Penye ukweli, uongo hujitenga
Na William Shao
Sikukusudia kuandika tena juu ya mada hii kwa sababu ziko mada nyingine nyingi zinazotuhusu wanadamu ambazo tunahitaji kuzijadili. Lakini nimeamua kuandika hii kwa faida ya wanaotaka kujua yasiyotakiwa kujulikana.
Wasiotaka yajulikane ni watu kama Leon Bahati, Joseph Ludovick, Innocent Mutahyabarwa.
Kwa jazba wamejikuta wakikwepa kujibu hoja yangu ya msingi na kudai kuwa makala za mwandishi Shao zina “mapungufu makubwa” na “hazijafanyiwa uchunguzi wa kutosha.” Udanganyifu ni njia rahisi zaidi ya kujitetea, nao wametumia njia hiyo kwa ujanja.
Hoja yangu ya msingi ni kwamba useja wa makasisi wa Katoliki hautokani na Biblia, Yesu wala Mitume wake. Ingawa wanakanusha, hawaelezi chanzo chake. Hawajaeleza waziwazi ni kifungu gani cha Biblia ambacho kwa hakika ndicho chanzo cha useja.
Inawezekana useja unalifaa sana kanisa, lakini nasema hautokani na Maandiko Matakatifu kama inavyodaiwa. Tuache itikadi, tuchambue historia bila upendeleo. Tuitendee haki historia kwa kuichambua kwa haki.
Ikumbukwe kwamba sikuushambulia Ukatoliki, bali nilifanya uchambuzi wa historia. Kwa kuwa makanisa mengine yote ya Kikristo yametokana na Kanisa Katoliki, historia yake haifai kupuuzwa.
Kihistoria, bila Kanisa Katoliki tusingekuwa na Kanisa la Kilutheri wala makanisa mengine kadhalika. Ndiyo maana naipenda historia yake rasmi na isiyo rasmi. Siyo kosa wala dhambi kuichambua. Wasiotaka ukweli wa historia ujulikane ni wale ambao ama wamejengewa kasumba mbaya au wanaofaidika na udanganyifu uliojengwa kwa karne nyingi.
Hata kitabu nilichoandika kinaitwa MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA, na wala si MIAKA 2000 YA UKATOLIKI. Nimezungumzia Ukristo, siyo Ukatoliki.
Kwa kuwa nafasi ya kujibu ni finyu, nitachambua machache kwa faida tu ya wale wanaotaka kujua uhalisi wa mambo haya. Kwa wale wasiotaka ni shauri nyingine.
Nianzie pale wanaposema naichukulia Biblia kijuu juu. Innocent anaonyesha kudai kwamba Biblia inaunga mkono makasisi kutooa, na anaungwa mkono na Bw. Leon na Ludovick.
Sikuona mahali popote katika Biblia panaposema mtu akiwa kasisi sharti asioe. Innocent anasema: “Na hata tukimsoma 1 Wakorintho 7:7…,” kana kwamba mstari huo unaunga mkono padri kutooa. (Mwenye Biblia na asome).
Tuanzie hapo. Ni kweli kwamba Biblia inasema: “...Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendeje Bwana; bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.” (1Wakorintho 7:32,33).
Sentensi hiyo ndiyo inayotumika kama kigezo cha useja? Kama hivyo ndivyo, hiyo haijaelezwa kuwa ni lazima, bali ni hiari tu. Ni nani anayeweza kudai kwa dhati kuwa sentensi hiyo ndicho kigezo cha useja katika kanisa?
Hata kama ndivyo, Biblia inasema huna hatia ukioa. Kwanini makasisi wakioa kanisa linawatia hatiani? Ingawa katika Ukatoliki kasisi akioa ni hatia na anaweza kutengwa, Biblia inasema hana hatia akioa wala hatendi dhambi.
Kwa kuonyesha tu kwamba hilo ni pendekezo, Biblia inasema hivi: “Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia ... Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi ...
“Lakini mtu awaye yote akiona ya kuwa hamtendei mwanamwali wake vipendezavyo, na ikiwa huyo amepita uzuri wa ujana wake, na ikiwapo haja, basi, afanye apendavyo, hatendi dhambi; na awaruhusu waoane.” (1 Wakorintho 7:28, 35, 36).
Sivyo Biblia isemavyo? Au kuna maana nyingine ya maneno hayo? Kudai kuwa Biblia inasema hivyo ndiyo kuichukulia kijuu juu? Kama watu hawa ni wasomaji wa Biblia, ni kweli kwamba vifungu hivyo hawakuwahi kuvisoma?
Yesu mwenyewe, wakati akijibu maswali ya Mafarisayo, alisema: “…Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si mwili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.” Mathayo 19:4-6.
