lililowahi kutukia awali.
Historia ni elimu maalum inayohusiana na matukio na mambo yaliyopita. Kwa hiyo ni vigumu—na pengine haiwezekani—kutabiri kwa uhakika mambo ya wakati ujao kwa kutegemea mambo yaliyopita.
Kutokana na ukweli huo, ikiwa kuna jambo lolote tunaloweza kujifunza kutokana na historia ni kwamba hakuna jambo lolote tunaloweza kujifunza kutokana na historia. Ni vigumu kutabiri yatakayotokea kwa kutegemea historia.
Je, tunakubali kwa urahisi tu kwamba kwa vile ujenzi wa jengo la
The Pentagon la Marekani (makao makuu ya Jeshi la Dunia?) ulianza rasmi Septemba 11, 1941 na hatimaye jengo hilo hilo ‘likashambuliwa na magaidi’ Septemba 11, 2001 ni historia ilijirudia?
Tukubali kwamba wakati
Richard Nixon aliyekuwa Rais wa Marekani (1969-1974) Septemba 11, 1972 alipounda jopo la watu wa kuunda mikakati ya kuilinda Marekani dhidi ya ugaidi na hatimaye tarehe kama hiyo hiyo, Septemba 11, 2001, ‘magaidi’ wakaipiga Marekani hiyo hiyo ni historia ilijirudia? Au ni jambo la bahati mbaya?
Tuseme ni jambo la bahati mbaya, au ni kujirudia kwa historia, kwamba kampuni ya ulinzi ya
STRATESEC inayoongozwa na Marvin Bush (ndugu wa Rais Bush) kutangazwa rasmi Septemba 11, 1997 na kupewa ‘tenda’ ya kulinda majengo ya WTC na kisha majengo hayo hayo inayoyalinda yakapigwa na ‘magaidi’ Septemba 11, 2001? Hakuna umuhimu wa kuandika mambo kama hayo?
Kuna mwingine akasema maswali ninayouliza ni ya kitoto. Niliwaandikia wasomaji wa
RAI walio tayari kupokea mawazo au mashauri mapya, watumie akili na busara zao kuitazama changamoto hii.
Tukubaliane kwamba maswali ni mengi sana kuliko majibu katika mambo haya. Kwa watakaofuatilia kwa karibu zaidi mambo yanayotendeka watagundua kuwa ukweli wa mambo ni tofauti sana na jinsi tunavyoambiwa na kutakiwa tuamini.
Duniani kuna mambo yanayotokea kwa bahati mbaya, lakini mengi tunayodhani ni ya bahati mbaya—au ni kujirudia kwa historia—ni mambo yaliyopangwa kutukia. Na mengine yanaruhusiwa yatokee, kama ilivyo kwa tukio la Septemba 11, 2001, au matukio mengine mengi ya Septemba ambayo orodha yake haiwezi kutosha katika toleo moja la gazeti la RAI.
Niliandika nilichoandika katika toleo la
RAI toleo la 686 kuonyesha kuwa kuna kinachoendelea duniani, hasa Marekani, na kisha nimewaachia wasomaji wangu waamue wakitumia udadisi zaidi.
Kwamba napotosha au la si hoja. Tutazame hoja, tusimtazame aliyetoa hoja. Wasomaji wengine wakasema tarehe nilizotaja ni mambo yaliyotukia kulingana na matukio mengine. Waswahili husema ni sadfa.
Wakati mmoja mwanasafu wa gazeti hili, Joseph Mihangwa, alisema “Zanzibar ni shamba la waandishi wa habari.” Nami nilikubaliana naye. Mavuno katika shamba hilo ni mengi, lakini wavunaji ni wachache.
Ukigeukia Marekani si tu shamba la habari kwa waandishi, bali pia ni bahari ya habari. Kama niliyoandika yanatia mashaka, tazama na haya mengine, kisha uamue mwenyewe kama ni bahati mbaya, au ni kujirudia kwa historia, au vinginevyo.