Katika Biblia, ndoa huchukuliwa na kuheshimiwa kama zawadi safi na takatifu kutoka kwa Mungu, na Mungu huzibariki ndoa kuwa ni kitu chema, kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Mithali 18:22, kwamba:
“Apataye Mke apata kitu chema; naye ajipatia kibali kwa Bwana.” Kwa kutumia kanuni ya mantiki tuseme kwamba mapadri hawana kitu chema, wala kibali kutoka kwa Bwana? Je, Biblia wanazosoma wao hazina vifungu hivi?
Zaidi ya hilo, inaelezwa kuwa ni “afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwezake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kimwinua” (Mhubiri 4:9, 10 na 11)
Ndiyo maana kuna mapadri wengine (si wote) huanguka katika zinaa na wala hawana wa kuwainua wala wa kuwazuia wasiangukie tena huko. Kuna wanaotumikia vifungo magerezani kwa ajili hiyo.
Mungu alipomuumba mwanadamu wa kwanza mwanamume, hakukusudia aendelee kuishi peke yake. Ingawa alikuwa akimtafutia mwenza wake, hakumletea mwanamume mwenzake, bali alimtengenezea mwanamke----mke wake.
Baada ya kumuumba mwanadamu katika Bustani ya Edeni, “Bwana Mungu akasema, Si vyema mtu huyo awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye … na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.
“…Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” (Mwanzo 2:18, 22-24).
Mtume Petro na baadhi ya watumishi wengine wa Mungu waliokubaliwa na waliokuwa na nyadhifa na mamlaka katika kazi za Kikristo siku za mwanzo za Ukristo walikuwa ni wanaume waliofunga ndoa.
Walikuwa na wake na familia zao. Hawa walikuwa ni Wakristo halisi kuliko Wakristo wengine—au wote—wa siku hizi. Mungu hakuwakataa watu hao kwa sababu ya kuoa kwao. Je, hawakumtumikia Mungu vyema kwa sababu ya ndoa zao? Yesu aliwatenga?
Ni padri gani, au Papa gani, anayeweza kujilinganisha na Petro katika huduma za Kikristo? Petro alikuwa na mke, na bado Yesu alimkubali. Tena Yesu alimtembelea nyumbani kwake. Petro angerudi leo na kuingia Kanisa Katoliki na akaamua kuoa wangemvumilia?
Wale ambao leo wanadai kuwa wanamtumikia Mungu kwa kutooa ni watakatifu kuliko Mtume Petro? Mungu anawakubali watu hao kuliko alivyomkubali Petro?
Biblia inasema: “Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.” (Mathayo 8:14)
Haiwezekani Petro akawa na mkwe na wakati huo huo asiwe ameoa mke. Hata mitume nao walikuwa wameoa. Hawakulazimishwa kuwa waseja ili waweze kushiriki katika kazi zao za utume.
Kitabu cha Matendo 21:8-9 kinasimulia hivi: “Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.
“Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.” Je, mtumishi huyo alikuwa na mabinti aliowapata kutoka wapi kama hakuwa na mke aliyemzalia watoto hao kupitia njia ya ngono?
Ingawa Kanisa Katoliki ndilo linalosisitiza makasisi wake wasioe, ukweli wa kihistoria ni kwamba kuna mapapa waliokuwa wameoa—nasema mapapa—si makasisi wa kawaida au viongozi wa kanisa Katoliki wa vyeo vya chini. Hawa walikubaliwa na kanisa licha ya kuoa kwao.
Hata baadhi ya wengine ambao hawakuoa walikuwa na mahawara, vimada na watoto waliozaa kwa siri. (tazama kitabu changu, MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA). Kitabu hicho kinawataja mapapa waliooa, idadi ya watoto waliozaa na hata watoto wa mapapa ambao wengine walitawazwa kuwa mapapa kama baba zao.
Wanaobisha wanaweza kusema kwanini kuna mapapa waliokuwa wameoa? Kwanini Ukatoliki uliwakubali watu wa aina hiyo kwa zaidi ya karne 12 na kisha ukawakataa baadaye? Kwanini haukuwakataa tangu Ukristo ulipoanza kama chanzo chake ni Ukristo?
Kwanini kuoa kwao kulikuwa halali kwa zaidi ya miaka 1,200 lakini kukawa haramu kwa kipindi cha miaka mingine 800 hadi leo? Ninayouliza hapa ni ile aina ya maswali ambaye wengine wanasema sijui ninachouliza. Lakini wanaweza kuyajibu hayo bila kuzunguka-zunguka?
Kwanini makasisi walikuwa wakioa lakini hatimaye Kanisa likaamua wasioe tena baada ya karne nyingi baada ya Kristo? Kama kuna neno la Mungu lililowaambia mapadri wasioe, neno hilo halikujulikana kwa miaka yote 1,200? Mh!!?
Haya ndiyo maswali ambayo Leon anasema nikiwa mwandishi ninatakiwa kufanya uchunguzi wa mambo kwa “kutumia hoja zenye uhakika”. Ilinichukua miaka tisa kukamilisha kitabu hicho nikichunguza kwa makini kila habari niliyoiingiza kitabuni.
Leon anadai kuwa shutuma zangu hazikufanyiwa uchunguzi wa kutosha kiuandishi. Lakini yeye mwenyewe nilipompa vielelezo na kumuuliza maswali alishindwa kunijibu. Hii ilikuwa ni siku mbili kabla gazeti hili halijachapisha makala yake ya UKATOLIKI NI USIKU WA GIZA KWA SHAO (RAI No. 688).
Alipoandika kuwa “…hakuna jambo ambalo unaweza kuuliza Kanisa Katoliki ukakosa jibu” hakujua nilichokwisha kufanya. Alimaanisha kuwa Kanisa lina majibu ya maswali yote? Kama ni kweli, basi wao wanaificha dunia kinachotendeka kwa maslahi wanayoyajua.
Nikiwa mwandishi niliwahi kuuliza maswali mengi ya aina hiyo lakini nikaambulia majibu ya ‘kuzunguka mbuyu’. Baadhi ya majibu ya aina hiyo ninayo kwenye miakanda ya vinasa sauti. Hiyo ni sehemu ya utafiti wangu.
Majibu mengine hawana uhakika nayo—au pengine hawana majibu au labda hawataki kusema kweli. Tazama majibu kwa maswali fulani waliyoulizwa Padri Paul Haule, Padri Benedict Shayo na Father Francois wa Jimbo Kuu Dar es Salaam.
Walipoulizwa jambo fulani wanaloshikilia sana kiimani linamaanisha nini na kwanini wanaliheshimu sana, viongozi hawa wa kanisa hawakuwa na jawabu la kuridhisha. Walijibu hivi: “…hatuna uhakika …tunafanya kimazingira na mazoea.”
Tazama jawabu lingine. Padri Haule alipoulizwa msimamo wake kuhusu jambo fulani, alijihami hivi: “Jibu ninalotoa siyo kwamba linapingana na fundisho la msimamo wa dini ya Katoliki…”
Hicho ndicho kile Leon anadai kuwa “…hakuna jambo ambalo unaweza kuuliza Kanisa Katoliki ukakosa jibu”? Inawezekana ni kweli huwezi kukosa jibu, lakini ni majibu yanayokwepa ukweli usijejulikana ukaharibu mustakabali uliokusudiwa.
Ni rahisi kuelewa msimamo wa mtu anayetoa majibu ya aina hiyo? Majibu hayo nimeyachapisha katika kitabu changu katika kurasa za 11, 12, 13, 30 na 31.
Sehemu ya majibu haya yalichapishwa katika gazeti ‘Mtanzania Jumapili’ (Des. 22, 1996) na magazeti mengine niliyowahi kuandikia. Kwa hiyo si kweli kwamba Kanisa lina majibu yote.
Hata Ukatoliki wenyewe unakiri waziwazi kwamba useja wa Kikatoliki haupendekezwi na Biblia. Mwaka 1967, Papa Paul VI (1897-1978)—au kama ndugu na rafiki zake wa eneo la Concesio, Italia walivyomjua, Giovanni Battista Montini, kwa mujibu wa jarida la Kikatoliki, Priestly Celibacy (Ijumaa ya Juni 23, 1967), alikiri hivi:
“Agano Jipya ambalo ndilo hutoa mafundisho ya Kristo na Mitume wake …halidai useja wa kushurutishwa kwa wahudumu wa kanisa …Yesu mwenyewe hakuweka jambo hilo kama sharti la kuwachagua Mitume wake Kumi na Wawili, wala Mitume walioongoza Ukristo katika zile siku za mwanzo hawakuwalazimisha watu wasioe ili wawe watumishi …Agano Jipya halilazimishi useja kwa wahudumu wa makanisa.”
Hayo ni maneno yalitamkwa na Papa ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani. Wazia ikiwa maneno hayo yangetamkwa na mtu mwingine jinsi ambavyo angeshambuliwa. Silaha ya kwanza kutumiwa ni madai ya “hakufanya utafiti” na “ana mapungufu.”
Nina imani Leon, kwa kadiri nimjuavyo, hajasoma jarida hilo la Kikatoliki lenye picha ya Papa juu kabisa ya ukurasa wa tatu. Sishangai kuwa yeye na wenzake angempinga Papa Paul VI.