Mambo mengi (si yote) yanayotendeka Marekani yamepangwa na, huenda, yamepangwa karne kadhaa zilizopita na yanaendeshwa na watu maalum. Hawa watu maalum ni pamoja na wale walioanzisha mabenki na mashirika makubwa ya dunia.
Mashirika yao yana alama zao wanazozijua wao kwa wao, na dunia inaambiwa kuwa mashirika hayo ni kwa ajili ya mustakabali mwema wa dunia. Watu hawa, kwa nyakati tofauti, walitofautiana na Marais wawili wa Marekani, John Kennedy na Abraham Lincoln, na baada ya kutofautiana huko, mwisho wa maisha ya Marais hao ulikuja haraka kuliko ulimwengu ulivyotarajia.
Huenda wasomaji wasikubaliane na hilo wakidai kuwa utafiti umepotoka, au umetegemea vyanzo visivyojitosheleza. Lakini tutazame lile tunaloweza kukubaliana, ambalo tunaweza kudai kuwa ni ama sadfa, bahati mbaya au kujirudia kwa historia juu ya
Abraham Lincoln na
John Kennedy.
Abraham Lincoln alichaguliwa kuingia katika Bunge la Marekani mwaka 1846. John F. Kennedy naye alichaguliwa kuingia katika Bunge hilo mwaka 1946. Hiyo ni tofauti ya miaka 100, au tuseme karne moja tangu kutokea kwa tukio moja hadi lingine. Pengine ni historia ilijirudia. Lakini kuna mengi zaidi ya hilo.
Mwaka 1856 Lincoln hakupata kura za kumtosha kupendekezwa kuwa mgombea Urais. Mwaka 1956 Kennedy naye alishindwa kuteuliwa kugombea umakamu wa Rais 1956. Hiyo ni miaka 100 barabara.
Abraham Lincoln alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 1860. John Kennedy akachaguliwa kuwa Rais 1960. Katika mbio za uchaguzi, Lincoln alimshinda Stephen Douglas aliyezaliwa mwaka 1813. Kennedy naye alimshinda Richard Nixon aliyezaliwa 1913.
Wote wawili—Lincoln na Kennedy—walijishughulisha na haki za kiraia, na wote walisomea sheria. Wake zao—Mary Todd Lincoln na Jacqueline Bouvier Kennedy—walifiwa na watoto wakati waume zao wakiwa Ikulu. Mtoto wa Lincoln aliitwa Edward Baker Lincoln aliyefariki mwaka 1846 akiwa na umri wa miaka minme.
Mtoto wa Kennedy, Patrick Bouvier Kennedy, alifariki dunia mwaka 1963 katika muda wa saa 48 tangu alipozaliwa. Watoto wote hao walikuwa wakitumia majina ya koo za mama zao—Bouvier (Kennedy) na Baker (Lincoln).
Wote wawili, Abraham Lincoln na John Kennedy, waliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Ijumaa na walipigwa risasi kichwani. Tofauti ni idadi tu ya risasi zilizopigwa.
Katibu wa Abraham Lincoln aliitwa Kennedy, na katibu wa John Kennedy aliitwa Lincoln. Marais wote wawili waliuawa na watu waliotoka kusini mwa nchi hiyo, na wote, baada ya kuuawa, walirithiwa na watu waliotoka kusini mwa Marekani.
Marais wote wawili, Kennedy na Lincoln, walikuwa na Makamu wa Rais waliokuwa na majina ya ‘Johnson’. Makamu wa Rais wa Lincoln aliitwa Andrew Johnson ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi mwaka 1847. Makamu wa Rais wa Kennedy aliitwa Lyndon Johnson ambaye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi mwaka 1947.
Warithi wao wote (Makamu wao wa Rais) waliitwa Johnson. Andrew Johnson, ambaye alimrithi Lincoln, alizaliwa mwaka 1808. Lyndon Johnson, aliyemrithi Kennedy, alizaliwa mwaka 1908.