Kwa Innocent, pengine, atasema kielelezo hicho Priestly Celibacy siyo kielelezo cha “historia halisi ya Kanisa Katoliki” kama alivyotaja katika makala yake katika RAI. Lakini hilo ni jarida la Kikatoliki lililomnukuu mkuu wa Ukatoliki Duniani. Watadai kuwa Habari ya jarida hilo haikufanyiwa uchunguzi? Au ina mapungufu?
Turejee Biblia. Maelekezo ya mtume Paulo kwa Timotheo juu ya kuwekwa rasmi kuwa waangalizi wa Wakristo, au mapadri, au maaskofu, hudhihirisha jambo hili:
“Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha ... Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote.” (1 Timotheo 3:2, 4, 11).
Kama kuna masharti aliyotamkwa Mtume Paulo ndiyo hayo. Lakini katika masharti hayo yote, ingawa hakuna hata moja linalomlazimisha askofu kuoa, hakuna hata moja linalomkataza asioe kwa ajili ya utumishi wake akiwa katika cheo cho chote cha utumishi wa kanisa katika Ukristo.
Mtume Paulo alionyesha tu kwamba ‘askofu’ hapaswi kuoa wake wengi, lakini haijatamkwa popote katika Biblia kwamba kasisi—au tuseme askofu—hapaswi kuoa kamwe ili aweze kumtumikia Mungu.
Anawajibika awe mume wa mke mmoja. Ikiwa amefunga ndoa, anapaswa kuwa na mke mmoja tu----wala si kutooa kamwe. Kifungu kinachofuata ndicho ambacho hudaiwa kuwa chanzo cha useja katika nyadhifa za kanisa. Lakini kisome kwa uangalifu mkubwa—tena mkubwa sana.
“Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karamu yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane. Ni heri wakae kama mimi nilivyo.” (1 Wakorintho 7:7, 8).
Ukiishia hapo (yaani kusoma kijuujuu) unaweza kushawishika kuwa kifungu hicho kinatetea useja. Lakini tuwe waangalifu zaidi katika kusoma.
Je, hilo ndilo neno linalochukuliwa kama chanzo cha useja katika nyadhifa za Kanisa? Huenda. Lakini Kanisa halijawahi kutamka waziwazi kuwa hicho ndicho chanzo. Haijawahi kuandikwa popote kuwa hiyo ndiyo hali.
Tuwe wachanganuzi zaidi. Paulo alikuwa akiwalenga nani? Mapadri? Maaskofu? Papa? La hasha! Alikuwa akiwaambia “watu wote…” Kama neno hilo ndilo chanzo cha useja huo, kwanini leo inakuwa ni makasisi peke yao badala ya “watu wote…”?
Kama linachukuliwa hivyo, ni kwanini jambo la kutooa linasisitiziwa makasisi peke yao lakini lisisisitizwe kwa “wale wasiooa bado, na wajane” kama Biblia inavyosema? Tazama Paulo alivyosema: “…Nipendalo.”
Hilo halikuwa sharti. Lilikuwa pendekezo (apendalo). Kwa hiyo hata Paulo angekuchukua utumike katika kazi fulani, na ikatokea kuwa umeoa ukiwa katika kazi hiyo, hangekutenga kama Kanisa Katoliki linavyofanya.
Hata kama makasisi ni watu ambao ni “wasiooa bado”, Biblia haiwazuii kuoa. Kwanini kanisa linakasirishwa kasisi anapooa? Sasa utaona kuwa siyo makasisi walioambiwa maneno hayo. Sawa!
Tuchukulie kuwa wao ndio walioambiwa, na kwamba hicho ndicho chanzo cha useja katika Ukatoliki. Kama tutakubaliana hivyo basi hoja za msingi ama zimesahaulika au zimepigwa chenga.
Hata ingekuwa walioambiwa maneno hayo ni makasisi, pale mwanzoni Mtume Paulo aliwaambia Wakorintho hivi: “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. (1 Wakorintho 7:1-2).
Hakuishia hapo. Alifafanua kwa kina zaidi. Katika mstari wa tisa anasema, “Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.”
Ni kweli kwamba mapadri hawagusi wanawake? Hawawaki tamaa? Hawazini? Vyovyote iwavyo, hata kama hawawaki tamaa au hawazini, katika Maandiko Matakatifu haijasemwa kwamba kutooa ilikuwa amri. Ni pendekezo tu. (katika kitabu changu nimeorodhesha makasisi waliokamatwa ugoni na kesi dhidi yao)
Akiuweka ujumbe wake katika hali ya kueleweka zaidi, Mtume Paulo anasema: “Lakini nasema hayo, kwa kutoa idhini yangu, si kwa amri.” (1 Wakorintho 7:6). Utaona kuwa yote hayo ni idhini tu, si amri.
Hakuna amri iliyotolewa. Isitoshe hiari hiyo haikutolewa kwa makasisi, bali ni wale wasiooa bado na wajane. Pengine makasisi nao wanaingia katika fungu hilo, lakini wasiooa bado na wajane si makasisi tu.
Kwanini leo Makanisa yanatoa amri, si kwa idhini? Kwanini yanatoa amri ambayo Biblia haijatoa? Wao walizipata wapi amri hizo? Amri zenyewe zinatimiza kusudi gani? Je, wao ni matowashi?
Haya ni aina ya maswali ambayo wengine wanadai kuwa nauliza maswali nisiyoyajua na kutoa majibu nisiyoyajua vilevile. Watasema sina uwezo wa kuitafsiri Biblia. Nasema sawasawa. Lakini sivyo Biblia inavyosema?
Biblia imezungumzia matowashi. Inasema kuwa wanamume na wanawake fulani huchagua useja kwa hiari zao wenyewe. Ni kweli. Na ingefaa useja uchaguliwe kwa “idhini..., si kwa amri.” (1Wakorintho 7:6).
“Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” (Mathayo 19:12).
Labda Innocent na Leon wangetamka kuwa mapadri ni matowashi kwa maana ya neno ‘towashi’. Hata hivyo, katika Biblia, neno ‘towashi’ halijapewa uzito wa upadri wala umaana wowote kwa cheo chochote katika utumishi wa Kanisa kwa maana kumtumikia Mungu si lazima uwe kasisi.
Neno hili, ambalo kwa Kiingereza ni ‘eunuch’, limeonekana mara 18 tu katika Biblia ya Kiingereza ya ‘Revised Standard Version’. Lakini limeonakana mara chache zaidi katika Biblia za Kiswahili.
Kwa hiyo neno hilo linamaanisha mambo mengi ikitegemea fasiri ya Biblia inayotumiwa. Kwa wanaotaka kulifuatilia kwa karibu zaidi katika Biblia ya Revised Standard Version watazame aya inayofuata.
Neno hilo limeonekana mara kadhaa katika vitabu kadhaa vya Biblia (tazama katika mabano). Katika kitabu cha Esta 2:3, 14, 15; 4:4, 5 (mara tano), Isaya 56:2, 3 (mara mbili), Mathayo 19:12 (mara tano), Yeremia 38:7 (mara moja) na Matendo 8:27, 34, 36, 38, 39 (mara tano).
Katika Biblia za Kiswahili neno hilo litamaanisha mambo mengi kuanzia towashi, bikira, suria(?) au mjakazi(?). yote niliyoeleza hapo juu yananishawishi kudai kuwa useja wa makasisi katika Ukatoliki haujatokana na mapendekezo ya Biblia. Umechochewa na mambo ya kilimwengu zaidi kuliko ya kiroho.
Useja ulikotoka na chanzo chake
Angalau sasa tunaweza kukubaliana kuwa hakuna kifungu chochote cha Biblia kinachoweza kudaiwa kuwa ndicho chanzo cha useja katika Ukatoliki.
Wamedai sikufanya uchunguzi, na kwamba nimeonyesha mapungufu makubwa. Nimetumia vielelezo vyote nilivyotafiti. Pengine walitaka nikafanye utafiti mbinguni pia? Kama huwezi kuutafuta ukweli pale ulipo, ni wapi utatazamia kuupata?
Ludovick akaandika: “…Kila mara (Shao) hukata rufaa kwenye mamlaka za kitaaluma kama vitabu vya Encyclopedia, Dictionaries na Comentaries na yeye hudhani vitabu hivyo hutoa mafundisho ya Kanisa Katoliki.”
Ninavyoamini ni kwamba silaha bora zaidi ya mtafiti na mchambuzi yeyote ni marejeo anayotumia. Ludovick anamaanisha nisitumie marejeo katika kufanya utafiti?
Wanataka kumaanisha nini? Alitaka utafiti niufanyeje kama si kwa kutumia “mamlaka za kitaaluma” kama anavyodai? Au anasema kitabu kikishatoa “mafundisho ya Kanisa Katoliki” ndicho kinachofaa kutumika kama marejeo na kwamba vingine tofauti na hivyo havifai?
Sawa. Nitaepuka vielelezo vingine vyote na nichambue vile vya “mafundisho ya Kanisa Katoliki” (Ludovick) na vile vya “historia halisi ya Kanisa Katoliki” (Innocent).
Kwa kuikwepa hoja ya msingi, Ludovick aliandika: “(Shao) Hajaona vipeperushi vya Vatican II. Mtakuwa mashahidi jinsi atakavyomwaga manyanga siku akivipata” na sehemu nyingine akasema (Shao) hajasoma barua ya Papa.