John Wilkes Booth, ambaye ndiye muuaji wa Lincoln, alizaliwa mwaka 1838. (si mwaka 1839 kama ilivyodaiwa na masimulizi fulani ya historia). Lee Harvey Oswald, ambaye ‘alimuua’ Kennedy, alizaliwa mwaka 1939. Ni tofauti tu ya mwaka mmoja.
Wauaji wote wawili walijulikana kwa majina yao yote matatu, na majina yao kila mmoja yana herufi 15.
Lincoln alipigwa risasi akiwa katika ukumbi ulioitwa “Ford” kwa heshima ya aliyekuwa mtengenezaji maarufu wa magari duniani aliyeitwa Henry Ford. John Kennedy alipigwa risasi akiwa katika gari lililoitwa "Lincoln" lililotengenezwa na kampuni ya Ford Motor Company iliyomilikiwa na Henry Ford.
Muuaji Booth, baada ya kumuua Lincoln, alikimbia kutoka ukumbini alimofanya mauaji na akakamatiwa katika bohari. Tofauti kidogo na huyo, ‘muuaji’ Oswald alikimbia kutoka katika bohari na kukamatiwa ukumbini. Wauaji wote wawili, Booth na Oswald, waliuawa kabla kesi dhidi yao hazijaanza.
Rais Lincoln alizaliwa Februari 12, 1809 na kufariki Aprili 15, 1865 akiwa na umri wa miaka 56. Rais Kennedy alizaliwa Mei 29, 1917 na kufariki dunia Novemba 22, 1963 akiwa na umri wa miaka 46.
Mwezi mmoja kabla Lincoln hajauawa alikuwa katika eneo linalojulikana kama Monroe lililoko Maryland, Marekani. Kwa upande mwingine, mwezi mmoja kabla John Kennedy hajauawa alionekana akiwa na mchezaji sinema maarufu aliyeitwa Marilyn Monroe, ambaye waandishi wengine wanadai kuwa alikuwa hawara yake.
Sinema peke yake iliyokamilika ambayo inaonyesha mauaji ya John Kennedy ilitengenezwa na mtu aliyeitwa Abraham Zapruder, na maelezo yaliyokamilika yanayoelezea mauaji ya Abraham Lincoln yaliandikwa na mtu aliyeitwa John Zelfindorfer.
Mtoto wa Lincoln aliyeitwa Tad alizikwa Julai 16, 1871. Baadaye maiti ya mtoto huyo ilichimbuliwa kutoka katika kaburi alimozikwa na kupelekwa kuzikwa katika eneo lingine la makaburi.
Mtoto wa John Kennedy, JFK Jr., akirusha angani ndege yake, alitoweka bila kujulikana alikokuwa na hatimaye kukutwa amekufa pamoja na abiria wake wawili waliokuwa katika ndege hiyo. Mmoja wao alikuwa mchumba wake. JFK Jr., alifariki Julai 16, 1999 (tazama hizo tarehe). Baada ya kupatikana maiti yake ilichukuliwa na kuzikwa upya.
John Kennedy na Abraham Lincoln, wote, kwa nyakati tofauti, walisoma sheria na wote waliwahi kufanya kazi jeshini.
Kennedy alichaguliwa kuwa Rais Novemba 8. Lincoln alichaguliwa kuwa Rais Novemba 8. Kennedy alikuwa mtoto wa pili katika familia yake. Lincoln naye alikuwa mtoto wa pili katika familia yake.
Wote wawili walitumia majina ya babu zao. Kennedy alikuwa na watoto walioitwa Robert na Edward, kadhalika Lincoln alikuwa na watoto walioitwa Robert na Edward. Kennedy alizaa watoto wanne, na Lincoln alizaa watoto wanne.
Lincoln alikuwa na daktari wake aliyeitwa Charles Taft. Kennedy naye alikuwa na daktari wake aliyeitwa Charles Taft. Lincoln alikuwa na rafiki na mshauri aliyeitwa William Graham. John Kennedy alikuwa na rafiki na mshauri aliyeitwa Billy Graham. Inasemekana kuwa Billy na William ni majina mawili yanayotofautiana katika kuandikwa lakini si katika maana.
Chanzo kimoja cha habari kinasema kuwa mwaka mmoja kabla Lincoln hajauawa alipokea barua 80 zilizotishia maisha yake. Kadhalika, chanzo hicho hicho kinasema, mwaka mmoja kabla ya kuuawa Kennedy alipokea barua 800 za kutishia uhai wake. Barua za kennedy ni mara kumi ya zile za Lincoln, lakini namba yake ni nane.
Lincoln aliuawa mbele ya mkewe na Kennedy aliuawa mbele ya mkewe. Wake zao hawakudhurika wakati wa mauaji ya waume zao. Orodha hiyo inaweza kuendelea hadi tukajaza kurasa nyingi za gazeti hili.
Kwa kutazama hilo, tunaweza kusema kuwa hiyo ni ama sadfa, bahati au kujirudia kwa historia. Ni rahisi kuamua haraka kiasi hicho. Haijulikani kama ni historia ilijirudia ama vinginevyo, lakini angalau tunaweza kukubaliana kuwa hiyo ndiyo hali halisi na ya wazi.
Kwa kuitazama vyema historia ya Marekani, utagundua kuwa Marais wote wa nchi hiyo waliochaguliwa katika miaka inayoishia na ‘0’, ukiondoa mwaka 1840, ama waliuawa au walikufa wakiwa madarakani kutokana na kile kilichoonekana kuwa ni kifo cha kawaida.
Mwaka 1840 Marekani ilikuwa na Rais wa nane, Martin Van Buren, aliyetawala kuanzia 1837-1841. Kinachotia shauku zaidi ni kwamba matukio hayo hutokea, au tuseme yalikuwa yakitukia, kila baada ya miaka 20 kwa miongo mingi iliyopita.
Robert Ripley aliyekuwa mchoraji maarufu wa katuni na mtunzi wa kitabu cha vichekesho chenye jina
Ripley's Believe It or Not katika jalada lake, aliwahi kutaja mtindo wa kila miaka 20 ya vifo vya Marais wa Marekani kati ya mwaka 1840 na 1920 kisha, katika sentensi moja iliyo chini ya katuni moja, akaandika “…1940!?”
Aliweka alama ya ulizo kwa kuwa hakujua kile ambacho kingetokea mwaka 1940 kwa sababu kilichapishwa mwaka 1935, miaka mitano kabla ya mwaka aliouwekea alama ya ulizo (?).
Ripley alikuwa akifikisha ujumbe kamili kwa wasomaji wake, lakini kwa kuwa wengi walimchukulia kama mchekeshaji tu, walipuuza, lakini alijua yaliyokuwa yakitendeka. Alikuwa akipitisha ujumbe wake kwa njia ya vichekesho, na watu hawakuupokea.
“…1940!?” ilidokeza kwamba Rais wa Marekani aliyechaguliwa mwaka huo angekufa angali akiwa Rais wa nchi. Je, Ripley alikuwa akichekesha tu? Lilikuwa jambo la bahati mbaya au kujirudia kwa historia hata Ripley akajua kwa hakika kile ambacho kingetukia? Rais huyo hakufa akiwa madarakani? Haya ni maswali ya kitoto?
Tangu alipokuja duniani Jumatatu ya Januari 30, 1882, kupitia kwa baba na mama yake, James Roosevelt na Sara Delano Roosevelt, Franklin Delano Roosevelt hakujua kuwa Jumanne ya Aprili 4, 1933 ndipo angekuwa Rais wa 32 wa Marekani. Na hata baada ya kujua hivyo, hakujua kuwa kuna mengine ambayo hakuyajua.
Wamarekani walimchagua tena mwaka 1936 dhidi ya mpinzani wake, Alfred M. Landon. Tofauti na marais wengi wa nchi hiyo, Roosevelt alitumikia zaidi ya vipindi vitatu. Lakini hilo si muhimu kwa maana ya Robert Ripley.