Hili si tu kwamba lilinishangaza, lakini halieleweki. Biblia haina cheo wala barua ya Papa. Sasa anataka kusema Papa ameamua kuandikia Wakristo barua baada ya kuona kuwa zile nyaraka za Mitume kama Paulo na Petro hazifai na sasa tuache kuzisoma na badala yake tuanze kusoma zile za Vatican?
Kwa upande wa Leon kwa kuwa ni mwandishi wa habari, namhimiza mchambuzi zaidi wa mambo badala ya kudhani yale anayoyajua ndiyo hayo tu anayopaswa kujua. Anadhani anayojua yanatosha kwa hivyo hahitaji kujua mengine.
Marejeo mengi ya Kikatoliki yanadokeza kwamba useja wa makasisi ulichochewa zaidi na falsafa za kipagani kuliko itikadi za kidini. Na hapa natumia vyanzo vya Kikatoliki tu.
Profesa Jorge Ponciano Ribeiro (Mkatoliki) wa Chuo Kikuu cha Brasilia, Brazili, aliandika hivi: “Useja ulianzishwa na Kanisa ili kuepuka matatizo kati ya Kanisa na urithi wa makasisi, wala si kwa sababu ya kwamba Neno la Mungu linaweza kutangazwa vyema zaidi na wale ambao hawajiingizi katika mahusiano ya ngono.” (‘A Study On the Effect of the Hierarchic Position’ © 1980).
Madai ya profesa huyo yanaungwa mkono na David Rice, mtafiti wa historia ya dini na mwandishi wa kitabu ‘Shattered Vows’. Rice aliwahoji makasisi wengi duniani walioamua kuoa. Alichapisha masaibu yao katika kitabu hicho) Katika ukurasa wa 161 wa kitabu chake anaandika: “Kwa kiasi kikubwa useja wa Kikatoliki umetokana na upagani…”
Mwanatheolojia Mkatoliki, Edward Schillebeeckx, katika kitabu chake kiitwacho ‘The Church with a Human Face’, ameandika mengi anayosema ni matokeo ya utafiti wake. Katika ukurasa wa 297 anaandika hivi:
“Kimsingi kuna aya mbili katika Agano Jipya (Mathayo 19:12 na 1 Wakorintho 7:7) zinazodaiwa kuwa msingi wa useja katika Ukatoliki …Lakini Kanisa lenyewe halijawahi kudai kuwa huo ndio msingi wa useja wa makasisi wake…”
Kitabu History of Monogamy kinasema katika mwaka 1022 (karne ya 11) Papa Benedict VIII alipiga marufuku ndoa za makasisi …kuharamishwa kwa ndoa hizo kulitokana na agizo la Biblia.
“Sababu iliyojificha nyuma ya kitendo hicho ni kuihami mali ya Kanisa dhidi ya urithi wa makasisi. Hawakunukuu kifungu chochote cha Biblia na kudai kwamba ndicho kilichowasukuma kufikia uamuzi huo …Hili (la kuharamisha ndoa za makasisi) halikuwa na uhusiano wowote na maadili.”
Mwaka 1045 Papa Boniface IX aligundua hilo. Aliamua kuachana na useja. Rejea kilichotamkwa na Papa Paul VI hapo juu mwaka 1967 aliposema “Agano Jipya …halidai useja wa kushurutishwa kwa wahudumu wa kanisa” wala “Yesu mwenyewe hakuweka jambo hilo kama sharti la kuwachagua Mitume wake 12…”
Hayo aliyatamka asubuhi. Kwa kuona kuwa hakuridhika, baadaye jioni siku hiyo hiyo akarudia kusema: “Agano Jipya halilazimishi useja kwa wahudumu wa makanisa.”
Hayo siyo maneno ya kasisi wa kawaida, bali ni ya Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani. Yeye ndivyo alivyosema, mbona wengine wanakataa. Hawakulisoma hilo? Wanaopinga wanafanya hivyo kwa kutojua. Hawaichambui historia?
Chanzo kingine cha Kanisa Katoliki kinachoaminika zaidi ni kitabu kiitwacho ‘The Catholic Encyclopedia’. Kinasema hivi: Katika ile karne ya kwanza ya Ukristo, “Hatujaona mahali popote katika Agano Jipya dalili yoyote inayoashiria kuwa useja ulifanywa kuwa jambo la lazima kwa Mitume wale waliofanywa kuwa watumishi wa Mungu.”
Hicho ndicho kitabu kinachoandikwa na Ukatoliki kwa maslahi ya Ukatoliki, lakini kinakiri waziwazi kwamba Agano Jipya halina dalili yoyote ya kwamba useja ni jambo la lazima kwa Mitume wa Mungu.