Alipochaguliwa kwa kipindi cha tatu mwaka 1940 dhidi ya Wendell Willkie, akatimiza kile kilichotazamiwa. Ikajulikana kwa watu wachache sana wa ulimwengu huu waliojua siri kuwa angekufa akiwa madarakani.
Hata hivyo alisonga mbele. Ukaja uchaguzi mwingine mwaka 1944, Roosevelt akamshinda Thomas E. Dewey. Lakini hilo halikuondoa ukweli kuwa alichaguliwa mwaka 1940. Alhamisi ya Aprili 12, 1945, Roosevelt, akiwa katika kipindi cha nne cha kutawala kwake, akafa angali akiwa Rais.
Hiyo ni bahati mbaya? Au ni kujirudia kwa historia? Kama twafikiri hivyo, tuwe makini zaidi. Mwanzoni mwa karne ya 20 mwanamke mmoja wa Australia aliyeitwa Foster Turner, akiwasiliana kwa njia ya ‘upepo’ na mtu aliyeitwa Arthur Conan Doyle, walitabiri kuzuka kwa Vita Kuu I na matokeo yake. Vyote alivyotabiri vikatokea. Je, alitabiri au alijua mipango iliyokuwapo? (Soma kitabu cha Max Freedom Long kiitwacho
The Secret Science Behind Miracles).
Kitabu kiitwacho
How to Succeed cha Brian Adams © 2004 (uk. 5) kinasema hivi katika aya ya pili: “Mauaji ya John F. Kennedy yalitabiriwa na mbashiri anayejulikana zaidi Marekani (mwanamke ambaye hakutajwa jina). Alitaja kwa usahihi kabisa wakati, mahali na tarehe ambayo mauaji hayo yangefanyika. Kwa bahati mbaya, onyo lake halikusikilizwa.”
Huo tutauita utabiri? Huyu ni Rais aliyechaguliwa mwaka 1960, mwaka unaoishia na ‘0’, na huyo aliyetabiri ni Mmarekani. Tunajuaje kama huyo ambaye mwandishi Brian Adams anamwita mbashiri alijua mipango ya kuwaua watu hawa hata akajua wakati, tarehe na mahali ambapo mauaji ya Kennedy yangefanyika?
Mwanamke huyo mbashiri ambaye kitabu hicho hakikumtaja jina, siye peke yake ‘aliyetabiri’ kuuawa kwa Kennedy. Mbona Robert Ripley mwaka 1935 alitabiri kifo cha Roosevelt miaka kumi baadaye ambaye pia alifariki akiwa madarakani? Je, hakuuawa? Au tuseme hakuuawa kwa njia ile ile aliyouawa John Kennedy au Abraham Lincoln?
Kwa kutazama vile vipindi vya kila miaka 20, wanajimu wengi, au wale waliojiita wanajimu, walibashiri kifo cha Rais John Kennedy mara alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 1960. kikatokea hatimaye.
Kwa njia hiyo hiyo ilitazamiwa pia kwamba hata Rais Ronald Wilson Reagan angeuawa au kufa ‘kifo cha kawaida’ angali Rais, jambo ambalo lilikaribia kabisa kutimia.
Jumatatu ya Machi 30, 1981, akiwa na umri wa miaka 70 na baada ya kukaa ofisini kwa siku 69 tu tangu aapishwe, Rais Reagan alijeruhiwa kwa risasi tano au sita zilizofyatuliwa na John Hinckley (25) na kukimbizwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu ya George Washington kufanyiwa upasuaji.
Cha kusubiri na kutazama ni kuona kama Rais wa sasa, George W. Bush, ambaye “alichaguliwa” mwaka 2000 na kuchaguliwa tena mwaka 2004 atakumbwa na mzimu huu wa kipindi cha miaka 20. Wanaobashiri wako wapi? Kwanini wasibashiri tena?
Inasemekana kuwa huenda hilo lisimpate kwa sababu yeye na familia yote ya Bush tangu vizazi vingi vilivyopita wanajua na kushiriki mambo mengi huko Marekani. Hata George (Baba) Bush alijua, na pengine (aliandika mwandishi mmoja) alikuwa na mkono katika tukio la Reagan wakati yeye akiwa Makamu wake wa Rais.