Kitabu hicho kinachapishwa na kampuni ya ‘Encyclopedia Press’ ya nchini Marekani. Kwa kuwa nilivutiwa nacho, niliamua kusoma historia yake. Toleo la kwanza la ‘Catholic Encyclopedia’, likiitwa ‘The Old Catholic Encyclopedia’, lilipatikana mwaka 1907. Lakini mkusanyiko wa vitabu vyote vya ‘encyclopedia’ hiyo vilikamilika mwaka 1914.
Uandishi (utafiti) wa ‘encyclopedia’ hiyo ulianza Januari 11, 1905 ukisimamiwa na wahariri watano ‘makini sana’ walioheshimiwa na kuidhinishwa na Kanisa Katoliki ambao wangesimamia upatikanaji na uchapishaji wa habari zake.
Watu hao ni Charles Herbermann (Profesa wa Kilatini na Mkutubi wa Chuo cha Jiji la New York), Edward Pace (Profesa wa Falsafa katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Amerika Jijini Washington), Conde Pallen (Mhariri), Kasisi Thomas Shahan (Profesa wa Historia ya Kanisa Katoliki) na Kasisi John Wynne (mhariri wa jarida la Kikatoliki lililoitwa ‘The Messenger’).
Ukiipekua historia zaidi, utagundua kuwa Kamusi ya Kikatoliki inayoitwa ‘Dictionary of Catholic Theology’ inathibitisha kuwa katika karne ya nne, “Ushahidi wa kale zaidi wa sheria ya useja wa makasisi ni Kanuni ya Kanisa (Canon 33) ya Baraza la Elvira [Spain], mnamo mwaka 300 baada ya Kristo.”
Kamusi hiyo inadokeza kwamba useja haukuwemo wakati wa Yesu na hata miaka 300 baadaye.
Baada ya ubishi wa muda mrefu, inasema ‘A Catholic Dictionary’ © 1997 iliyohaririwa na Donald Attwater (Mkatoliki) ambayo ni chanzo kingine cha Kikatoliki, “Baraza la Nicaea lililokaa mwaka 325 lilikataa kuamuru kupitishwa kwa sheria hii [Elvira Canon 33] kwa Kanisa lote.”
Hapa nagusa tu vile vyanzo vya habari vya “historia halisi ya Kanisa Katoliki” (Innocent) na vya “mafundisho ya Kanisa Katoliki” (Ludovick) na kuvichunguza (Leon). Ukisoma kitabu kiitwacho Cyclopedia of Biblical, Theological, and Ecclesiastical Literature utagundua mengi zaidi.
Katika aya moja (uk. 68) kinasema hivi: “Kwa karne kadhaa suala la useja wa makasisi lilikuwa mada ya ubishi usiokwisha ndani ya Kanisa.
The Catholic Encyclopedia iliyotajwa hapo juu ikaelezea yaliyotokea katika karne ya 12. Inasema: “Hatimaye, katika mwaka wa 1123, wakati wa utawala wa Papa Callistus II, katika mkutano mmoja uliojulikana kama First Lateran Council, pendekezo (la useja) liligeuzwa kuwa sheria, na likasisitizwa zaidi liendelee kuwa amri ya Kanisa.
Kitabu nilichotaja hapo juu, ‘Cyclopedia of Biblical, Theological, and Ecclesiastical Literature’, kinasema: “Katika Baraza la Trent (1545-63) maaskofu kadhaa, na mfalme Charles V (aliyetawala Rumi mwaka 1519-1558), aliunga mkono kulegezwa kwa sheria ya useja. Lakini alipingwa.”
Ukweli ulio katika historia ni wa kutisha zaidi utakapozidi kuuchimbua. Kuna vielelezo vingi vinavyozungumzia jambo hilo na kuhitimisha kuwa useja hautokani na Biblia. Lakini ikiwa useja wa kulazimishwa haujatokana na Yesu Kristo wala mitume wake, unatokana na nini?
Pengine hili ni swali la kitoto, wanaweza kulijibu kiutu uzima? Siulizi na kujijibu mwenyewe, bali natumia vielelezo.
“Nyakati za wapagani useja ulikuwa ukiheshimiwa sana,” wanaandika wanatheolojia John McClintock na James Strong katika kitabu chao, ‘Cyclopedia of Biblical, Theological, and Ecclesiastical Literature’.(encyclopedia hiyo yenye zaidi ya makala 31,000 pia imo katika CD).
Kazi nyingine za marejeo zinaonyesha kuwa “zamani za Upagani” ni wakati wa Babeli na Misri ya kale. Kitabu ‘The New Encyclopedia Britannica’ kinasema: “Wakati wa kuanza kwa ustaarabu mkubwa wa zamani za kale, useja uliibuka katika mazingira mengi tofauti.”