Kwa kushangaza, marais waliochaguliwa katika miaka iliyoishia na ‘0’ wote walifariki wangali madarakani na walikufa katika miaka inayoishia na ‘1’, ‘3’ na ‘5’. Kwa hiyo, mwaka 2005 ulikuwa ndio wa George W. Bush. Lakini huo umepita.
Katika hili kuna mambo ya kutazama pia. Rais wa 12 wa Marekani, Zachary Taylor (1849-1850), alifariki dunia akiwa madarakani. Lakini hakuchaguliwa mwaka unaoishia ‘0’. Alichaguliwa mwaka 1848 na akafariki dunia mwaka 1850 kutokana na maumivu ya tumbo.
Ilisemwa kuwa ni kifo cha kawaida, lakini uchunguzi unaodokezwa na vielelezo vingi vya kihistoria ni kwamba bila kutambua Rais huyo alilishwa sumu iliyochanganywa na kemikali nyingi.
Haikuwa lazima Taylor achaguliwe mwaka ule wa ‘0’. Mwaka 1991, ikiwa ni miaka 141 tangu kifo chake, mwili wake ulifukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi upya kuthibitisha madai hayo.
Lakini, baada ya ‘uchunguzi’, serikali ya Marekani ilisema madai hayo ni ya uongo. Hakuna aliyetazamia serikali ingesema madai hayo ni ya kweli, kwani kwa kufanya hivyo ingekuwa serikali ndiyo iliyomuua Rais wao na hivyo kuharibu rekodi ya Marekani.
Tazama orodha ya marais hao ilivyo (miaka ya kuchaguliwa kwao ikiwa katika mabano). Thomas Jefferson (1800), alinusurika jaribio la mauaji dhidi yake, hatimaye alifariki dunia Julai 4, 1826. James Monroe (1820) naye alinusurika. Alifariki Julai 4, 1831.
William Henry Harrison (1840), alifariki akiwa Rais Aprili 4, 1841 kutokana na kichomi(?). Abraham Lincoln (1860), kama ilivyotajwa mara nyingi katika makala hii, aliuawa Ijumaa ya Aprili 15, 1865.
Wengine ni James A. Garfield (1880) aliuawa Julai 2, 1881. William McKinley (1900), aliuawa Septemba 19, 1901. Warren G. Harding (1920), aliuawa Agosti 2, 1923 kwa kulishwa sumu iliyowekwa katika chakula. Franklin D. Roosevelt (1940), alifariki Aprili 12, 1945 kutokana na kile kilichoitwa ‘kiharusi’, lakini kumbukumbu nyingi za matibabu yake hazijawahi kupatikana. John F. Kennedy (1960) aliuawa kwa risasi Novemba 22, 1963 na Ronald Reagan alikoswa koswa Machi 30, 1981, hata hivyo hatimaye akafariki dunia Juni 5, 2004.
Kuna marais wengine wa Marekani ambao waliwahi kunusurika. Lakini hii inaonekana kuwa ajali zaidi kuliko makusudi kama inavyoonekana kwa wengine waliotajwa hapo juu.
Hiki ndicho kile tunachokiita “historia imejirudia”, kwamba mauaji ya Lincoln na yale ya Kennedy ni historia iliyojirudia. Kuna haja ya kuyatazama mambo kwa makini zaidi ili kuona kilichofichika kuliko kuridhika na mtazamo wa juu juu.
Huenda haya niliyoandika ni ya kijinga au ya kitoto kama msomaji mmoja alivyosema, lakini kwa wanaotaka kuyaona watayaona, ila kwa wasiotaka kuyaona kamwe hawatayaona kwa kuwa tumefunikwa na kasumba ya kuona tunachoambiwa ndicho tunachopaswa kukiamini.
**************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu cha
MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754-989837, E-mail:
shao2020@yahoo.co.uk.
**************************************