Ulikuwa, kwa mfano, unahusishwa na kumwabudu mungu jike wa Misri aliyejulikana kama Isis, ambaye alikuwa mungu-jike wa uzazi wa Misri. Kama ‘Britannica’ inavyodokeza: “Kujizuia kufanya ngono lilikuwa takwa kamili la wale waliosherehekea miujiza yake.”
Kwa kuongezea, Alexander Hislop anasema hivi katika sura ya sita ya kitabu chake, The Two Babylons: “Kila mwanazuoni anajua kwamba ibada ya Cybele, mungu-jike wa Babeli, ilianzishwa huko Rumi ya Kipagani, ilianzishwa katika muundo wake wa kizamani, na ilianzishwa na kasisi kapera (mseja).”
Cybele, mungu-jike wa asili na uzazi, ambaye aliabudiwa sana katika Rumi kama Mama Mkuu wa Miungu (habari hii inafanana na ile ya Bikira Mariamu?), dhehebu lake liliongozwa na makasisi waliokuwa matowashi waliojulikana kama Corybantes.
Ili kuwa kasisi katika dhehebu hilo, sharti la kwanza la kutimizwa ni kutooa—yaani kuwa mseja. Hiyo ndiyo ilikuwa sifa kubwa, na pengine ya kwanza, hata kama mtu mhusika ni rijali.
Lakini ikiwa useja wa kulazimishwa katika Kanisa Katoliki ni upagani, au angalau umetokana na upagani, kwanini kwa kuiga wapagani wa kale Kanisa hilo liliamua kuanzisha useja wa kulazimishwa katika ngazi zake za utumishi wa Kanisa?
Kama mwandishi hayo ndiyo maswali ya kuuliza. Lakini kama viongozi wahusika hawawezi kujibu, tutaendelea kuchimbua vielelezo. Nilihoji haya kama nilivyoeleza hapo juu, lakini hakuna majibu ya kuridhisha niliyopata kwa watu hao.
Jambo moja la hakika ni kwamba useja wa makasisi katika Kanisa hulifanya kanisa kuwa na nguvu ya mamlaka. Hii ni kwa sababu, kwa mapadri kutokuwa na warithi katika kazi na mali zao, nyadhifa za makasisi zinaweza tu kubadilishwa kwa kutumia mfumo wa kikanisa usioingiliana na ule wa familia za makasisi.
Hata kitabu The Catholic Encyclopedia kinakubali kwamba Rumi (Vatican) imekuwa ikishutumiwa kwa kuutumia useja kama “chombo cha kuhakikisha kasisi anakuwa mtiifu kwa Mamlaka Kuu ya Rumi”—au tuseme Vatican. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa Corybantes katika ibada za Cybele.
Hapa nimetumia vielelezo vya Kikatoliki tu ambavyo havikuandikwa na mtu wa madhehebu mengine yoyote (isipokuwa, pengine, ‘The New Encyclopedia Britannica’). Ningejumlisha na marejeo mengine ingetosha hata kuandika vitabu vitano juu ya mada hiyo moja.
Ingawa wako makasisi wengi, ni wachache, au hakuna yeyote, anayeweza kueleza asili hasa na maana halisi ya useja wa kulazimishiwa na dini. Hata wale wanaojua ukweli wa mambo hawataki kuusema ukweli huo wasijeonekana kuwa wako kinyume na makanisa yao.
Majibu utakayoambulia ni kama “…hatuna uhakika …tunafanya kimazingira na mazoea” au “Jibu ninalotoa siyo kwamba linapingana na fundisho la msimamo wa dini ya Katoliki…” Hayo ndiyo majibu unayoweza kuambulia.
Kwa wengine kama Ludovick na Innocent naweza kunyamaza kwa sababu sijui nyadhifa zao, lakini kwa Leon ninayemjua kama mwandishi namshauri aepuke sana kuufunika uandishi wake na itikadi za dini au siasa. Aandike ukweli hata kama unasuta imani yake—ili mradi ni ukweli.
Historia ya dunia yetu imefunikwa na wingu kubwa. Ni kazi ya waandishi kujitahidi kuondoa wingu hilo, lakini kwa Leon inaonekana kuwa ni kazi yake kuendeleza wingu hilo.
Mambo ya kweli ni marahisi sana kueleweka mara ukweli unapogunduliwa; kazi ngumu peke yake iko katika kuugundua ukweli huo. Wanaoficha ukweli watakuwa wakali kuliko nyuki mara ukweli wanaouficha unapofichuka. Haitashangaza kwamba wanaoufunika watakasirika sana utakapofunua wanachofunika.
****************************************************
William Shao ni mwandishi wa habari na mwandishi wa kitabu MIAKA 2000 YA UKRISTO: HISTORIA ILIYOPOTOSHWA. Anapatikana kwa simu 0754 989 837, e-mail: shao2020@yahoo.co.uk.
No comments:
Post a Comment